Na Hadija Omary, LindiÂ
Serikali imewaagiza viongozi katika ngazi ya Halmashauri zilizopo pembezoni mwa ukanda wa Bahari ya Hindi kuwahamasisha wananchi kuchangamkia fursa ya ufugaji wa mazazo ya bahari katika maeneo yao.
Agizo hilo limetolewa na Naibu Waziri wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Abdalla Ulega alipokuwa akizungumza na viongozi wa halmashauri za Mikoa ya Lindi na Mtwara katika kikao kazi kilichofanyika mkoani Lindi.
Kikao hicho kilikuwa na lengo la kutambulisha, kuhamasisha, kuweka mikakati ya pamoja ya namna ya kutumia rasilimali za mazao ya bahari kibiashara.
Ulega amesema kuwa licha ya Tanzania kubahatika kuwa na rasilimali nyingi hasa zinazohusiana na uvuvi pamoja na fukwe zilizosheheni rasilimali ambazo ni fursa kwa wananchi wanaoishi kanda hizo kuweza kuwekeza na kujiongezea kipato lakini bado fukwe hizo azijatumika kikamilifu.
“Ili fukwe hizo ziweze kutumika kwa tija ni wajibu wetu sisi kama viongozi kuwa na dhamira ya dhati ya kuwasaidia wananchi hawa kwa kuwahamasisha ili kuzitambua fursa zilizopo na baadae kukuza kipato cha mtu mmoja mmoja na nchi kwa ujumla,” amesema Ulega.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya hiyo, Shaibu Ndemanga ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Lindi, amesema licha ya kipato kidogo kinachopatikana kutokana na uvuvi wa samaki mkoa huo umejipanga kuhakikisha unaboresha sekta hiyo ya uvuvi.
Amesema katika kuhakikisha eneo la ufugaji wa samaki elimu inatolewa kwa kiwango cha juu kwenye mikoa hiyo miwili ya Lindi na Mtwara na kwamba tayari imeanzisha shamba darasa katika halmashauri ya Mtama litakalotumika kuzalishia mbegu za samaki pamoja na kutoa elimu kwa wafugaji.
Nae Mbunge wa Kilwa, Ally Kasinge amesema kuwa mpango huo ulioletwa na serikali kupitia wizara ya mifugo na uvuvi inaonyesha ni kiasi gani serikali imeamua kuwashika mkono wavuvi.
“Huko nyuma sekta hii ya uvuvi ni kama vile wavuvi walikuwa wameachwa wenyewe pasipo kuwa na msaada wenye kuonekana kutoka serikalini, mathalani sisi wavuvi wa wilaya ya Kilwa tulikuwa tunatumia fursa ya bahari katika utaratibu wa kawaida lakini kwa mpango huu ambao wizara imekuja nao ni wazi kuwa wananchi wanakwenda kuelimishwa namna bora ya uvuvi na ufugaji wa mazao mengine ya bahari,” amesema Kasinge