25 C
Dar es Salaam
Sunday, October 6, 2024

Contact us: [email protected]

Umasikini, ukosefu wa ajira unapoibua tisho jipya la ugaidi

JOSEPH HIZA, DAR ES SALAAM

KATIKA kipindi cha miaka mitano iliyopita, kundi la Al-Shabaab limeendesha mashambulizi zaidi ya 20 nchini Kenya, ambayo yamesababisha vifo vya watu zaidi ya 400.

Kati ya mashambulizi hayo kubwa zaidi kutokana na idadi ya walioouawa ni lile lililotokea katika Chuo Kikuu cha Garissa, ambako watu zaidi ya 150 waliuawa, wengi wao wakiwa wanafunzi waliokuwa na ndoto nyingi.

Pamoja na ukubwa wa unyama kulinganisha na mashambulizi wengine tukio hilo linaonekana kufunikwa na mashambulizi yanayolikumba jiji la Nairobi.

Hiyo haishangazi kutokana na umaarufu wa jiji la hilo, hivyo kumulikwa zaidi ndani na nje ya nchi. Nairobi ni makao makuu ya serikali, makao makuu ya mashirika ya kimataifa, ni kioo cha utalii na kitovu cha biashara na uchumi wa taifa hilo.

Kwa msingi huo bila Nairobi ‘hakuna’ Kenya. Ni moyo au injini ya uchumi wa taifa hilo kama ilivyo Dar es Salaam kwa Tanzania. Kwa sababu hiyo, ni mji unaolengwa zaidi na wapiganaji wa al-Shabaab ili kulihujumu Taifa hilo kama kisasi cha uwapo wa majeshi ya Kenya nchini Somalia.

Umekumbwa na mashambulizi kadhaa kutoka kundi hilo, lakini makubwa yaliyoutikisa ni mawili; la kwanza lilitokea mwaka 2013 dhidi ya kituo cha biashara cha maduka ya kisasa cha Westgate, ambalo watu 67 walikufa katika operesheni ya siku nne.

Ikachukua miaka mitano hali kutulia, ikiashiria namna kwa vyombo vya ulinzi na usalama vilivyojidhatiti, hali iliyoweza kuzuia mashambulizi mengine kabla ya kutokea na washukiwa kukamatwa.

Baada ya hapo kukiwa na hali ya kujisahau, al-Shabaab walikuwa wameshapata mbinu mpya ya kufanikisha malengo yao kabla hawajashikwa na vyombo vya usalama, wakaanza kuifanyia kazi kwa miaka kadhaa kama si miezi.

Na ndivyo walivyofaulu kuendesha shambulio la pili Jumanne ya wiki iliyopita katika hoteli ya kifahari maarufu ya Dusit D2.

Shambulio hilo lililodumu kwa saa 19 liligharimu maisha ya watu 21 wengi wao wakiwa Wakenya na huku washukiwa wenyewe watano au sita wakiuawa.

Wakati kukiwa na mfanano fulani baina ya matukio hayo lakini pia kulikuwa na tofauti kadhaa ikiwamo suala la utaifa wa wapiganaji. Katika tukio la Westgate wapiganaji walitokea Somalia, lakini tukio la sasa sehemu kubwa walitokea Kenya na ndiyo maana imeonekana kuharakisha upelelezi kubainisha mengi kulinganisha na lile la kwanza.

Baada ya kushindwa kuendesha mashambulizi mengine kutumia wageni, al-Shabaab ikabadili mbinu ya kuwatumia Wakenya zaidi, ambao isingekuwa rahisi kubainika kulinganisha na wageni walio rahisi kushtukiwa.

Imeripotiwa wapiganaji hao walikuwa wakionekana mara kwa mara katika hoteli hiyo katika kile kinachoonekana kusoma mazingira kabla ya kuendesha shambulizi.

Na hawakushtukiwa kutokana na mwonekano wao wa ‘Kikenya’ na kirafiki bila kusahau zungumza yao ikiwamo Kiswahili halisi cha humo.

Sasa ni mbinu gani walizotumia kuwapata wapiganaji Wakenya? al-Shabaab kama yalivyo makundi mengine mengi ya kigaidi linafahamu urahisi wa kurubuni watu kujiunga nao pasipo kutumia nguvu nyingi ni umasikini, ukosefu wao wa ajira, uduni wa elimu, matatizo ya kijamii, au kutengwa na serikali ama ufahamu mdogo ikiwamo wa dini.

Walengwa ni vijana na hivyo baada ya kuahidiwa pesa kuondokana na umasikini kwao na familia zao pamoja na motisha nyinginezo ingawa wengine hujiunga kwa hiari wakichochewa na baadhi  sababu tajwa hapo juu au huruma kwa al-shabaab.
Baada ya hapo huwapeleka kwenye kambi zao za mafunzo hususani nchini Somalia. Mbali ya mafunzo mbalimbali ya kijeshi pia hujazwa itikadi kali tayari kwa kazi wanazoandaliwa kuzifanya.

Hilo linaonekana kuwa tisho jipya si kwa Kenya pekee bali pia majirani zake kama Tanzania, Uganda, ambako pia kuna makundi makubwa ya vijana waliokata tamaa kimaisha, elimu au matatizo ya kijamii.

Kama, ambavyo vijana walioathirika hasa kutoka vitongoji masikini wako tayari kugeuka punda kuwafanyia matajiri kazi hatari ya kusafirisha mihadarati, ndivyo ilivyo rahisi kuwalaghai kujiunga na makundi haya.

Kitongoji hiki cha Majengo ni moja ya vile vyenye vijana wengi wa aina hiyo. Ni asubuhi mapema wakazi wa kitongoji hicho kilichopo katika mji wa Nyeri, katikati ya Kenya, wanatoka kwa tahadhari kutoka nyumba zao kana kwamba kuna tatizo.

Wengi wao wanaonekana kimya na wako mbali kimawazo huku makundi ya wanafunzi wa waliovalia sare wakiharakisha kuelekea shule.

Siku moja kabla ya siku hiyo, jamii hiyo ya Majengo ilikuwa imebaini kuwa mmoja wa wakazi wao wenyewe alihusika na shambulio baya katika hoteli ya kifahari ya Dusit D2 katika mji mkuu wan chi hiyo,  Nairobi.

Picha za usalama za CCTV kutoka eneo la tukio zilimuonesha Salim Ali Gichunge maarufu kama Farouk kuwa mmoja wa washambuliaji wa tukio hilo na kuwashtua wengi.

Wakazi wa kitiongoji hicho cha makazi yaliyojengwa kiholela walibakia katika mshtuko siku hiyo, wakijiuliza maswali mengi yasiyo na majibu wapi Gichunge wanayemfahamu kama ‘mtoto wao mzuri’ tangu utotoni alikoitoa roho ngumu ya kikatili kushiriki mauaji ya ndugu zake Wakenya.

“Watoto wetu hawana ajira. Wanahitaji kula. Wengi wao wameacha shule na wazazi wao ni masikini mno kuweza kuwasaidia kuendelea na elimu,” kiongozi wa jamii hiyo ya Majengo, Ratib Hussein anasema.

“Wazazi hawana hili wala lile wakati wasaka wapiganaji wa al-Shabab wanapowajia watoto wao,” Hussein anaongeza huku akiwa amesimama umbali mfupi tu kutoka nyumba. ambayo Gichunge alizaliwa na kutumia miaka yake ya awali.

Kikiwa katii ya Wilaya ya Kibiashara  Nyeri na eneo la King’ong’o, kitongoji holela cha Majengo ni moja ya maeneo yenye mbanano mkubwa wa watu katika mji huo na nyumbani kwa watu masikini zaidi.

Wengi wa wakazi wa kitongoji hicho ni vibarua na eneo hilo linahifadhi wahalifu hatari, wavuta bangi, makahaba, wauza pombe haramu na wachuuzi wa mihadarati.

Inaaminika bidhaa zinazoibwa katika mji na maeneo kuuzunguka hufichwa katika kitongoji hicho huku wahalifu wenyewe pia wakijenga viota.

Ijapokuwa ni eneo lenye watu wengi, watu hufahamiana sana na hivyo wageni ni rahisi kuwajua na hata kuwafuatilia. Ndiyo maana eneo hilo ni hifadhi salama kwa wahalifu wanaosakwa.

Nyumba za humo zimetengenezwa kwa vitu vya ubora hafifu na kodi ni hadi Sh 10,000 za Tanzania kwa mwezi.

Hata hivyo, polisi walivamia nyumba ya Farouk iliyoko eneo la Guango, Ruaka, Jumatano ya wiki iliyopita ambako wanaamini shambulio lilipangwa.

Farouk unaweza sema ni mmoja wa wakazi wachache wenye unafuu pengine kutokana na al-Shabaab kwani alipanga katika nyumba aliyoishi na mkewe alilipia kodi ya Sh 800,000 za Tanzania kwa mwezi. Mkewe huyo, Violet Kemunto Omwoyo bado anasakwa na polisi.

Kwa sababu ya umasikini mkubwa katika eneo hilo, wamekuwa tegemeo kubwa la wanasiasa na wanaharakati wanaoitisha maandamano ya mitaani kwa kushawishiwa kwa fedha.

“Kwa Sh200 tu za Kenya sawa na Sh 4000 za Tanzania unampata mtu kirahisi kuingia katika maandamano ya kufa mtu kutimiza matakwa ya wanasiasa au wanaharakati.

Ndiyo maana wasaka wapiganaji wapya wa al-Shabaab eneo hilo kwao ni mgodi mzuri wa kujipatia wapiganaji wa kutimiza mipango yao wakitumia udhaifu wa umasikini wa wakazi na kutokuwa na ajira au elimu duni na ufahamu mdogo na wepesi wa kulaghaiwa.

