30.2 C
Dar es Salaam
Sunday, September 25, 2022

UMMY MWALIMU: TUSITUMIE FEDHA ZA UKIMWI KULIPANA POSHO


Na MWANDISHI WETU    |

MALENGO ya Serikali ni kuhakikisha siku moja Tanzania inatangaza kuwa hakuna tena maambukizi ya VVU/ Ukimwi. Hili ni jambo linalowezekana iwapo kutakuwapo ushirikiano thabiti kati ya serikali na wadau wa sekta ya afya nchini.

Uwezekano huo, unathibitishwa hata na takwimu zilizotolewa na Tume ya Kudhibiti Ukimwi nchini (Tacaids), ambayo ilibainisha kuwa maambukizi ya VVU yameshuka kutoka asilimia 5.1 mwaka 2011/12 hadi kufikia asilimia 4.7 mwaka 2016/17.

Ili kufanikisha fedha za kutunisha Mfuko wa Ukimwi zinapatikana na kuendelea jitihada zilizofikiwa, Serikali na Tacaids kwa kushirikiana na Mgodi wa Geita Gold Mine (GGM) tangu mwaka 2002 wameitumia kampeni ya kupanda Mlima Kilimanjaro inayoitwa ‘Kili Challenge’ ili kuendesha harambee ya upatikana wa fedha za kutokomeza na kuelimisha jamii kuhusu VVU nchini.

Lakini pia Serikali nayo haijabaki nyuma katika kutunisha mfuko wa Ukimwi ambao ulianzishwa mwaka 2015, kwani katika mwaka huu wa fedha wa 2018/19, imetenga kiasi cha Sh bilioni tatu.

Akifafanua malengo ya serikali katika jitihada za kutokomeza Ukimwi nchini, Waziri wa Afya, Jinsi, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, anasema muda umefika sasa kwa wadau mbalimbali kushirikiana na serikali.

Ummy ambaye hivi karibuni amezindua harambee ya kuchangisha fedha hizo kwa mwaka 2018 kwa ajili ya afua za Ukimwi nchini, anasema ili kufikia malengo hayo pia mbinu mbadala na ubunifu wa hali ya juu unahitajika.

“Inabidi kuweka mikakati dhabiti itayohakikisha fedha zinazotengwa kwa ajili ya mapambano dhidi ya Ukimwi zinatumika kwa kusudi halisi ili kuondoa utegemezi wa misaada kutoka kwa wafadhili.

“Fedha zinazopatikana kwenye harambee hizi zinatakiwa zielekezwe moja kwa moja kwa wahusika na si kutumika kama posho za vikao kwa sababu pia zinatakiwa kusaidia serikali katika kuzipa nguvu sekta ndogo ili kuendelea kuthibiti maambukizi ya UKIMWI nchini,” anasema.

Anasema harambee hiyo inayoenda sambamba na kampeni ya kupanda Mlima Kilimjaro iitwayo ‘Kili Challenge’, itasaidia kutekeleza malengo ya serikali kuacha kuendelea kuwa tegemezi.

“Nawaomba wadau tuwe na moyo wa kujitolea ili kutunisha mfuko wa Kili Challenge kwa manufaa ya wananchi. Wahenga walisema; ‘kutoa ni moyo na si utajiri.’ Serikali, tayari tumetenga fedha Sh bilioni tatu, tunaomba mtuunge mkono,” anasema.

Hoja hiyo ya Ummy Mwalimu, inaungwa mkono na Mkurugenzi wa mgodi wa dhahabu Geita (GGM), Richard Jordison ambaye anasema kwa upande wa kampuni hiyo kwa ushirikiano na TACAIDS wamekusudia kuboresha upatikana wa huduma za uhakika kwa wagonjwa wa Ukimwi nchini.

Anasema kama ilivyo kwa malengo ya serikali kuifanya Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa viwanda, GGM nayo imedhamiria kutokomeza tatizo la Ukimwi nchini.

Aidha, Mkurugenzi wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania Bara (TACAIDS), Dk. Leornald Maboko, anasema kutokana na maambukizi ya VVU na Ukimwi, ni vema kuwapo kwa ushiriki wa wadau mbalimbali nchini kutokomeza maambukizi hayo.

“Kwa hiyo, kuendelea kuboresha mfuko huu wa Kili Challemge, si tu kumeongeza huduma kwa walengwa bali imesaidia utekelezaji wa dhima ya “Kili Challenge” ya kushirikisha wadau kuchangia kwa hali na mali katika udhibiti wa Ukimwi,” anasema.

Dk. Maboko anasema pamoja na jitihada kubwa zinazofanywa na serikali kwa kushirikiana na wadau, bado Ukimwi ni tatizo linaloathiri jamii kiuchumi.

“Bado kuna maambukizi mapya yanayokadiriwa kufikia watu 81,000 kila mwaka ambayo ni sawa na kiwango cha maambukizi ya asilimia 4.7. Pia takribani watu milioni 1.4 wanaishi na VVU nchini huku wanawake wa rika zote wakiwa waathirika wakubwa,” anasema.

Akifafanua kwa kina kuhusu mfuko huo, Dk. Maboko anasema Kili Challenge ni mfuko unaochangia juhudi za serikali katika mapambano dhidi ya Ukimwi na kutoa elimu kwa jamii kuhusu maambukizi ya VVU.

“Kili Challenge ni mfuko muhimu unaoshirikiana na taasisi za nje na ndani ya nchi katika kuendeleza mapambano dhidi ya VVU/Ukimwi kwa jamii ya Kitanzania na dunia kwa ujumla ili kuwapa matumaini ya kuhakikisha jamii inabaki bila kuathiriwa na VVU/Ukimwi katika miaka ijayo.

“Mfuko huo pia unalenga kuisaidia Serikali kukabiliana na VVU//Ukimwi sambamba na kutoa nafasi kwa watalii wa ndani na nje kuupanda mlima Kilimanjaro,” anasema.

Anasema kwa miaka 17 sasa, Tacaids kwa kushikiriana na GGM wamehamasisha Watanzania na watalii kutoka ndani na nje ya nchi kupanda mlima Kilimanjaro na kufanikisha kutunisha mfuko huo wa mapambano dhidi ya VVU/Ukimwi nchini.

“Ili kushiriki GGM Kili Challenge, unaweza kuchangia mfuko huu kwa kujifadhili au kumfadhili mwingine kupanda au kuzunguka mlima Kilimanjaro,” anasema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
201,896FollowersFollow
553,000SubscribersSubscribe

Latest Articles