24.2 C
Dar es Salaam
Sunday, September 25, 2022

UKUTA WAONGEZA MAUZO YA TANZANITE MARADUFU

Na MAREGESI PAUL-DODOMA          |      


WAZIRI wa Madini, Angellah Kairuki, amesema fedha zilizopatikana baada ya kuuza madini ya Tanzanite tangu kuzungushwa kwa ukuta, yanazidi yale yaliyopatikana kwa miaka mitatu wakati kukiwa hakuna ukuta.

Akisoma hotuba ya bajeti kwa mwaka 2018/19, Kairuki alisema: “Juni 2017, mheshimiwa Spika aliunda kamati maalumu ya Bunge iliyoshughulikia shughuli za uchimbaji wa madini na uuzaji wa madini ya Tanzanite nchini.

“Kamati hiyo ilitoa mapendekezo mbalimbali, yakiwamo kuwapo kwa mfumo mpya wa udhibiti wa madini hayo.

“Kutokana na mapendekezo hayo, Septemba 20, mwaka jana, Rais John Magufuli aliagiza Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania, kujenga ukuta kuzunguka eneo la migodi ya Tanzanite iliyoko Mirerani ili kudhibiti utoroshwaji wa madini hayo.

“Kutokana na udhibiti huo, katika kipindi kifupi cha miezi mitatu ya kuanzia Januari hadi Machi, mwaka huu, wizara imefanikiwa kukusanya mrabaha wa Sh bilioni 714.67 na katika kiasi hicho, shilingi bilioni 614.67 zinatokana na makusanyo kutoka kwa wachimbaji wadogo.

“Kiasi hicho kilichokusanywa, kinazidi makusanyo ya mrabaha yaliyokusanywa kwa miaka mitatu iliyopita kutoka kwa wachimbaji wadogo.

“Nasema hivyo kwa sababu katika mwaka 2015, tulikusanya mrabaha wa Sh milioni 166.85, mwaka 2016 tulikusanya mrabaha wa shilingi milioni 71.86 na mwaka 2017,

tulikusanya mrabaha wa Sh milioni 147.14,” alisema Kairuki.

Alisema pia Serikali iko mbioni kukamilisha utaratibu wa kutangaza Tanzanite kuwa madini maalumu na utaratibu huo utakamilika katika mwaka huu wa fedha.

Pamoja na kufanikiwa katika udhibiti huo, Kairuki alisema bado kuna utoroshaji wa madini japokuwa matukio ya ukamataji wa watu wanaojihusisha na biashara haramu

ya madini hayo yamepungua.

Aliwataka wamiliki wa leseni za madini kuacha tabia ya kukwepa au kuchelewa kulipa kodi, kulipa mrabaha na tozo nyingine wanazotakiwa kulipa kwani adhabu wanayoweza kukabiliana nayo pindi wanapokiuka sheria za biashara zao ni kunyang’anywa leseni na kufikishwa mahakamani.

Kuhusu mipango ya wizara hiyo kwa mwaka huu wa fedha, alisema wamepanga kuimarisha ukusanyaji wa mapato yatokanayo na madini, kuwaendeleza wachimbaji wadogo wa madini, kuimarisha ukaguzi wa usalama wa afya katika uzalishaji wa madini na kuendeleza kuboresha mazingira ya wananchi kunufaika na madini.

Akizungumzia Shirika la Madini la Taifa (Stamico), alisema katika mwaka huu wa fedha litaendeleza mradi wa dhahabu katika Mgodi wa Buhemba, Mkoa wa Mara kwa kuanza kujiridhisha juu ya kiasi cha madini kilichopo.

“Stamico pia itaendeleza mradi wa kuchimba makaa ya mawe Kiwira, Mkoa wa Mbeya na pia inatarajia kuanza mradi wa kuchimba kokoto katika eneo la Ubena Zomozi, Mkoa wa Pwani,” alisema Kairuki akiliomba Bunge liidhinishe maombi yake ya Sh bilioni  58.9.

MAONI YA KAMATI

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Dustan Kitandula, alisema kamati yake hairidhishwi na mwelekeo wa Mgodi wa Dhahabu wa Buhemba unaomilikiwa na Serikali kupitia Stamico.

Kwa mujibu wa Kitandula, Mgodi wa Buhemba unakabiliwa na deni la Sh milioni 89.02 lililotokana na mapunjo ya mafao ya wafanyakazi wa zamani walioachishwa kazi mwaka 2007 wakati mgodi huo ulipokuwa ukimilikiwa na Meremeta.

Alisema kamati yake inaishauri Serikali ifanye tathmini ya uwekezaji katika migodi yote iliyo chini ya Stamico na pia iwe na utaratibu wa kutoa fedha za miradi ya

maendeleo iliyo chini ya wizara hiyo.

Pamoja na hayo, alisema wizara hiyo imejitahidi kuongeza ukusanyaji wa mapato katika sekta ya madini, uliotokana na kuimarika kwa udhibiti wa utoroshaji wa madini

kwa kushirikiana na vyombo vya Serikali, kuongezwa kwa viwango vya mrabaha kutoka asilimia nne hadi sita kwa madini ya metali na kutoka asilimia tano hadi sita

kwa madini ya vito.

MICHANGO YA WABUNGE

Akichangia bajeti hiyo, Mbunge wa Mtwara Mjini, Maftah Nachuma (CUF), aliitaka Serikali iweke utaratibu wa kuwaua watu watakaokamatwa na madini ya Tanzanite wakiyauza kinyume cha sheria.

“Kwanza kabisa, naiomba Serikali inunue mashine za kuchakata madini ya Tanzanite, kwa sababu kitendo cha kutoyachakatia nchini kinazinufaisha nchi nyingine ikiwamo India ambako uchenjuaji umeajiri watu laki sita.

“Pamoja na hayo, naiomba Serikali iongeze kasi ya kudhibiti utoroshwaji wa madini ya Tanzanite na wakati huo huo madini hayo yawekwe kwenye orodha ya nyara za

Serikali ili atakayekamatwa nayo auawe,” alisema Nachuma.

RASHID AKBAR

Mbunge huyo wa Newala Vijijini kupitia CCM, Rashid Akbar, aliitaka Serikali ilivunje Stamico kwa kile alichosema shirika hilo limeshindwa kusimamia sekta ya madini nchini.

Kwa mujibu wa Akbar, kitendo cha Serikali kuendelea kuwa na shirika hilo, ni kielelezo cha sekta ya madini kutolinufaisha taifa.

Aliiomba Serikali iwaelimishe wananchi ili wajue thamani ya madini yaliyoko nchini, kwa kuwa wengi wao wakiwamo wabunge hawajui aina za madini yaliyopo nchini.

CONSTANTINE KANYASU

Mbunge wa Geita Mjini, Constantine Kanyasu (CCM), aliitaka Serikali ieleze jinsi inavyoshughulikia malalamiko ya wananchi wenye nyumba zenye nyufa jirani na Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM).

Wakati huo huo, Kanyasu aliitaka Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST), kutoa taarifa za upatikanaji wa madini katika maeneo mbalimbali nchini, kwa kuwa kutokuwapo kwa taarifa sahihi za madini katika maeneo husika, kunawaingiza gharama kubwa wachimbaji.

“GST amekuwa akitoa taarifa zisizo sahihi za upatikanaji wa madini na hali hii wakati mwingine unaona ni bora uwatumie watafiti wengine kwani sababu wao GST wanafanya tafiti kwa ujanja ujanja,” alisema.

Pamoja na hayo, Kanyasu aliitaka Serikali iwashirikishe watumishi wa kitengo cha manunuzi katika halmashauri nchini wakati wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo

ili kudhibiti matumizi mabaya ya fedha.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
201,853FollowersFollow
553,000SubscribersSubscribe

Latest Articles