Benjamin Masese -Mwanza
SHIRIKA la Umoja wa Mataifa linaloshughulika na Masuala ya Wanawake (UN Women), limewakutanisha wazee 225 maarufu wa mila kutoka mikoa tisa ikiwa ni sehemu ya kuisaidia Serikali ya Tanzania kutimiza malengo ya mikataba ya kimataifa na kikanda ya kukomesha vitendo ukatili wa jinsia na kuleta usawa ndani ya jamii.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa semina kwa wazee hao waliokutanishwa jijini Mwanza, Ofisa Elimu na Uhamasishaji kutoka UN Women, Lucy Tesha alisema wadau wakubwa wa mashirika ya kimataifa ni Serikali ambapo kwa pamoja hushirikiana katika masuala ambayo yamewekwa katika mikakati ya kimaendeleo kwa kuwafikia walengwa ambao ni wananchi.
Tesha alisema suala la ukatili wa kijinsia, mimba kwa wanafunzi na ndoa za utotoni zimekuwa jambo kubwa ndani ya jamii ambapo sababu kubwa zinazochangia uwepo wa mambo hayo ni baadhi ya mila na desturi za makabila mbalimbali.
“Kama shirika ;la UN Women ambayo tunashughulika na masuala ya wanawake, tumeona kuna haja ya kuisaidia Serikali ya Tanzania kutokomeza vitendo vya mimba za wanafunzi, ukatili wa jinsia na ndoa za utotoni, sote tunajua kila nchi imekuwa na mikakati yao ya ndani, pia yapo malengo ya kimataifa.
“Kwa Tanzania tunataka kuona wanawake wanachangia maendeleo ndani ya familia na sio tu wanaume pekee, hapa tunao wazee 225 tuliowakutanisha kutoka mikoa ya Mwanza, Tabora, Mara, Simiyu, Kagera, Shinyanga, Katavi, Geita na Manyara ambapo kila mmoja atatueleza mila na desturi zao, tutajadiliana na kuona zipi zinafaa na zipi hazifai na kuwashauri kuachana nazo.
“Kama UN Women tunataka kuona wazee hawa wawe muhimili wa ndani ya jamii katika kubadilisha fikra za wengine ili wanawake wapate usawa, mimba za kwa wanafunzi ziishe na ndoa za utoto zisiwepo tena, hatuhitaji kisikia tena ramli changanishi zinaendelea tena,”alisema.
Hata hivyo takwimu za 2015/2016 zilizowasilishwa katika semina hiyo kutoka Ofisi ya Takwimu nchini (NBS) zimeonyesha mikoa inayoongoza kwa vitendo vya ukatili ni Mara na Shinyanga zikiwa na asilimia 78, Tabora 71, Kagera 67, Geita 63, Simiyu 62, Kigoma61, Mwanza 60, Njombe53, Dodoma na Katavi 50.
Mikoa mitatu inayoongoza kwa ndoa za utotoni ni Shinyanga asiliamia 59, Tabora 58 na Mara 54 ambapo mikoa inayoongoza kwa mimba za shuleni ni Katavi asilimia45, Tabora 43, Dodoma 39, Morogoro 39,Mara na Shinyanga zikiwa na asilimia 37.
Alisema shirika hilo limeamua kujikita kwa wazee hao kwa kuwa asilimia kubwa ya jamii bado inawaamini hivyo ni rahisi kupeleka elimu katika maeneo wanayoishi kwa lengo la kutokomeza ukatili, ndoa za utotoni na mimba kwa wanafunzi.