24.1 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Ummy apokea Sh bil 1 kukabili corona

 MWANDISHI WETU

WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amepokea hundi ya Sh bilioni 1.1 kutoka Kampuni ya Uchimbaji Madini Geita (GGML) ili kukabiliana na mapambano dhidi ya maambukizi ya corona.

Akipokea hundi hiyo, Ummy alitoa wito kwa viwanda vya ndani kuchangamkia fursa za uzalishaji wa vifaa tiba na kinga dhidi ya ugonjwa wa Covid-19 kutokana na fedha zinazochangwa na kampuni mbalimbali nchini. 

Ummy alisema hayo jana Dar es Salaam wakati akipokea hundi hiyo kutoka GGML ambayo mbali na kutoa fedha hizo pia imeandaa mikakati kadhaa kudhibiti corona nchini.

Alisema Serikali inaendelea kuthamini msaada mkubwa unaotolewa na wadau hao katika kuonyesha jitihada za kuwalinda watumishi wa afya walio mstari wa mbele kudhibiti maambukizi.

“Niwaombe wadau wanaotoa misaada kutoka nje ya nchi kuzingatia mwongozo wa upokeaji wa dawa na vifaa tiba kwa kuhakiki ubora. Tutaendelea kuelekeza TMDA, kuhakikisha wanaongeza umakini uhakiki na usalama, kumekuwa na wimbi la uingizaji wa vifaa tiba, lazima kuhakikisha ni salama na vina vigezo vinavyohitajika.

“Pia natoa wito kwa viwanda vya ndani kwamba tunahitaji sana barakoa, PPE, sanitizer, hela hii ielekezwe kununua vifaa vinavyozalishwa ndani ya nchi, mfano barakoa za ndani ya nchi, kuna kiwanda Pugu, uwezo bado mdogo,” alisema Ummy.

Akizungumza katika hafla ya kukabidhi hundi hiyo, Makamu Rais, Maendeleo Endelevu GGML, Simon Shayo alisema kampuni yao pia imezindua mikakati kadhaa ya kupambana na janga hili ambalo lilibisha hodi hapa nchini Machi 16, mwaka huu na kuathiri zaidi ya watu 400 hadi kufikia sasa.

Alisema mikakati hiyo inalenga kushirikiana na Serikali pamoja na wataalamu wa afya kuelimisha jamii kuhusu virusi vya corona ikiwa ni pamoja na kugawa vifaa kwa jamii inayozunguka mgodi na wafanyakazi wa GGML kujikinga dhidi ya ugonjwa huo.

“Kwanza tumekabidhi hundi hii ya Sh bilioni 1.1, ni sehemu ya Sh bilioni 1.6 fedha ambazo GGML imetoa katika kutekeleza mikakati mbalimbali ya kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona nchini.

“Fedha hizi Sh bilioni 1.1 zitaelekezwa kwenye ngazi ya kitaifa kupitia mfuko maalumu wa mapambano dhidi ya Covid–19 ambao unasimamiwa na ofisi ya Waziri Mkuu.

“Hata hivyo, fedha nyingine kiasi cha Sh milioni 500 zinatumika kwa ajili ya kusaidia juhudi zinazofanywa katika ngazi ya mkoa na jamii, zitakazojumuisha ununuzi wa vifaa-tiba muhimu na vitendea kazi kama vile vifaa vya kujikinga, barakoa, mashine za kusaidia upumuaji,” alisema Shayo.

Pia alisema GGML ilikabidhi matanki 10 yenye ujazo wa lita 1,000 kila moja yaliyowekwa kwenye sehemu za wazi za mji wa Geita ili kuwawezesha wananchi kunawa mikono. 

“GGML pia imetoa kimiminika cha klorini ambacho kinatumika kutakasa mikono badala ya sabuni.

“Mradi huo pia unawezeshwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira ya Mjini Geita (Geuwasa) ambayo itatoa maji kila mara ili kuhakikisha kuwa huduma hiyo inapatikana kwa umma wakati wote. 

“Matanki hayo ambayo ni sehemu ya usambazaji wa msaada huo yamewekwa katika maeneo yafuatayo: Kituo cha mabasi (2), Kituo cha Mwatulole (1), Kituo cha Shilabela (1), Kituo cha Nyankumbuko (1), Soko la Nyankumbuko (1), Hospitali ya Geita (1), Soko la Dhahabu (2) na kituo cha Moyo Watoto Yatima cha Huruma (1),” alisema Shayo.

Aidha, aliongeza kuwa katika kujenga uelewa kuhusu janga hili kwa jamii zinazozunguka mgodi, GGML imekuwa ikigawa vipeperushi vyenye taarifa za virusi vya corona ndani na nje ya mgodi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles