29.7 C
Dar es Salaam
Monday, October 2, 2023

Contact us: [email protected]

UMAARUFU HAUKUZUII KUWA BABA AU MAMA BORA

NA AZIZA MASOUD,

MALEZI ya mtoto kutoka pande zote mbili ni kitu muhimu kinachosaidia kumjengea mtoto kukua katika hali nzuri.

Katika familia za Kiafrika baadhi ya watu hudhani kuwa dhima ya malezi ni kwa mama pekee.

Kuna baadhi ya kina baba hawana muda kabisa katika malezi ya watoto wao hata mtoto anapomuuliza kitu chochote anamwambia amwambie mama.

Tabia ya kutojali na kutomfuatilia mtoto pia ipo hata kwenye makundi ya wazazi wanajulikana katika jamii ama kwa jina jingine watu maarufu ama wanaokuwa na nyadhifa za juu katika eneo fulani.

Watoto wenye wazazi maarufu au kuwa na wadhifa si kwamba hawalelewi vizuri isipokuwa wanapata muda mfupi wa kuwasiliana na wazazi wao kutokana na majukumu makubwa yanayowakabili.

Kutokana na hali hiyo, mara nyingi kundi hilo linakuwa na nafasi kubwa ya kuharibikiwa kimaadili na hata kujiingiza katika makundi ya vijana wanaofanya  vitendo viovu kama wizi.

Wapo watu maarufu wenye nyadhifa kubwa wanajitahidi kutenga muda wa kufanya mambo yao ya kikazi na wa kukaa na mtoto.

Unapotaja kundi la watu waliowahi  kuwa na madaraka makubwa lakini wanaonekana kujali familia zao huwezi kuacha kutaja majina ya viongozi kama Rais mstaafu wa Marekani, Barack Obama pamoja na Rais mstaafu wa Awamu ya Nne Jakaya Kikwete.

Viongozi hawa pamoja na umaarufu mkubwa waliokuwa nao baada ya kufikia ndoto zao za urais, walijitahidi kuionyesha dunia kuwa familia zao pia ni muhimu zaidi.

Rais Kikwete mara kadhaa alikuwa akionekana kuwa karibu na familia yake  hasa mke wake na hata kutamka hadharani kuwa akistaafu atatumia muda mwingi kupumzika na familia yake.

Katika hotuba zake, Kikwete pamoja na kuzungumzia mambo ya kitaifa pia alikuwa akiomba radhi kwa familia yake ikiongozwa na mkewe mama Salma, kwa kutumia muda mwingi kuwatumikia wananchi na kukosa nafasi ya kuhudumia familia.

Hali hiyo pia ilikuwa kwa Rais Obama akiwa na mkewe Michelle na watoto wake Maria na Sasha, walikuwa wakionekana katika maeneo mbalimbali wakiwa katika mitoko ya kifamilia.

Obama alipata umaarufu mkubwa kutokana na maisha anayoishi ya kujali familia yake kama anavyojali kazi zake.

Maisha ya viongozi hawa yanaonyesha jinsi gani nafasi ama umaarufu anaokuwa  nao mzazi hauwezi kumtenganisha na familia yake.

Ushauri wangu wazazi mliopo katika nafasi kubwa mnapaswa kujali familia zenu kwa kuwa umaarufu na madaraka vyote huisha lakini familia ndicho kitu pekee unachokuwa nacho katika maisha yako yote.

Tuache tabia za kujifanya tuko busy na vitu vya kupita na kuwapa watu nafasi ya kutuharibia watoto wetu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,770FollowersFollow
575,000SubscribersSubscribe

Latest Articles