26.9 C
Dar es Salaam
Thursday, May 26, 2022

Ulaya: Kijana aliyepania kumaliza shida ya umeme Rukwa

ASHA BANI

SERIKALI inafanya kila jitahida kuhakikisha inamaliza tatizo la umeme.

Pamoja na jitihada hizo, bado kuna changamoto ya upatikanaji wa umeme katika baadhi ya maeneo nchini.

Miongoni mwa maeneo hayo ni Mkoa wa Rukwa, ambao umeme wake umechukuliwa kutoka nchini Zambia, unaoingia kwenye gridi ya taifa.

Wakati mwingine, wananchi mkoani humo hutumia jenereta zinazo tumia mafuta ya dizeli kupata umeme.

George Ulaya, mkazi wa Sumbawanga, mkoani Rukwa, amejipatia umaarufu mkubwa baada ya kuunda mashine kubwa ya kufua umeme inayotumia upepo.

Mashine hiyo ni ya kilowati 3.5 kwasasa inatumika katika Chuo cha Walimu Rukwa, ambapo inayo uwezo wa kuwasha taa zaidi ya 300 zilizopo chuoni hapo.

Mbali na hiyo, amefunga mashine nyingine inayotumia maporomoko ya maji yenye kilowati 20 katika Shule ya Seminari Kaengesa, iliyopo Sumbawanga mjini. “Mashine hii inathamani ya Sh milioni 4.5 inao uwezo wa kuwasha umeme shuleni hapo, kwenye nyumba za walimu na kusukuma maji kwa saa 24,” anasema Ulaya.

Akizungumzia mashine inayotumia maporomoko ya maji inavyofanya kazi, anasema hufungwa kwenye eneo lenye maporomoko kuanzia mita tano hadi 60 kwa kuwa nguvu ya umeme inatokana na wingi wa maji.

Hivi majuzi, Ulaya alifanya utafiti unaolenga kuzalisha umeme kutoka Bonde la Rukwa kwenye maeneo matatu yaliyopo vijiji vya Uzia, Kalumbaleza na Nkwilo.

“Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech) imetuwezesha kwa kiasi kikubwa. Pia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ikatusaidia fedha Dola 60,000 (Sh milioni 261) ili kukamilisha miradi hiyo,” anasema.

Anasema kati ya miradi hiyo, mmoja umepata mwekezaji wa kusaidia ujenzi.

“Tutatumia mzunguko wa mita 150 na utazalisha umeme kuanzia kilowati 500,” anasema Ulaya.

Anasema ujenzi wa miundombinu ya mieadi hiyo, hauwezi kuzidi miezi sita kuanzia siku utakaoanza.

Anabainisha kuwa kampuni yake imeshapata vibali vyote vinavyowawezesha kuendelea na mradi.

Ulaya anasema mradi wa Nkwilo utasaidia kupunguza adha ya umeme mkoani Rukwa.

“Sasa hivi, Rukwa inatumia megawati nne kutoka Zambia, lakini hautoshelezi mahitaji hivyo, inatakiwa kuingiza umeme zaidi kwa sababu matumizi ni makubwa,” anasema.

Ulaya anasema matarajio yake ni kutengeneza miradi ya kusambaza umeme vijijini ili kuwasaidia wakulima kuwa na viwanda vidogo vidogo vya kusindika mazao yao.

Ulaya alianza kujipatia umaarufu mkubwa baada ya kushiriki maonesho mbalimbali yakiwamo ya viwanda vidogo vidogo (Sido) ambako alikuwa akionesha kazi zake.

Historia yake

Ulaya alianza kuona kipaji chake alipokuwa akisoma elimu ya sekondari katika Shule ya Don Bosco iliyopo Iringa,

Anasema alikuwa mdadisi mno hivyo, wakati wa likizo alikuwa akiunda vitu mbalimbali ili kupata mwanga wa kusomea nyumbani.

“Hiyo ilikuwa mwaka 1986; kijijini kwetu Senga, kulikuwa na shida ya umeme nikawa naunda jenereta inayotumia upepo ya wat 300, yenye uwezo wa kuwasha taa tano,” anasema na kuongeza:

“Watu wengi walishangazwa na kipaji changu. Nyumbani kwetu kukawa kama sehemu ya makumbusho, watu wengi walitoka sehemu mbalimbali kuja kushangaa ubunifu huo.”

Asajili kampuni

Anasema mwaka 2009 alifanikiwa kusajili kampuni yake ya kuzalisha umeme wa maji na upepo, ambapo kipindi hicho vijiji vilivyopo mkoani Rukwa havikuwa na umeme.

“Nikiwa nafanya utafiti nilikwenda kwenye maonesho ya Sido na kutembelewa na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), ambayo ilifurahishwa na ubunifu wangu, wakanisaidia vifaa mbalimbali vya kujiendeleza vyenye thamani ya Sh milioni 12,” anasema.

Anavitaja vifaa hivyo kuwa ni mashine ya kukata vyuma, mashine ya kutoboa vyuma, kuunganisha vyuma na ya kuchongea, ambavyo vilimsaidia kuboresha kazi zake kwa kuchonga vipuri vizuri zaidi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
192,379FollowersFollow
541,000SubscribersSubscribe

Latest Articles