30.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

UMASIKINI UNAVYOWAINGIZA WANAFUNZI KWENYE NDOA BILA KUPENDA

JOHANES RESPICHIUS-DAR ES SALAAM


NDOA na mimba za utotoni ni tatizo kubwa kwa watoto wa kike nchini, ambalo limekuwa likikatiza ndoto zao za baadae.

Utafiti uliofanywa kuhusu vichocheo na madhara ya ndoa za utotoni wa mwaka 2016; unaonyesha zaidi ya asilimia 50 ya wasichana katika mikoa ya Shinyanga, Mara, Dodoma na Tabora wanaolewa kabla hawajafikisha umri wa miaka 18. Katika Mkoa wa Iringa, ni msichana mmoja kati ya 10 na Dar es Salaam ni msichana mmoja kati ya watano wanaolewa kabla ya muda.

Utafiti huo wa Taifa umefanywa na Serikali kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Kupunguza Umaskini (REPOA), Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Idadi ya Watu Duniani (UNFPA), Shirika la Plan International, Forward na Shirika la Jukwaa la Utu wa Mtoto (CDF).

Katika uzunduzi wa ripoti ya utafiti huo, Mtaalamu wa masuala ya uchumi kutoka Repoa, Dk. Lucas Katera anasema utafiti huo umewashirikisha watu 3,299 kutoka katika mikoa 10 yenye viwango vya juu, kati na chini vya ndoa za utotoni.

 

Vichocheo

Anasema utafiti umegundua kwamba kichocheo kikubwa cha ndoa na mimba za utotoni ni umaskini, jambo ambalo husababisha familia zenye maisha magumu kuozesha watoto wao wa kike wakiwa na umri mdogo.

“Kutokana na hali hiyo, watoto wa kike kujikuta wakikikatizwa masomo yao na kuozwa kama njia ya kujipatia mali kupitia mahari inayolipwa kwa familia ambapo mara nyingi huwa ni ng’ombe au fedha taslimu.

“Pia mila na desturi katika makabila mbalimbali kama vile sherehe za matambiko, ngoma za kimila na ukeketaji kwa watoto wadogo huwa ni ishara kwamba yuko tayari kuolewa,” anasema Dk. Katera.

Anasema hali ya kutokuwa na usawa wa kijinsia kati ya wasichana na wavulana hususan majumbani, inahamasisha ndoa za utotoni kwa sababu mabinti wanaonekana hawana thamani ya kiuchumi zaidi ya mahari na elimu haichukuliwi kama

kipaumbele kwao.

Anasema inakidiriwa kuwa watoto 36 kati ya 10 huolewa kabla ya kufikisha miaka 18 na wengine 27 kati ya 100 hupata mimba kabla ya kufikisha umri huo.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu ndiye aliyezindua utafiti huo.

Anakiri kuwa sheria ya ndoa ya mwaka 1971 ni changamoto katika mapambano dhidi ya ndoa na mimba za utotoni na kwamba ataendelea kuwashawishi viongozi wake kuangalia namna ya kuirekebisha.

“Katika suala la ndoa na mimba za utotoni nimeamua kujilipua, sheria ya ndoa ya mwaka 1971 ni kichocheo kikubwa ambacho kinamfanya mtoto wa kike kuolewa na kubebeshwa mimba mapema.

“Sichoki na sitachoka kuendelea kushawishi viongozi wenzangu  ili tuifanyie marekebisho, kama ingekuwa chini ya wizara yangu ningeshaishughulikia lakini ipo Wizara ya Katiba na Sheria, hivyo nitashirikiana nao tulifanyie kazi suala hilo,” anasema Ummy.

Anasema wakati sheria hiyo ikisubiriwa kufanyiwa marekebisho ni bora sheria ya elimu kama ilivyorekebishwa mwaka 2016 itekelezwe ili kuendelea kupinga ndoa za utotoni.

Hivyo, anaagiza walimu wakuu wa shule za msingi na sekondari kutekeleza sheria hiyo ya elimu kwa vitendo kwa kuwasilisha kwa Kamishna wa Elimu, taarifa ya robo mwaka ya wasichana waliopata ujauzito wakiwa shuleni.

“Pia maofisa ustawi wa jamii ambao wapo chini wizara yangu nao wapite kila nyumba kukusanya takwimu za watoto waliopata ujauzito na walioolewa chini ya umri wa miaka 18.

“Lazima waje na taarifa sahihi zinazoeleza changamoto wanazipitia watoto huko majumbani ili tuzifanyie kazi ipasavyo,” anasema.

Naye Mkuu wa Kitengo cha Ulinzi wa Mtoto kutoka Shirika la Plan International – Tanzania, Jane Mrema anasema ripoti hiyo imeonyesha jinsi gani nafasi ya watoto wa kike haipo.

 

“Chngamoto za elimu zimekuwa kichocheo kikubwa kwa watoto wa kike kuingia kwenye ndoa za utotoni hasa kutokana na shule nyingi kutokuwa na mazingira rafiki ya kumfanya aendelee kusoma.

“Pia kukosekana kwa sera rafiki zinazoweza kumwezesha msichana akipata ujauzito akiwa shuleni aweze kuendelea na masomo yake baada ya kujifungua,” anasema Jane.

Anasema kutokana na changamoto ya uhalisia wa takwimu za ndoa za utotoni, ndiyo maana Plan International kwa kushirikiana na Serikali pamoja na wadau mbalimbali wameamua kufanya utafiti huo,” anasema Jane.

Anasema shirika hilo litaendelea na harakati za kupigana na tatizo hilo ambapo katika mpango kazi wa miaka mitano kuanzia 2017- 2022 wanakusudia kuwawezesha zaidi ya wasichana milioni moja ulimwenguni kujitambua na kuhakikisha hakuna anayeachwa nyuma katika suala la maendeleo.

Anasema kuna haja ya kuchukua hatua stahiki kwa wahusika wanaochangia ongezeko la ndoa za utotoni hapa nchini ikiwa ni pamoja  na marekebisho ya sheria hizi za ndoa zinazokinzana.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles