26.2 C
Dar es Salaam
Monday, October 3, 2022

UKUTA MIRERANI WASOMBA KIGOGO

Na Veronica Simba – Manyara


NAIBU Waziri wa Madini, Doto Biteko, ameagiza Kaimu Ofisa Madini Mkazi wa Mererani, Fredrick Girenga, kuondolewa kwenye wadhifa wake kwa kushindwa kuchukua na kutunza kumbukumbu za madini yanayotolewa kwenye geti la ukuta uliojengwa hivi karibuni kuzunguka machimbo hayo ili kudhibiti magendo kwenye biashara ya Tanzanite.

Biteko akitoa maagizo hayo kwa Kamishna Msaidizi wa Madini Kanda ya Kaskazini, Adam Juma, alisema pia ofisa huyo ameshindwa kuchukua na kutunza kumbukumbu za watu wanaoingia na kutoka kwenye machimbo hayo kupitia getini.

Alitoa agizo hilo jana, baada ya kufanya ziara ya kukagua shughuli zinazoendelea Mererani, hususani kwenye ukuta huo na kubaini udhaifu katika uchukuaji na utunzaji wa kumbukumbu za wahusika wanaoingia ndani ya eneo hilo na kutoka, pamoja na madini yanayotolewa kupitia getini.

“Rais amewekeza pesa nyingi sana hapa. Haiwezekani sisi watendaji tushindwe kujituma hata kwa mambo madogo kama haya ya kusimamia utekelezaji wa ulinzi wa rasilimali hizi, yaani tusubiri yeye aje tena kutuelekeza hata mbinu ndogo za udhibiti. Lazima tuwe wabunifu na wenye kujituma,” alisema Biteko.

Alisema mtu yeyote atakayepangwa kufanya kazi ya usimamizi wa ukuta huo, ajue macho ya Serikali yameelekezwa mahali hapo.

“Hata usipomwona waziri, naibu mawaziri, katibu mkuu na kamishna wa madini, ujue macho yetu yapo huku na usipotimiza wajibu wako kwa kiwango kinachoridhisha, tutakuwajibisha mara moja,” alisema Biteko.

Akizungumza na waandishi wa habari, baada ya kuhitimisha ziara yake, Biteko alisema udhaifu alioubaini upo kwa upande wa wizara.

Alisema hakuna rekodi yoyote inayoonyesha nani anaingia katika machimbo hayo yaliyozungushiwa ukuta, kwa muda gani, na nani amepangwa kufanya kazi ipi.

Aliongeza hata rekodi ya madini yanayotoka ndani ya machimbo hayo kwenda nje haipo.

Kutokana na hali hiyo, alisema wizara haiwezi kuruhusu mtu yeyote kuirudisha nyuma katika kusimamia rasilimali za madini, hasa baada ya jitihada zilizofanywa kuisaidia sekta hiyo kukua ili mchango wake kwenye pato la taifa uongezeke.

“Kusema kweli, hilo hatuwezi kukubaliana nalo. Ndiyo maana nimemwelekeza Kamishna wa Madini wa Kanda, tuangalie namna ya kubadilisha uongozi hapa Mirerani ili tuweze kupata mtu ambaye anaweza kusimamia vizuri,” alisema Biteko.

Alisema pia zipo taarifa za baadhi ya maofisa wa wizara hiyo waliopangwa kufanya kazi Mirerani kutokutimiza wajibu wao ipasavyo, ikiwa ni pamoja na kutokuwapo mahali pa kazi kwa muda wote wa kazi kama wanavyopaswa.

“Hili jambo haliwezi kuvumiliwa kwenye wizara yetu. Tunataka tudhibitiane na tusimamiane vizuri ili ndoto ya rais wetu aliyokuwa nayo katika kudhibiti madini haya iweze kutimia,” alisema.

Kwa upande wake, Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Profesa Shukrani Manya, alisema lengo la Serikali la kujenga ukuta huo ni kuhakikisha tatizo la kutoroshwa kwa madini linafika mwisho.

“Ziara hii imetufanya tubaini kuwa udhibiti wa utoroshaji madini uliopo unapaswa kuwekewa mkazo kwa kuhakikisha maelekezo ya Serikali yanayotaka kila idara husika kuweka mbinu zaidi za udhibiti, yanatekelezwa ipasavyo,” alisema Profesa Manya ambaye pia ni kamishna wa madini.

Ukuta unaozunguka migodi ya madini ya Tanzanite Mirerani, ulizinduliwa rasmi na Rais John Magufuli, Aprili 6, mwaka huu, kufuatia agizo alilolitoa yeye mwenyewe kama njia ya kudhibiti utoroshwaji wa madini hayo adhimu.

Ulijengwa baada ya Bunge kuunda kamati iliyoongozwa na Biteko kuchunguza biashara ya madini hayo na yale ya almasi ambayo iliibua madudu mengi.

Mauzo ya Tanzanite duniani yanafikia Dola za Marekani milioni 50.

Tanzanite ni jiwe lenye miaka milioni 600 na iligundulika Mererani mwaka 1967.

mwisho

 

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
202,573FollowersFollow
554,000SubscribersSubscribe

Latest Articles