29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Ukweli kuhusu mazoezi ya Aerobics au Cardio?

aerobics1Dk. Fredirick L Mashili, MD, PhD

SINA uhakika kama Baraza la Kiswahili limeshatoa tafsiri sahihi na maneno halisi ya Kiswahili yanayobeba maana ya aerobics au cardio. Lakini hata hivyo, sina shaka kuhusu matumizi ya maneno haya katika jamii ya watu wanaopenda na kufanya mazoezi. Wengi wetu tunayatumia mara kwa mara.

Tukubaliane pia kwamba, kuna utata kidogo katika matumizi ya maneno haya mawili. Utata huu upo pia katika matumizi ya maneno haya kwa lugha ya Kiingereza. Je, maneno haya yana maana sawa, au tofauti? Na kama yana maana sawa kwanini yatumike maneno tofauti? Kwa kifupi, maneno haya yanawakilisha vitu viwili tofauti ambavyo vinahusika kuleta madiliko yanayofanana. Kwa maana rahisi, maneno haya yana maanisha kitu kimoja, na hutumika kwa kubadilishana. Mtu mwingine amezoea kutumia ‘cardio’ wakati mwingine anakuwa amezoea zaida neno ‘aerobics.’

Chukulia mfano mzuri kabisa wa mazoezi ya cardio, kutembea au kukimbia kwa mwendo wa kawaida.

Nimesema kukimbia kwa mwendo wa kawaida kwa sababu kukimbia kwa mwendo wa kasi (sprinting), kama mtu anapokimbia mita 100 au 200, hakukidhi vigezo vya kuwa cardio. Mtu anapokimbia kwa mwendo wa kawaida au kwa lugha ya kitaalamu mchaka mchaka, mambo mawili muhimu hutokea. Kasi ya mapigo ya moyo na ile ya kupumua huongezeka na kuwa juu kwa kipindi chote anachofanya mazoezi.

Ni rahisi kutambua mabadiliko haya tunapofanya aina hii ya mazoezi. Nia kubwa ya kuongezeka kwa kasi ya mapigo ya moyo na kupumua, ni  kuweza kufikisha hewa ya oksijeni katika chembe hai, hususani zile za misuli ambazo hufanya kazi ya ziada wakati wa mazoezi. Oksijeni hii ndiyo inayowezesha kupatikana kwa nguvu inayotumika wakati wa mazoezi ya cardio au aerobics.

Sasa tumesema vitu viwili, kasi ya mapigo ya moyo na ile ya kupumua, vikiwa na lengo la kupeleka hewa ya oksijeni ya kutosha kwenye misuli. Neno cardio hapa linamaanisha moyo. Limetokana na neno la kilatin ‘kardia’ likimaanisha moyo.  Hii ni kutokana na ukweli kwamba mazoezi ya aina hii huongeza kasi ya mapigo ya moyo.

Lakini pia, mazoezi haya huongeza kasi ya kupumua kwa kufanya kazi kwenye mapafu. Nia na madhumuni ni kuimarisha utumiaji wa hewa ya oksijeni. Neno aerobics, limetokana na neno la Kigiriki ‘aerobic’ ambalo maana yake halisi ni ‘yenye hewa ya oksijeni.’

 

KUTEMBEA NI MFANO MZURI WA MAZOEZI YA CARDIO/AEROBIC

Kwa maana hiyo kama tulivyoona hapo awali mazoezi ya cardio, halikadhalika yale ya aerobics, huchochewa na uwapo wa hewa ya oksijeni. Fikiria aina zingine za mazoezi ya aina hii-cardio au aerobics. Kuogelea, kucheza dansi, kuendesha baiskeli na mazoezi yote yanayohitaji kufanyika kwa kipindi cha muda fulani, kwa ujumla yanasababisha kasi ya mapigo ya moyo na kupumua kuongezeka kwa muda, hivyo kupeleka hewa ya oksijeni katika chembe hai za misuli. Unapokuwa unafanya mazoezi haya unatambua kiurahisi kwamba moyo na mapafu yako vinafanya kazi ipasavyo, tufauti na unapofanya mazoezi kama kunyanyua au kusukuma uzito. Unapofanya mazoezi ya kunyanyua au kusukuma uzito ambayo si cardio wala aerobics, japo mwanzoni utahisi moyo na mapafu kufanya kazi sana, baadaye utahisi ni misuli ndiyo inafanya kazi zaidi.

Mazoezi kama kunyanyua vyuma, kusukuma mashine, kukimbia mbio fupi kwa kasi kubwa na hata kuvuta kamba, ni tofauti kabisa na mazoezi ya cardio au aerobics. Kitaalamu mazoezi haya hujulikana kama resistance exercises, strength training, weight training au anaerobic exercises. Japo aina fulani za mazoezi ya aina hii husababisha kuongezeka kwa kasi ya mapigo ya moyo na kupumua pamoja na utumiaji wa oksijeni haraka haraka, mazoezi haya hayawezi kufanyika kwa muda mrefu hivyo kutokukidhi vigezo vya kuwa cardio au aerobics.

Kwa maana hiyo basi, mazoezi ya cardio au aerobics ni yale yanayosababisha kasi ya mapigo ya moyo, kupumua na matumizi ya hewa ya oksijeni kuongezeka kwa kipindi cha muda fulani. Ili kuweza kufanya mazoezi haya kwa muda huo. Mazoezi haya huwa ni ya nguvu  kidogo mpaka ya wastani. Mfano, huwezi kimbia kwa muda mrefu kama utakimbia kwa mbio zako zote. Huwezi beba uzito mkubwa kwa muda mrefu. Unapotembea, unaweza kutembea hata kwa saa moja.

Kwa kifupi mazoezi ya cardio au aerobics hutegemea nguvu na muda unaotumika. Kwa kuwa muda ni muhimu, maana yake ni kwamba nguvu kidogo au ya wastani hutumika ili kuweza kufanya mazoezi haya kwa muda mrefu.

Mazoezi haya hutujengea uwezo wa kufanya vitu au shughuli kwa muda mrefu. Wakati mazoezi ya cardio au aerobics yakisaidia kwa kiasi kikubwa katika ufanyaji kazi wa moyo na mapafu, hivyo kutupa uwezo wa kufanya vitendo au shughuli kwa muda mrefu, mazoezi ya kunyanyua au kusukuma uzito huimarisha misuli na mifupa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles