28.5 C
Dar es Salaam
Wednesday, August 17, 2022

Unajua vipi kama mpenzi wako anaridhika na wewe?

NI raha sana kuwa na mtu unayemridhia katika mahusiano yako. Mtu ambaye kwa kumridhia kwako, matendo na kauli zake zinasababisha furaha na amani katika maisha yako.

 Wengi wasio na furaha katika mahusiano, wako kwenye hali hiyo sio tu kwa sababu wanatendewa vibaya na wenzao ama wanakosa baadhi ya mahitaji muhimu. Hapana. Wengi wako hivyo kwa sababu wako na watu wasio waridhia katika maisha yao.

 Kuwa na mtu ambaye hujamridhia  wakati mwingine ni kama kula chakula ambacho sio chaguo lako. Mbali na kushiba ila hakikupi ladha na utamu stahili katika ulimi. Na kwa maana hiyo hujisikii fahari wala raha kukila.

 Mahusiano yanayotokana na maridhiano baina ya wahusika wawili, mbali na faida zingine ila pia yanasababisha furaha zaidi na hamu kubwa kwa kila mmoja juu ya mwenzake.

 Ikiwa uko na mtu iliyemridhia hata hisia na akili yako vitamtafsiri vizuri. Kwa sababu hiyo utajikuta ukiona raha kuongozana naye, kula naye pamoja, kuoga naye na hata kushiriki naye kila linalofaa.

 Kama ukiwa na mtu ambaye hujamridhia kwa kiwango stahili unaweza kujikuta hata huna hamu ya kukutana naye faragha. Unajikuta hujisikii hata kumuomba radhi ukimkosea. Unajikuta tu hata kumtambulisha kwa ndugu na jamaa huoni kama ni muhimu sana.

Swali, unajuaje kama mwenzako ameridhia kwa kiwango stahili kuwa na wewe? Unajuaje kama mwenzako hakukubali kuwa na wewe kwa sababu ya kazi ama umasikini wake tu? Unajuaje kama mwenzako kawa na wewe kwa sababu aliachwa katika mahusiano yake yaliopita hivyo akaamua kuwa na wewe kudhihirisha kuwa yeye bado ni bora na sio sababu anakupenda?

 Kwa haraka kama unataka kujua kama mwenzako kawa na wewe kwa sababu ya msukumo halisi wa hisia zake juu yako. Ebu tazama matendo na kauli zake kisha tazama mwenendo wake wa ujumla juu yako.

 Anafurahia uwepo wako? Kauli na matendo yake hata kama anazungumza na kufanya  vitu vingine na wewe, huwa vinabeba ujumbe gani?

 Mtu mwenye uzito wa mapenzi kwa mpenzi wake, jumla ya matendo yake hubeba ujumbe wa kimapenzi kwa muhusika. Mfano, akimkosea muhusika hujiona ana jukumu na ulazima wa kumuomba msamaha. Huona haja ya kufanya hivyo kwa sababu mapenzi halisi huleta unyenyekevu na huruma. Mapenzi halisi humfanya mtu ajione ana jukumu la kuhakikisha furaha na amani kwa mwenzake.

 Tafiti zinaonesha watu wengi wako katika mahusiano na watu wasio waridhia kabisa. Kwa sababu hiyo ndio maana usaliti na migogoro imekuwa mingi sana. kwa sababu hiyo ndio maana watu wengi wako katika mahusiano huku wakiwa na huzuni na hawajui kwanini hawana furaha.

 Kwa sababu ya watu kuishi na watu wasiowaridhia kwa kiwango stahili, basi hata idadi ya watu kuachana na kusalitiana imekuwa kubwa zaidi. Mtu haoni ubaya kuachana na mwenzake kwa sababu kwake kitendo hiko ni sawa na kupata uhuru wa kufurahia maisha na mapenzi.

 Mapenzi sio sehemu ya kuonyesha ufahari ama ukomando wako. Mahusiano sio sehemu ya kujaribu ama kumkomoa mtu. Mahusiano ya kimapenzi ni sehemu ya kulea hisia zako za amani na furaha. Ni sehemu muafaka kwa ajili ya kukutana na mtu ambaye anaweza kugeuka mwiba katika maisha yako hata ukaona maisha hayafai ama kukutana na mtu atakayekufanya ujivunie naye na awe mshirika mwema katika safari yako ya kupata mafanikio na amani ya kweli ya nafsi.

Instagram: g.masenga

 Mwandishi wa makala haya ni mtaalamu mbobezi wa masuala ya ushauri wa uhusiano, maisha na utulivu wa hisia ( Psychoanalyst)

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,908FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles