30 C
Dar es Salaam
Friday, January 27, 2023

Contact us: [email protected]

UMUHIMU WA MWANAMKE WAANIKWA

Wanawake wakiingia katika Uwanja wa Mwembeyanga Temeke Dar es Salaam jana wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani.

Na WAANDISHI WETU-DAR ES SALAAM

SERIKALI, vyama vya siasa na wadau mbalimbali, wametoa matamko kuhusu Siku ya Wanawake Duniani iliyoadhimishwa jana.

Akizungumzia siku hiyo, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, alisema Serikali inatambua ukatili dhidi ya wanawake bado ni tatizo ambalo linaathiri ushiriki wao katika shughuli za uchumi na jamii.

Alisema katika kukabiliana na tatizo hilo, Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeandaa mpango kazi wa taifa wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto.

“Serikali inatambua ukatili dhidi ya wanawake bado ni tatizo kubwa ambalo linaathiri ushiriki wao katika shughuli za uchumi na jamii.

Katika kukabiliana na tatizo hilo, Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeandaa mpango kazi wa taifa wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto (2017/18 – 2021/22) ambao ulizinduliwa Desemba 13, mwaka jana,” alisema.

Alisema kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu, ‘Tanzania ya Viwanda; Wanawake ni Msingi wa Mabadiliko ya Uchumi’, imetolewa kutokana na kaulimbiu ya kipaumbele ya Umoja wa Mataifa mwaka huu katika mkutano wa 61 wa Hali ya Wanawake Duniani (CSW).

“Kaulimbiu hii ya “Tanzania ya Viwanda: Wanawake ni Msingi wa Mabadiliko ya Uchumi” inalenga kuhamasisha jamii, asasi za raia, sekta binafsi, taasisi za Serikali, vyama vya siasa, wabia wa maendeleo, mtu mmoja mmoja na wadau wengine nchini kuongeza wigo wa fursa za uchumi kwa wanawake kuwawezesha kushiriki na kunufaika na hatua za maendeleo,” alisema.

SAMIA

Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, amelaani na kukemea vitendo vya ukeketaji wa wanawake na ubakaji vinavyoendelea katika jamii.

Aliwataka wananchi kote nchini kushirikiana kukabiliana na vitendo hivyo.

Alitoa wito kwa wananchi na wadau wote bila kujadili dini, kabila wala rangi kupambana ipasavyo na vitendo hivyo ambavyo vinarudisha nyuma jitihada za kumkwamua mwanamke katika uchumi.

Kuhusu maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, Samia alisema jukumu kubwa la Serikali ya awamu ya tano ni kuhakikisha wanawake wanaboreshewa ipasavyo mazingira ya kufanyia kazi, hasa shughuli za ujasiriamali waweze kufikia malengo waliyojiwekea.

“Inapofika katika shida zetu wanawake ni lazima tuwe kitu kimoja na sauti moja katika kulinda na kutetea haki zetu bila kujali itikadi za siasa,” alisema.

CHADEMA

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimetoa wito kuwahamasisha na kuwataka wanawake wote duniani kutambua nguvu waliyonayo na umuhimu wao kama chachu ya mabadiliko ya siasa, uchumi na jamii.

“Tunatambua nguvu ya wanawake katika harakati za mabadiliko. Tunatoa wito kwa jamii nzima kuendelea kuwahamasisha wanawake na wasichana wa Tanzania tupambane pamoja kuleta mabadiliko,” alisema Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliao wa chama hicho, Tumaini Makene.

   Meya wa Manispaa ya Ubungo, Boniface Jacob, alisema endapo wanawake wataelimishwa, watakuwa ni chachu ya kupunguza matumizi ya dawa za kulevya.

Alisema katika maadhimisho hayo wametembelea hospitali ya Wilaya ya Ubungo ya Palestina iliyopo Sinza, Kituo cha Afya  Kimara na Mbezi ambako waligawa zawadi kwa wanawake waliokuwa wamelazwa.

“Tumegawa kanga, sabuni za unga na vipande, maji, soda na pampas, lengo likiwa ni kuwasaidia wanawake ambao ndio chachu ya maendeleo katika jamii kwa ujumla,” alisema Jacob.

Alisema kwa vile Manispaa ya Ubungo ina maeneo mengi, wamejipanga kuhakikisha inajengwa hospitali kubwa itakayokuwa ya wilaya na itakuwa na uwezo wa kutoa huduma mbalimbali kwa wananchi.

ACT-WAZALENDO

  Kiongozi Mkuu wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, alisema akiwa amelelewa na mwanamke mwenye ulemavu na mpiganaji wa kweli wa haki za wananchi walio pembezoni, hana budi kutoa heshima zaidi ya kuongoza chama chenye misingi thabiti ya kumkomboa mwanamke.

“Kwa wanawake, ninyi ndio mhimili wa taifa hili, wazalishaji wakuu na walezi wa taifa letu. Kuirejesha nchi kwenye misingi ni wajibu wa kutambua nafasi yenu stahili katika jamii.

“Nikiwa nimelelewa na mwanamke mwenye ulemavu na mpiganaji wa kweli wa haki za wananchi walio pembezoni, sina namna kutoa heshima yangu zaidi ya kuongoza chama chenye misingi thabiti ya kumkomboa mwanamke.

“Msitarajie watu wengine kuwapigania, mnapaswa kuchukua hatua kupitia jukwaa la ACT-Wazalendo,” alisema Zitto.

TAMWA

Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA), Edda Sanga, alisema azma ya Serikali kuipeleka Tanzania katika uchumi wa kati wa viwanda itafikiwa endapo haki ya elimu kwa mtoto wa kike itapewa kipaumbele na kuhakikisha sera na sheria kandamizi zinarekebishwa.

“Tunaamini kuwa azma ya nchi ya kuipeleka Tanzania katika uchumi wa kati na viwanda  itafikiwa endapo haki ya elimu kwa mtoto wa kike itapewa kipaumbele na kuhakikisha sera na sheria kandamizi kwa wanawake na watoto wa kike zitarekebishwa na kuwezesha ushirikishwaji wa wanawake katika ngazi mbalimbali za uongozi na uamuzi,” alisema Sanga.

DC TEMEKE

Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Felix Lyaniva, aliwataka wanaume wanaonyanyaswa na kupigwa na wake zao kujitokeza hadharani kuwashtaki katika madawati ya jinsia.

“Wapo baadhi ya wanaume nao wananyanyaswa na wake zao… nawaomba msione aibu jitokezeni nanyi mshtaki katika dawati la jinsia,” alisema Lyaniva.

Lyaniva alikuwa mgeni rasmi katika maadhimisho hayo akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,063FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles