Na Nora Damian, Mtanzania Digital
Tanzania na Umoja wa Ulaya zimekubaliana kuongeza upatikanaji wa masoko ya umoja huo kwa bidhaa za Tanzania na kuvutia uwekezaji zaidi katika sekta za kimkakati kama vile nishati jadidifu, viwanda na maendeleo ya miundombinu.
Makubaliano hayo yamefikiwa baada ya majadiliano ya pamoja ambayo yamefanyika kwa mujibu wa Mkataba wa Samoa uliosainiwa mwaka 2023 unaoelekeza umuhimu wa kuwa na majadiliano ya mara kwa mara kati ya Umoja wa Ulaya na nchi za Afrika, Karibian na Pasific.
Akizungumza Desemba 10,2024 Mwenyekiti Mwenza wa majadiliano hayo ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Cosato Chumi, amesema wamejadili kwa kina masuala muhimu yanayogusa pande zote mbili ikiwemo utawala bora, demokrasia, usalama wa baharini, biashara na uwekezaji, ulinzi na usalama kikanda na kimataifa.
“Majadiliano haya yamethibitisha nguvu na ukubwa wa ushirikiano kati ya Tanzania na Umoja wa Ulaya, yametuonyesha dhamira ya pamoja ya kuendeleza maendeleo endelevu kushughulikia changamoto za kikanda na kimataifa na kukuza amani na usalama.
“Tuna matumaini ya kuendelea kutekeleza ahadi zilizotolewa katika majadiliano haya na kuimarisha zaidi ushirikiano kati ya Tanzania na Umoja na kwa manufaa ya wananchi wetu sote,” amesema Chumi.
Amesema kwa sasa Umoja wa Ulaya umewekeza miradi ya utalii na miundombinu yenye thamani ya Sh trilioni 8.5.
Akizungumzia usalama baharini amesema wamejadiliana kuimarisha ushirikiano wa kukabiliana na changamoto za usalama wa baharini kama vile uvuvi haramu, usafirishaji haramu wa bidhaa na uharamia.
Kuhusu amani na usalama kikanda amesema kupitia majadiliano hayo wameangazia umuhimu wa Tanzania kama Mwenyekiti wa Asasi ya Siasa ya Ulinzi na Usalama wa SADC mchango wake katika Umoja wa Afrika na Jumuiya ya Afrika Mashariki.
“Tumekubaliana kuendelea kuimarisha juhudi za kukabiliana na changamoto za ulinzi na usalama katika ngazi ya kikanda na kimataifa ambapo umoja huo umeahidi kuendelea kuchangia juhudi za kupatikana amani katika ukanda wa Afrika na kwa ujumla,” amesema.
Amesema pande zote mbili zimekubaliana kuongeza ushirikiano ili kuhakikisha matokeo chanya na yenye manufaa kwa wananchi.
Kuhusu ushirikiano wa maendeleo amesema wameushukuru Umoja wa Ulaya kwa msaada wake endelevu kupitia mpango wa maendeleo wa majirani na ushirikiano wa kimataifa ambao umewekeza Euro milioni 726.
Amesema fedha hizo zimewezesha utekelezaji wa miradi muhimu katika sekta za nishati, uchumi wa buluu, mabadiliko ya tabianchi na mpango wa miji kuwa kijani.
“Tanzania imeomba uwekezaji wa baadaye uende sambamba na Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050 na utekelezaji wa haraka wa miradi chini ya mpango wa Umoja wa Ulaya unaojulikana kama Global Network,” amesema.
Kuhusu utawala bora na demokrasia amesema Tanzania imesisitiza kuendeleza misingi ya utawala bora na demokrasia chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan na kueleza mabadiliko muhimu ambayo yamefanyika kupitia falasafa ya 4R.
Amesema Umoja wa Ulaya umekubali kuimarisha ushirikiano wake kwa kuheshimu viongozi wa mkataba wa Viena juu ya mahusiano ya kidiplomasia.