23.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Ummy ataka wanafunzi wanywe maziwa shuleni

RAMADHAN HASSAN -DODOMA

WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amepiga marufuku utoaji wa vidonge vya Asidi ya Foliki kwa wanafunzi au wasichana balehe isipokuwa viendelee kutolewa kwa wajawazito na wanawake walio katika umri wa kuzaa.

Pamoja na hilo Ummy amesema atamwandikia barua Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako kutoa pendekezo kuanzia Septemba mosi mwaka huu, kila shule ya msingi na sekondari iwe na kibanda cha maziwa kwa ajili ya wanafunzi kupata lishe.

Kauli hiyo aliitoa jana Jijini hapa wakati akizindua wa Siku ya Lishe na Maadhimisho ya Lishe Kitaifa ambapo alisema fedha zilizokuwa zikitumika kwa ajili ya vidonge hivyo kwa wanafunzi na wasichana balehe, zitumike kuanzisha bustani shuleni ili kuzalisha vyakula vinavyotoa madini hayo.

Waziri Ummy alisema fedha ambazo zinatolewa na wadau wa maendeleo kwa ajili ya kununua vidonge vya asidi ya foliki zitumike kuanzisha bustani shuleni kwa ajili ya kuzalisha maboga, karoti na matunda mengine ambayo yanazalisha asidi hiyo.

Alisema fedha hizo pia zinaweza kupelekwa kwa vijana ili waanzishe miradi ya bustani za mboga kwa ajili ya kuzalisha mazao yanayozalisha asidi hiyo yakiwemo badala ya kutoa vidonge kwa wanafunzi.

Waziri Ummy alisema kwa kuanzisha bustani vijana watapata ajira na wataongeza kipato lakini pia watakuwa wamezalisha vyakula vyenye asidi ya foliki ili kusaidia wanafunzi badala ya vidonge hivyo.

Kuhusu unywaji wa maziwa shuleni, Waziri Ummy alisema atamwandikia barua Waziri wa Elimu Profesa Ndalichako ili kutoa pendekezo kuanzia Septemba mosi mwaka huu kila shule iwe na kibanda cha maziwa.

Alisema hajapiga marufuku uuzaji wa vyakula vingine shuleni, lakini ataomba katika kila shule hasa za bweni lazima ziwe zina na kibanda kimoja cha maziwa kwa kutumia fedha wanazopewa na wazazi kununua bidhaa hiyo ili wanafunzi waweze kupata lishe bora.

Ummy alisema kuanzisha vibanda vya maziwa shuleni hasa shule za kutwa, kutasaidia wanafunzi kuboresha afya yao, lakini pia  kutasaidia kupanua soko la bidhaa ya maziwa na kuongeza kipato.

Alisema utafiti wa Shirika la Afya Duniani (WHO) unaonesha kwamba kila mtu anatakiwa kunywa nusu lita ya maziwa sawa na lita 180 kwa mwaka, lakini kwa sasa kila mtu anakunywa lita 40 kwa mwaka sawa na vijiko 10 vya chai kwa siku.

Aliitaka Taasisi ya Chakula na Lishe kuharakisha mwongozo sahihi wa uandaaji vyakula vya nyongeza kwa watoto vyenye virutubisho, ambao unaandaliwa na taasisi hiyo kwa ushirikiano na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kupitia ufadhili wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP).

Kuhusu udumavu wa watoto wa chini ya miaka mitano japokuwa umepungua kutoka asilimia 34.4 mwaka 2014 hadi asilimia 31.8 mwaka juzi, Waziri Ummy alisema bado kasi hiyo haitoshi inatakiwa kupungua zaidi.

Pia aliomba kuongeza kasi katika kupunguza changamoto ya wanawake kuongezeka uzito na viribatumbo kwa walio katika umri wa kuanza kuzaa kutoka asilimia 29.7 mwaka 2014 hadi asilimia 31.7 mwaka 2018.

Naibu Katibu Mkuu Tamisemi (Afya) kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Tamisemi, Dk. Doroth Gwajima alisema fedha ambazo zinatengwa Sh 1,000 kwa kila halmashauri kwa ajili ya kuimarisha lishe ya watoto zimekuwa zikiongezeka.

Dk. Gwajima ambaye ni Naibu Katibu Mkuu (Afya) Tamisemi alisema, fedha hizo zilianza kutengwa 2017/18 ambapo zilipatikana Sh bilioni tisa na zikatumika asilimia 30 tu, 2018/19 zilitengwa Sh bilioni 15 zikatumika asilimia 45.

Alisema Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Tamisemi, Selemani Jafo amekuwa akifuatilia tangu alipopewa  jukumu hilo na Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan baada ya kusainiana mikataba ya lishe na wakuu wa mikoa ambao walishusha kwa wakuu wa wilaya hadi katika ngazi ya vijiji na dhamana kufuatilia akapewa waziri huyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles