30.2 C
Dar es Salaam
Thursday, November 30, 2023

Contact us: [email protected]

Umma walaani Jaji Warioba kupigwa

Jaji Joseph Warioba
Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba

NA WAANDISHI WETU

SIKU moja baada ya watu wanaodhaniwa kuwa ni wafuasi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuvamia mdahalo uliokuwa umeandaliwa na Taasisi ya Mwalimu Nyerere kuhusu Katiba inayopendekezwa na kusababisha kuahirishwa, wadu wengi wamejitokeza na kulaani tukio hilo.

Katika mdahalo huo, aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba alipigwa makofi mawili mgongoni na viongozi wenzake walinusurika kupigwa baada ya kuokolewa na walinzi katika Hoteli ya Blue Peal, Dar es Salaam juzi.

Katika tukio hilo polisi walilazimika kutumia risasi za moto kutawanya washiriki wa mdahalo huo.

Akizungumzia tukio hilo, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Ummy Mwalimu, alisema haungi mkono uhuni aliofanyiwa Jaji Warioba na wenzake.

“Ni lazima tuukemee kwa nguvu zetu zote uhuni huu, siungi mkono,” alisema.

DC Gambo

Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, Mrisho Gambo, alisema vurugu zilizotokea kwenye mdahalo huo ni upuuzi mtupu.

“Huu ni wakati mwafaka kwa watu wenye weledi kuwaelimisha Watanzania masuala ya msingi kuhusu Katiba yao kabla ya kura ya maoni ya wananchi wote.

“Ni upumbavu kutoka nyumbani kwako na kwenda kufanya vurugu, tunalea ujinga,” alisema.

CHADEMA

Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Profesa Abdalah Safari, alisema kitendo hicho ni kiashiria tosha kuwa huko mbele twendako hali si salama kama vijana wanaweza kuthubutu kukubali kutumika kwa kiwango hicho.

Alisema Tanzania ni ya Watanzania wote, kwa maana hiyo hayupo mtu mweye uwezo wa kudai kuwa na hatimiliki ya kuwazuia wengine kutoa uhuru wa mawazo yao.

Profesa Safari alisema watu wanapoongelea dhana nzima ya demokrasia nchini, ni pamoja na kukubali kusikiliza  mambo hata yale wasiyopenda kuyasikia.

“Huwezi kuwazuia watu kusema hususani katika masuala nyeti kama haya ya Katiba, vinginevyo hiyo siyo Katiba ya wananchi,” alisema Profesa Safari.

Aliseama kama kweli vijana hao walihisi kuudhiwa na yale yaliyokuwa yakijadiliwa kwenye mdahalo huo, ni bora nao wangeitisha mdahalo mwingine kwa lengo la kujibu kuliko kujidhalilisha mbele ya jamii.

MCHUNGAJI MWAMALANGA
Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kipentekoste, Mchungaji William Mwamalanga, alisema  kitendo kilichofanywa na vijana hao hakina tofauti na kuchukua fimbo na kulichapa kaburi la Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Nyerere.

Alisema hali iliyojitokeza juzi ni kiashiria cha aina ya vijana waliopo Tanzania ya leo ambao kwa siku za karibuni wamekuwa vinara wa kutaka kuongoza nchi.

Mchungaji Mwamalanga alisema wao kama kanisa wanasubiri kauli kutoka kwa Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete juu ya tukio hilo la kihuni lililomdhalilisha Jaji Warioba.

“Kanisa haliwezi kukubali kuwa na vijana wahuni wa kiwango hiki, tunalaani kwa nguvu zote tukio hilo lisilokuwa na chembe ya nidhamu,” alisema Mchungaji Mwamalanga.

Alisema kwa kipindi cha miaka mingi Watanzania wamekuwa na utamaduni wa kuwaheshimu wazee, lakini kitendo kilichofanywa na vijana kinaonyesha wazi kuporomoka kwa maadili.

KATIBU MKUU TEC
Baraza la Maaskofu wa Katoliki Tanzania (TEC) limelaani tukio hilo na kusema halipendezi wala halifurahishi.

Katibu Mkuu wa TEC, Raymond Sama, alisema wakati huu wa mchakato wa Katiba mpya ni vyema watu wakaheshimiana na kusikilizana.

“Kitendo kile hakipendezi na wala hakifurahishi, kipindi hiki tunapaswa kuwa na utulivu, kuheshimiana na kusikilizana,” alisema Sama.

DK. AZAVEL LWAITAMA

Aliyewahi kuwa mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Azavel Lwaitama, alisema uhai wa taifa lolote duniani ni nidhamu ya vijana na kama watakosa nidhamu basi taifa hilo halina tofauti na taifa mfu.

Alisema inapofikia katika nchi watu wanashindwa kubishana kwa hoja na badala yake wanataka kulazimisha hoja kwa kutumia mabavu, basi ni ishara ya kuchoka.

Dk. Lwaitama alisema demokrasia pana ni ile inayotoa mwanya wa mijadala mpana, hususani kwa masuala nyeti kama Katiba ni lazima yajadiliwe kwa uhuru.

Alisema vijana wa UVCCM wameonyesha udhaifu mkubwa kwa kukidhalilisha chama chao na viongozi wake kuanzia wa ngazi ya chini hadi taifa.

DK. HONEST NGOWI

Mhadhiri wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Dk. Honest Ngowi alisema waliohusika hata kama walikuwa wanapingana na hoja za Jaji Warioba walipaswa kumjibu kwa hoja.

“Ni aibu kwa wote waliohusika kwa sababu hata kama walikuwa wanapingana na hoja zake wangemjibu kwa hoja badala ya kumfanyia vitendo kama vile.

“Katiba inayopendekezwa inatambua suala la uhuru wa kujieleza, kwa kufanya kitendo kile kimetia doa taifa,” alisema Dk. Ngowi.

MOSENA NYAMBABE

Katibu Mkuu wa Chama cha NCCR-Mageuzi, Moses Nyambambe, alisema hata kipindi cha Mwalimu Nyerere watu walikuwa wakibishana, lakini si kwa kukoseana adabu kama ilivyoshuhudiwa juzi ikifanywa na vijana wa CCM.

Alisema hii ni ishara tosha kuwa CCM haipo tayari kwa mabadiliko na ndiyo maana wanapoona wamezidiwa huwa ni wepesi kutumia nguvu.

Nyambabe alisema CCM kama chama tawala, lazima kikubaliane na hali halisi ilivyo sasa vinginevyo watajikuta wakienda na maji.

“Kama taifa tuwe na utamaduni wa kuheshimiana, hata kama hoja zangu zinaonekana kutokukubalika na wewe kinachotakiwa ni wewe kunijibu kwa hoja si kwa kutumia nguvu,” alisema.

BUTIKU
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku, amesema kitendo kilichotokea ni cha aibu na cha kihuni na kinapaswa kupingwa, na Serikali inatakiwa kuingilia kati ili kisijirudie tena.

MAKONDA
Katibu wa Uhamasishaji wa UVCCM amekanusha tuhuma hizo za kumshambulia kwa kipigo Jaji Warioba.

Alisema kuhusishwa kwake na tukio hilo ni sawa na kutomtendea haki, kwa sababu alikuwa miongoni mwa watu waliokuwa wakimtetea Jaji Warioba.

Makonda alisema taarifa zilizosambazwa na baadhi ya watu za kumhusisha kuwakusanya vijana wanaosadikiwa kuwa wa CCM ili kufanya vurugu na kumpiga kiongozi huyo ni miongoni mwa mikakati ya kumshusha kisiasa.

POLISI
Katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi Mkoa wa Kinondoni, limejichanganya kuhusu kukamatwa  kwa  Makonda kutokana na vurugu hizo.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camilius Wambura, alikiri Makonda kupatiwa dhamana baada ya kufikishwa Kituo cha Polisi Magomeni.

“Sifahamu ni watu gani walikuja kumtolea dhamana, lakini alipatiwa dhamana baada ya kufungua kesi ya kupigwa katika tukio lilotokea juzi eneo la Ubungo,” alisema Wambura.

Habari hii imeandaliwa na Patricia Kimelemeta, Shabani Matutu, Michael Sarungi na Nora Damian.

- Advertisement -

Related Articles

7 COMMENTS

  1. kitendo kilichofanywa kumpiga mzee warioba ni cha kihuni. serekali inapaswa kuchukua hatua kali juu ya suala hilo haipaswi kukaa kimy kwa hilo. na tukilifumbia macho suala hili huko tuendako itafika mahali sisi wenyewe kuuwana wenyewe kama matukio yatatokea kisha tukae kimya.

  2. Waliompiga judge, hawakuelimika kwani walioelimika hawatumii mabavu. Halafu wachukiliwe hatua kwani kupiga mtu ni criminal offence, na tuache kusema kirahisi rahisi kuwa ni wahuni, kwani hao walijipanga kumpiga.

  3. Nimesikitishwa sana na tukio la juzi. Nililiangalia tangu mwanzo hadi mwisho. Kweli tumefikia pabaya. Mimi si mwanachama wa chama chochote hata chama tawala sipo. Mimi ni mchungaji niliyekwisha staafu. Ni mzee mimi lakini kilichotokea ndugu zangu kimeshusha hadhi ya nchi hii sana. Naomba niulize, CCM imepanga isimamie nchi hii kwa staili gani? Hivi kama kitendo hiki kingefanywa na vijana ambao sio wa CCM leo tungekuwa tunashuhudia nini? CCM wanataka kufikia malengo yao kwa kupitia njia gani? Nimeshangaa nilipomsikia mtu mniliyemheshimu sana mzee Samwel Sitta. Anasema yaliyomfika Warioba amejitakia. Yaani ni kwamba hairuhusiwi kuongea chochote kuhusu katiba. Kwa hiyo, wewe Warioba umetoka wapi kufanya kitu kisichoruhusiwa? Je, ni hapo CCM imefika? Mnataka kulazimisha watu waseme ndiyo hata kama hawataki? Ama kweli, “the end justifies the means”. Yuko mfalme mmoja ambae alimkasirisha sana Mungu mpaka Mungu akawauliza malaika, “Ni nani atakayekwenda kumdanganya Ahabu (mfalme) apange vita ili niende nikammalizie huko?” Je, CCM imefika mahali pa kupanga vita na wananchi wote wa Tanzania ili imalizikie huko? Tunahitaji busara sana katika suala hili. Serikali inaponyamaza inazidi kujiharibia. Maana inajulikana wazi mipango ilifanywa na akina nani.

  4. Ni laana nyingine kwa nchi yetu tunayoipenda sana TANZANIA, mtu mwenye heshima kubwa tuliyepaswa kuchota hekima, busara, ushauri na mawazo yanayoweza kututoa hapa tulipo na kutupeleka mbele hatimaye tunampiga na kumdhalilisha. Hii ni hatari lakini Mzee wetu Warioba ni mtu mwenye busara nyingi na ni mwenye imani dhabiti na iliyosimama ninamuomba awasamehe wale wote waliofanya kitendo kile cha kumpiga na kumdhalilisha pengine leo wanajiona majasili kwa kufanya kitendo kile ila naamini hawatakaa milele bila kugundua ujinga walioufanya. Mungu akupe maisha marefu mzee wetu Joseph Sinde Warioba ili sisi tunaojua thamani yako tuendelee kuchota hekima kutoka kwako mzee wetu. MUNGU IBARIKI TANZANIA.

  5. Ni maskitiko makubwa na mmomonyoko mkubwa wa maadili katikat taifa Letu. Tusisahau Tanzania ni yetu wote na katiba ni yetu wote Kuikataa kama ni mbovu ni kwa faida yetu wote na kikubali kama ni nzuri iwe kwa faida yetu wote. Katiba si ya watawala wala watawaliwa bali Maridhiano ya kweli kwa wote.

  6. Okay Warioba kapigwa, JE kwanini hao watu wasikatwe?? Kwani hakukua na mwenye video kamera akirecord mkutano ulipokua ukiendelea??? Kama alikuwepo then Ni rahisi sana wakienda through that video kwani wahusika wote wataonekana. From there then wanaeza Kua identified na wakafikishwa mahakamani. Pole sana Mzee wetu worry not Mungu atawanyoosha tu wote waliohusika na hizo vurugu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
579,000SubscribersSubscribe

Latest Articles