UMUHIMU WA KINGA KWA WAJAUZITO, FAO LA UZAZI

0
742

Na Christian Gaya


KINGA ya uzazi kwa kinamama lazima ichangie afya na ustawi wa mama pamoja na watoto wao ili kutimiza malengo namba 4 na 5 ya maendeleo ya millennia ya Tanzania kama mwanachama wa Umoja wa Mataifa.

Kutokana na kanuni na haki za uzazi na utaratibu wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) lengo kubwa la kuwa na fao la uzazi ni kuhakikisha kazi za wanawake haziingiliwi na hali hatarishi ya afya ya wanamke pamoja na mtoto wake na kwamba shughuli za kujifungua hazikwamishi shughuli zao za kiuchumi za kila siku, pamoja na usalama wa kazi zao iwe ya kujiajiri au kuajiriwa.

Utafiti unaonesha kuwa idadi kubwa ya kinamama wanaokufa kwa sababu ya kukosa huduma wakati wa kujifungua inaongezeka kila siku hasa kwa nchi zinazoendelea.

Pia kati ya wajawazito kumi wanaojifungua, wanne hupoteza maisha pamoja na watoto wao. Matukio haya yote hutokea katika nchi za Kiafrika ikiwamo Tanzania

Takwimu za hivi karibuni hapa nchini zinaonesha kwa mwaka, Tanzania inapoteza akina mama 7,900 kutokana na sababu zitokanazo na ujauzito. Idadi hiyo ni sawa na vifo 22 kwa siku. Magonjwa yanayoongoza kusababisha vifo vya wazazi nchini na mataifa mengine ni kifafa cha mimba, uzazi pingamizi, kupoteza damu nyingi wakati na baada ya kujifungua na maambukizi baada ya kujifungua.

Elementi kuu za kinga za uzazi ni kama kupata likizo ya uzazi, kupata mafao taslimu ya kuhakikisha mama anaweza kujikimu yeye pamoja na mtoto wake wakati akiwa likizo ya uzazi, kuhakikisha anapatiwa matibabu, mjamzito anapatiwa kinga ya afya ya ujauzito bila kumsahau mtoto wake kupatiwa kinga kutokana na hali hatarishi zinazoweza kusababishwa na sehemu za kazi zenyewe.

Ndiyo maana Mfuko wa hifadhi ya jamii Zanzibar (ZSSF) unatoa fao hili la uzazi ambalo ni matokeo ya juhudi za Serikali  kupambana na kupunguza vifo vya wajawazito na watoto.

Mfuko wa ZSSF unakwenda sambamba na malengo ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ambapo katika mwaka 2012 serikari ilitangaza rasmi kufuta malipo kwa wajawazito wakati wanapojifungua katika hospitali zote Unguja na Pemba.

“Uamuzi huu wa kutoa fao la uzazi unakwenda sambamba na jitihada zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali za kuimarisha ustawi wa wajawazito pamoja na kupunguza vifo vya watoto ambavyo baadhi husababishwa na umasikini ambao ndio chanzo cha watoto waliopo tumboni kukosa mahitaji ya msingi kwa afya zao au huduma muhimu wakati wanapozaliwa na mara baada ya kuzaliwa,” anasema Mkurugenzi mkuu wa ZSSF Abdul-Wakil Hafidh.

Mkurugenzi huyo anasema mafao ya uzazi yanalipwa kwa wanachama wanawake waliotimiza vigezo vya kuchangia kwa muda wa miezi 36, miezi sita iwe mfululizo kutoka tarehe anayoomba mafao, uthibitisho wa madaktari wenye kutambulika, vielelezo vya ushahidi wa kuthibitisha madai ya mafao, awe mjamzito ambaye ujauzito wake umefikia miezi 28 na awe amejifungua mtoto aliye hai. 

Kigezo cha malipo hayo ya fao la uzazi ni asilimia 30 ya wastani wa mshahara wa mwezi wa wanachama wote wa mfuko.

Hafidh anataja faida za fao hilo kuwa ni kuziba pengo la akina mama wanaojifungua, kusaidia huduma za matibabu za akina mama na watoto, kusaidia gharama za matunzo na mahitaji ya mtoto, hulipwa fedha taslimu, pia ni ya kipekee nchini ambapo malipo huongezeka iwapo mwanachama amejifungua mapacha.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here