Kwa maelezo ya baba yake, Ali Gichunge, sajenti wa zamani wa Jeshi la Ulinzi Kenya (KDF), ambaye alikamatwa kabla ya kuachiwa, alipoteza mawasiliano na mwanae huyo peke wa kiume miaka mitano iliyopita na hakufahamu kama alijiunga kwa siri na al Shabaab.

Anasema mwanae huyo alizaliwa na kukulia katika familia yenye maadili ya Kiislamu huko Isiolo na alikuwa na ndoto kubwa za kuwa mhandisi. Hakukosekana Madrassa kwao Isiolo alikokulia.

Wakati baba mtu akitokea Isiolo, mama yake Salma Gichunge anatokea kitongoji hicho cha Majengo,  Nyeri.

Gichunge anasema anadhani kutengana kwake na mkewe wa kwanza yaani mama yake Farouk mwaka 2010 ni chanzo cha mwanae kupoteza mwelekeo.

Farouk alipenda michezo ya kuigiza shuleni na wakati wa madrassa, hata hivyo hakupata alama za kutosha kumwezesha kujiunga na chuo kikuu, ambako angetimiza ndoto yake ya kuwa mhandisi.

Baba yake anasema kwamba aliendelea kuonana na mwanae hata kumsaidia kuifedha hadi mwaka 2015 wakati alipoteza mawasiliano naye.

Baada ya kushindwa kujiunga na chuo kikuu, Farouk alikaa na mama yake katika nyumba yao ya Isiolo ambako alifanya kazi chafu kama vile kuuza milungi.

Badaye akaondoka  Isiolo kwenda  Nyeri na mwaka 2015 alienda  Mombasa ambako alipanga kusomea na kufundisha dini ya Kiislamu katika msikiti wa Majengo huko Mombasa kwa mujibu wa majirani.

Baada ya Farouk kuondoka Nyeri, alikata mawasiliano na babake lakini aliendelea kuwasiliana na mama na dada zake wawili ambao bado wako shule na wanaishi Isiolo.

Baba mtu anasema alipomwuliza Salma alipo mwanae, naye alidai hana mawasiliano lakini alitilia shaka hilo, akiamini kwamba mzazi mwenzake huyo amelenga kumweka mbali na mwanae na hivyo akaamua kujikita kulea familia mpya ya mke wa pili.

“Nilikuja shtushwa kumuona pichani, atakuwa alichukuliwa Majengo kule Nyeri, kisha Mombasa ambako alighilibiwa akili kuwa na  misimamo mikali,” alisema.

Mkenya mwingine ni Mahir Khalid Riziki (25) aliyejitoa mhanga kwa kujilipua ndani ya mgahawa wa hoteli ya DusicD2. Riziki , aliacha shule akiwa kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari Bhadala mjini Mombasa mwaka 2011 kabla ya kuoa mwaka uliofuata 2012.

Mkewe Sahaila Bakari Mwinyi, alikuwa amekamatwa siku tano baada ya shambulio hilo huko Bakarani, Kisauni sambamba na baba wa Khalid aliyekamatiwa Majengo, Mvita. Hata hivyo baada ya kuhojiwa mjini Nairobi waliachiwa huru siku iliyofuata.

Kwa kutumia mifano ya Gichunge na Riziki wakiwa kama Wakenya ni kielelezo hicho ya vijana kutokea makazi duni, kutatizika kwa ndoto zao za kielimu kunakowaweka na hatari ya kunaswa na mitego ya al-Shabaab.

Yote hayo yanaonesha Wakenya na hata majirani wakae chonjo kwani wanakabiliwa na tisho jipya la ugaidi unaotengenezwa nyumbani.

Suluhu si matumizi ya nguvu tu bali busara ikiwamo utatuzi wa matatizo ya kielimu, kijamii na kiuchumi ili kupunguza kama si kuondoa kabisa uwezekano wa vijana kujiunga na makundi hayo, kwani utafiti unaonesha wale wenye maisha mazuri au waliosoma sana si rahisi kulaghaika..

Siku chache baada ya shambulio hilo kulitokea video iliyokuwa ikisambaa kwa kasi katika mitandao ya jamii ikieleza uwapo wa tishio la ugaidi Tanzania na kwamba wapiganaji wengi wa al-Sahaabn ni Watanzania, hata hivyo serikali imeikana video hiyo kuwa si tu ni ya zamani bali pia maudhui yake yamejikita katika hisia.

Katika kila jiji kubwa la Kenya kama ilivyo mataifa mengine jirani, kuna makazi holela, ambako watu wanahaha kuhakikishga mkono unaenda kinywani.

Vijana wengi wadogo katika miji hiyo hukaa vijiweni au huondoka nyumbani asubuhi na kurudi jioni au usiku mwingi huku shughuli wafanyazo zikiwa hazijulikani. Wengine hutoweka bila kutojulikana walipo. Ni hatari bila kuchukua hatua.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles