29.7 C
Dar es Salaam
Wednesday, August 17, 2022

Ummy ataka kamati za ulinzi wa wanawake kila halmashauri

Mwandishi Wetu -Dodoma

SERIKALI imewaagiza maofisa maendeleo ya jamii wa mikoa na halmashauri zote kuhakikisha wanasimamia uanzishwaji na uendeshwaji wa kamati za ulinzi wa wanawake na watoto za ngazi za mikoa, wilaya, kata na vijiji.

Agizo hilo lilitolewa jana mkoani Dodoma na Waziri wa Afya na Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, wakati akizindua siku 16 za kampeni ya kupinga ukatili wa kijinsia Uwanja wa Jamhuri jijini hapa.

Kampeni hiyo iliratibiwa na Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo Afrika (WiLDAF) kwa kushirikiana na Mtandao wa Kupambana na Ukatili wa Kijinsia (Mkuki).

Ummy alisema kuanzishwa kwa kamati hizo ni maelekezo ya mwongozo wa mpango wa taifa wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto.

Aliagiza pia maofisa maendeleo ya jamii na ustawi wa jamii wa halmashauri zote kuanzisha programu za kijamii za kutokomeza ukatili wa kijinsia na kutoa msaada kwa waathiriwa wa vitendo vya ukatili katika halmashauri husika.

Aidha, ameagiza kuanzishwa kwa madawati ya jinsia katika taasisi za elimu ya juu ili kukomesha vitendo vya rushwa ya ngono na ukatili mwingine kwa wanafunzi.

Alisema Serikali itaendelea kushirikiana na asasi za kiraia katika mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia maeneo yote hapa nchini.

Alisema kuwa Serikali ya awamu ya tano imedhamiria kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia ili kuwawezesha wanawake na watoto kupata haki na kulindwa dhidi ya ukatili wa kijinsia, dhuluma, ubaguzi na unyanyasaji.

Ummy alisema kampeni ya kupiga vita ukatili wa kijinsia inahusu wanaume na wanawake, hivyo hakuna sababu ya wanaume kuona haya kwenda kutoa taarifa wanapofanyiwa vitendo vya aina hiyo.

Aliwataka wanaume wanaofanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia na wake zao kuacha kuona aibu kuomba msaada na badala yake watoe taarifa kwenye madawati ya jinsia ili waweze kusaidiwa kupata haki zao.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. John Jingu alisema ukatili wa kijinsia haukubaliki sehemu yoyote ile, hivyo kuitaka jamii kuacha manyanyaso dhidi wanawake na watoto.

Naye, Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia wanawake, Hodan Addou alisema kuwa shirika hilo litaendelea kushirikiana na Serikali kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa makundi yote ili kujenga jamii yenye usawa.

Aliongeza kuwa vitendo vya ukatili wa kijinsia ni tatizo la kidunia linalohitaji jitihada za pamoja katika kulikomesha.

Mkurugenzi wa WiLDAF, Anna Kulaya alisema ukatili wa kijinsia ni moja kati ya ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu na umeendelea kuwa kikwazo kikubwa katika kufikia malengo 17 endelevu, hususan usawa wa kijinsia.

Anna alisema ni dhahiri kwamba nchi haiwezi kufikia uchumi wa viwanda kama ukatili utaendelea katika jamii na kwamba ukatili wa kingono, hasa ubakaji umeendelea kuongezeka mwaka hadi mwaka.

Alisema kampeni ya mwaka huu inahamasisha ushiriki mkubwa wa wanaume na wavulana kuzuia vitendo vya kikatili.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,905FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles