31.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 20, 2024

Contact us: [email protected]

UNATUMIA 60,000 BODABODA TU, MSHAHARA WAKO 300,000 UNA AKILI? – 2

Na ATHUMANI MOHAMED

KARIBUNI katika safu yetu inayozungumzia mambo ya msingi kuhusiana na maisha yetu ya kila siku. Kwa wadau wa kila siku bila shaka kuna mengi waliyojifunza kuhusu maisha na mafanikio.

Tunaendelea na mada yetu iliyoanza wiki iliyopita, ambayo naamini inatoa mwanga wa maisha yetu. Tunaangalia namna ambavyo watu wengi wanapenda kufanya mambo kwa kuwafurahisha watu bila kuangalia madhara yanayoweza kutokea kwenye maisha yao.

Kwa kuanzia nilianza kwa mfano wa mfanyakazi mwenye kulipwa mshahara wa 360,000 (baada ya makato yote) na matumizi yake, ambapo tuliona kwa mfano mtu mwenye mazoea ya kutumia bodaboda, anaweza kutumia karibu 60,000 kwa mwezi kwa usafiri huo pekee.

Sasa tunaendelea…

  • Unakula nini?

Je, mlo wako ukiwa kazini ni wa namna gani? Watu wengi makazini wanapenda kula vyakula vya haraka (fast food), siyo kwamba vyakula vingine hakuna, ila wanafanya hivyo kwa kufuata mkumbo.

Mathalani mwenzake akiagiza chips kuku, chips mishikaki au chips mayai na yeye anapenda kuiga. Kwa bei ya kawaida kwenye miji mingi, chips mayai ni kuanzia 2,000 – 2,500.

Chips kuku ni 3,000 – 4,000, chips kavu ni kuanzia 1,500 – 2,000, mishikaki ni 500 – 1000 wakati kuku wa kukaanga kwa kipimo cha robo ni kati ya 2,000 – 3,000.

Angalia gharama ilivyo juu. Kwa kawaida hapo, kama ukila chips na kitoweo chochote lazima bei haitakuwa chini ya 3,000, utaagiza na juisi ya 1,000 na maji jumla ni 5,000 au zaidi.

Pamoja na gharama hiyo kubwa, unapata nini kwenye chips kuku? Wataalamu wa afya kila siku wanaeleza madhara yanayopatikana kwa vyakula vya haraka hasa vinavyotumia mafuta mengi, lakini chips zimetajwa moja kwa moja kama moja ya vyakula vya hatari vinavyosababisha magonjwa mengi.

Unadharau ugali dagaa ambao unauzwa kwa bei ya 1,500 – 2,000 ambayo utapewa na matembele, yenye bei ndogo lakini ukiwa na thamani kubwa kwenye mwili wako.

Achana na mazoea.

Mwingine ataingia mgahawani, atamwangalia mwenzake anaagiza nini, kama akiona wengi wanakula wali kuku, wali samaki ambavyo ni 5,000 – 6,000 na yeye anaagiza, wakati ukweli ni kwamba kwa mshahara wake anapaswa kula chakula cha 2,000 tu.

Siyo kama nafundisha watu kuwa wabahili, la hasha lakini ukweli ni kwamba ukitaka kuwa na maisha bora kuna mambo mazuri inabidi uyaache kwa wakati fulani ili kujenga maisha bora mbele yako.

  • Unazingatia unavyokunywa?

Mwingine anaweza asione kama ni jambo lenye umuhimu, lakini unafikiria kuhusu ubora na gharama wa vinywaji unavyotumia kwa siku? Baadhi ya ofisi zina utaratibu wa kuweka maji ya kunywa ya bure, lakini nyingi hazina utaratibu huo kwahiyo kila mfanyakazi hujitegemea.

Je, kwa siku unatumia maji ya shilingi ngapi? Kwa wastani mtu anaweza kutumia maji lita moja na nusu mpaka mbili mchana. Maji hayo kwa gharama ya kawaida kabisa yatakugharimu siyo chini ya 1,500.

Mwingine hawezi kumaliza mchana wake bila soda au juisi za viwandani. Anaweza kutumia labda 1,500, ukichanganya na maji jumla ni 3,000 kwa siku moja.

Inakugharimu nini kubeba chupa yako ya lita mbili na kwenda nayo kazini kwako? Gharama ni kuchemsha na kubeba tu. Lakini mwingine anaogopa. Unahofu nini?

Beba maji yako, nenda tumia ofisini na uokoe 1,500. Kama ni lazima kunywa juisi ukiwa ofisini, angalia msimu wa matunda, nunua ya kutosha, saga kwa brenda na ubebe kiasi unachotaka.

Maisha ni zaidi ya kuangalia watu wanasema nini. Jali yako, acha kuangalia watu wengine, maana hawatakusaidia kitu.

Maisha ni yako mwenyewe. Usikose wiki ijayo katika sehemu ya mwisho ambapo tutaangalia kwa mchangunuo wa matumizi sahihi  na yasiyo sahihi wala malengo.

Ni mimi rafiki yako katika mafanikio, Athumani Mohamed.

Wasalaam.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles