24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

UN yalaani mataifa ya kigeni kuingilia mzozo wa Libya

 GENEVA, USWISI

KATIBU Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres amesema uingiliaji unaofanywa na mataifa ya kigeni katika mzozo wa Libya umefika katika kiwango kibaya na kisicho cha kawaida.

Akizungumza katika mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Guterres amelaani hali inayoendelea Libya na kuelezea wasiwasi kuhusu vikosi vya kijeshi vilivyoko kwenye mji wa Sirte na eneo lililoko kati ya Tripoli upande wa magharibi na Benghazi upande wa mashariki.

‘’Mzozo umeingia katika hatua mpya, kutokana na uingiliaji wa nchi za kigeni kufikia kiwango kisicho cha kawaida, ikiwemo kuingiza vifaa vya kisasa na idadi ya mamluki wanaoshiriki katika mapigano,’’ alisema Guterres.

Hata hivyo, Guterres hakuitaja nchi yoyote ile, ingawa ametoa wito kwa jumuia ya kimataifa kutumia kila fursa kuhakikisha wanaondoa mkwamo wa kisiasa nchini Libya.

Guterres pia amezungumzia uwezekano wa kuanzisha eneo lisilo la kijeshi litakalodhibitiwa na kikosi cha Umoja wa Mataifa nchini Libya.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Heiko Maas amewaambia wajumbe wa mkutano huo kwamba upelekaji wa silaha nchini Libya umeendelea, licha ya kuwepo vizuizi vya kudhibiti kusambaa kwa janga la virusi vya corona. 

Ujerumani ambayo inashikilia urais wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa mwezi huu ndiyo ilikuwa mwenyekiti wa mkutano huo.

Maas alisema wakati nchi nyingine zinajaribu kuyaokoa maisha ya watu katikati ya janga la Covid-19, hospitali nchini Libya zinashambuliwa, huku meli, ndege na malori yenye silaha pamoja na mamluki zikiendelea kuingia kwenye miji ya nchi hiyo. 

Naye Balozi wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa, Kelly Craft alisema wataendelea kupinga uingiliaji wowote ule wa kijeshi wa nchi za kigeni nchini Libya. Aidha, Balozi wa Urusi kwenye Umoja wa Mataifa, Vassily Nebenzia alikanusha madai kwamba nchi yake inajihusisha na mzozo wa Libya. 

Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Umoja wa Falme za Kiarabu, Anwar Gargash aliliambia baraza hilo kwamba kuna takriban mamluki 10,000 wa Syria wanaoendesha operesheni nchini Libya, mara mbili zaidi ya idadi iliyokuwepo miezi sita iliyopita.

Guterres alisema kati ya Aprili na Juni mwaka huu, Ujumbe wa Umoja wa Mataifa kuhusu Libya (UNSMIL) ulirekodi visa 356 vya mashambulizi dhidi ya raia, ikiwemo vifo 102 pamoja na majeruhi 254, ikiwa ni ongezeko la asilimia 172 ikilinganishwa na kipindi cha kuanzia mwezi Januari hadi Machi.

Alisema pia takriban mashambulizi 21 yamefanyika kwenye vituo vya afya, magari ya kubeba wagonjwa pamoja na maofisa wa afya. Ugonjwa wa Covid-19 ni sababu ya kuongezeka kwa wasiwasi nchini Libya, ambapo mwezi Juni nchi hiyo ilirekodi visa 1,046 vya virusi vya corona na vifo 32.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles