26.6 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Ukweli kuhusu pikipiki ya maajabu Dar

pg-5aVeronica Romwald na Leonard Mang’oha, Dar es Salaam

UKWELI juu ya pikipiki iliyoko eneo la Veterinary, Temeke, inayodaiwa kuwa na maajabu umejulikana.

Juzi katika mitandao mbalimbali ya kijamii zilisambaa picha zinazoionesha pikipiki hiyo ikiwa na maelezo kuwa iliibiwa mkoani Tanga na mtu ambaye baada ya kuifikisha kituoni hapo kwa ajili ya kutafuta abiria alianguka na kufa papo hapo.

Zaidi ilidaiwa kuwa pikipiki hiyo haihamishiki wala haisogezeki.

MTANZANIA Jumamosi lilifika katika eneo hilo na kuzungumza na viongozi mbalimbali kuhusiana na pikipiki hiyo yenye namba za usajili T 684 CJZ.

Akizungumza, mmoja wa madereva wa bodaboda wa kituo hicho ambacho pikipiki hiyo imeegeshwa hapo kwa takribani miaka mitatu sasa pasipo kuibiwa, Shukuru Kiyomola, alisema kile kilichoandikwa mtandaoni hakina ukweli wowote.

“Hii pikipiki ilikuwa ikiendeshwa na mwenzetu anaitwa Frank William, hajafariki kama inavyosambazwa mtandaoni, yupo hai, mara nyingi huwa anabeba abiria usiku, lakini kwa kutumia pikipiki nyingine.

Pikipiki hii ipo hapa takribani miaka mitatu kwa sababu kuna mgogoro kati ya Frank na bosi wake,” alisema.

Alisema si kweli kwamba pikipiki hiyo haihamishiki, lakini alikiri kuwa wanaogopa kuihamisha au hata kuisogeza kwa kuhofia kudhurika kwa kupata mabaya.

“Ukiisogeza, inasogezeka, lakini tunaogopa kufanya hivyo hata mwenyewe (Frank) akiwepo, akikuona unaisogeza au hata kuikalia anakufokea uondoke, sasa hatujui ina nini na pengine ndiyo maana haijaibiwa na ipo hapa muda wote huo,” alisema.

Waandishi wa habari hii waliikagua pikipiki hiyo ambayo inaonekana kuwa kuu kuu hivi sasa na kubaini kuwa tayari imenyofolewa sehemu ya kuwekwa funguo ili kuiwasha.

Si hivyo tu, pia walijaribu kuisogeza kujiridhisha na kubaini inahamishika.

Mwenyekiti wa Umoja wa Waendesha Bodaboda wa Mtaa huo (WAMAPIME), Godliving Bahati, alisema ni kweli pikipiki hiyo ipo katika eneo hilo kwa muda mrefu.

Alisema Frank ambaye ndiye aliyekuwa dereva wake amekuwa akiwagombeza wenzake na kuacha kuisogelea au kuigusa pikipiki hiyo bila kuwaeleza sababu za msingi.

“Kwa kweli siri ya hii pikipiki anaijua Frank mwenyewe na bosi wake, hata ukimlazimisha aongee akueleze, hasemi, hilo ndilo linalosababisha hofu na mnaweza kugombana kabisa tena ugomvi mkubwa hadi watu wakaja kuwaamulia,” alisema.

Bahati alisema tayari wametoa taarifa juu ya pikipiki hiyo katika Kituo Kidogo cha Polisi- Maganga na katika Ofisi ya Serikali ya Mtaa wa Veterinary na kwamba wanasubiri viongozi waende kuiondoa.

“Kwa sababu tulishamueleza Frank afanye utaratibu wa kuiondoa, lakini hakuna chochote alichofanya na bado imeendelea kuwepo, hataki kuitoa na hana sababu za msingi anazotueleza,” alisema.

YAGEUKA MAONESHO

Waandishi wa habari hii walishuhudia pikipiki hiyo ikiwa imefunikwa pande zote, licha ya awali kuelezwa kuwa ilikuwa ikiachwa wazi.

Aidha, mbele yake kulikuwa na ubao uliokuwa unasomeka ‘Kuangalia 1,000, Kupiga picha 2,000. Hatari’.

Akizungumzia hilo, Mwenyekiti huyo alisema wamechukua uamuzi wa kuifunika pikipiki hiyo kwani tangu taarifa zake zisambae zimesababisha kero katika eneo hilo.

“Unajua tangu iliposambazwa ile picha juzi eneo hili naweza kusema kumekuwa hakuna utulivu, watu wanajaa mno, leo (jana) umekuta wachache kwa sababu tumeifunika.

“Hatujafanya hivi kwa lengo la kupata fedha, bali kurejesha utulivu kama ilivyokuwa awali, watu wamekuwa wakimiminika kuja kuishangaa,” alisema.

Alisema hata usiku imekuwa ikibaki yenyewe katika eneo hilo na hakuna mtu anayethubutu kuisogelea au hata kuiiba, licha ya wizi wa vyombo kama hivyo kushamiri katika jiji la Dar es Salaam.

Alisema wananchi ambao wamekuwa wakifika  kuishangaa pikipiki hiyo wamekuwa wakiogopa kuisogelea na hata kuigusa kwa kuhofia kudhurika.

“Wanaogopa eti watanasa au watakufa, hivyo tumeona bora tuifunike iwe kama mwali eneo hili kuwe na utulivu,” alisema.

Wakati mahojiano hayo yakiendelea, watu walianza kujaa katika eneo hilo kuishangaa pikipiki hiyo.

Mpigapicha wa gazeti hili alimuomba mwenyekiti huyo aifunue pikipiki hiyo ili aweze kuipiga picha, hali iliyozusha hofu kwa baadhi ya wananchi.

“Mungu wangu wanaifunua, waiache hivyo hivyo bwana… bora niondoke zangu, kwa kweli haya mambo yanatisha, yaani pikipiki haisogei sijawahi kuona,” alisikika mmoja wa wananchi waliofika katika eneo.

KWELI INASOGEA

Wakati hatua hiyo ya upigaji picha ikiendelea, mwandishi wa habari hii alijaribu kuisogeza ili kuthibitisha kile kilichoelezwa na ilisogezeka.

OFISI YA MTAA

Mwenyekiti wa Mtaa wa Veterinary, Ally Mwamba, alisema alipata taarifa za pikipiki hiyo tangu alipoanza kusimamia usafishaji wa mazingira kwenye mtaa huo.

“Binafsi nilianza kuiona pikipiki ile tangu wakati wa kampeni, nilikuwa nakuta vijana wameweka bendera ya Chama cha Wananchi (CUF), sasa mimi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) nikawaomba na yetu iwe inawekwa na zote mbili zikawa zinapepea pale.

“Sasa uchaguzi ukamalizika, tukaanza kutekeleza amri ya Rais John Magufuli ya kufanya usafi kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi, ndipo wale vijana wakanieleza ukweli juu ya ile pikipiki na kunitaka niwasaidie kuiondoa,” alisema.

Alisema vijana hao walimweleza kuwa imekuwapo kwa muda mrefu katika eneo hilo kutokana na mgogoro wa maslahi uliopo baina ya mmiliki wa pikipiki hiyo na dereva wake.

“Kabla ya haya yote kutokea, Frank ambaye ni miongoni mwa waanzilishi wa kituo kile alikamatwa na polisi pamoja na viongozi wenzake na wakavuliwa uongozi kwa ubadhirifu wa fedha za chama.

“Sasa tangu alipotoka ndani hakukuwa na maelewano na mmiliki wa pikipiki hiyo ambaye wamenieleza kuwa anaishi mkoani Mbeya. Walisema kulikuwa na mkataba kati ya mmiliki na dereva huyo uliomtaka aiendeshe kwa muda wa kati ya miezi sita hadi mwaka mmoja kabla ya kukabidhiwa kuwa mali yake,” alisema.

Mwenyekiti huyo aliongeza “Frank aliendesha pikipiki hiyo na kumjulisha mmiliki kuwa muda waliokubaliana ulikuwa umekwisha, hivyo amkabidhi kadi ya pikipiki hiyo, lakini mmiliki huyo aligoma na ndipo mgogoro ulipoanzia.”

Alisema alitaka kuchukua hatua ya kuiondoa pikipiki hiyo lakini ameshindwa, kutokana na kuwapo kwa mgogoro huo.

“Naogopa kuiondoa maana baadaye nisije nikajikuta na mimi najumuishwa katika mgogoro huo, nimewaeleza waje mezani wajieleze ili nichukue hatua zaidi ya kuripoti kituo cha polisi, lakini bado sijawaona,” alisema.

Mwamba alisema hata hivyo, hajawahi kusikia wala kuthibitisha iwapo pikipiki hiyo ina miujiza kama wengi wanavyoeleza.

“Ni uzushi tu, pikipiki inasogezeka toka eneo moja hadi lingine kama kawaida,” alisema.

Juhudi za gazeti hili kumpata Frank hazikuzaa matunda, lakini lilimpata aliyekuwa Katibu wa umoja huo ambaye aliondolewa pamoja naye katika uongozi.

“Frank si rahisi kumpata, sina hata namba yake siku hizi, kwani amekuwa akibadilisha kila mara, ninachojua ni kweli ana mgogoro na bosi wake na ndiyo kisa cha kila mmoja kuisusa pikipiki hiyo,” alisema.

 

KAMANDA WA POLISI

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Gilles Muroto, alipoulizwa alisema hafahamu lolote juu ya pikipiki hiyo na kuahidi kulifuatilia suala hilo.

“Sijui ndugu mwandishi wewe ndiye wa kwanza kunieleza, nitafuatilia kwa kina ukweli wa suala hili,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles