26.6 C
Dar es Salaam
Sunday, October 1, 2023

Contact us: [email protected]

CUF YAADHIMISHA MAUAJI YA 2001 KWA MAJUTO

JONAS MUSHI

Na ASHA BANI

-DAR ES SALAAM

ATHARI ya mgogoro ndani ya Chama cha Wananchi (CUF), imejidhihirisha kwa mara nyingine tena jana wakati chama hicho kikiadhimisha miaka 16 ya mauaji ya wafuasi wake yaliyofanywa na Jeshi la Polisi mwaka 2001.

Kila upande katika pande mbili zinazotofautiana ndani ya chama hicho zilifanya maadhimisho hayo peke yake, huku Mwenyekiti wa CUF anayetambuliwa na msajili wa vyama vya siasa, Profesa Ibrahim Lipumba, akitumia fursa hiyo kujutia mgogoro unaoendelea kukitafuna chama hicho.

Upande wa Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad, ulitoa taarifa kupitia vyombo vya habari ukipinga ukiukwaji wa haki za binadamu na kulaani wote wanaojaribu kuirejesha nchi katika misingi ya chuki iliyosababishwa na dhuluma.

 

PROFESA LIPUMBA

Akizungumzia maadhimisho ya mauaji hayo yaliyotokana na mgogoro wa kisiasa wa mwaka 2001 ambayo huadhimishwa kila mwaka Januari 27, Profesa Lipumba alikiri kuwa mgogoro ndani ya chama hicho umekirudisha nyuma huku akimtaka Katibu Mkuu wake, Maalim Seif kukubali mazungumzo.

 “Awali tulidhani tumepiga hatua baada ya maridhiano ya mwaka 2010, lakini sasa tumerudi nyuma. Nasononeshwa kuona tuna mgogoro usio na sababu ambao unasababishwa na kutoheshimu katiba. Tunapokuwa na mgogoro ni vizuri kuzungumza na kusameheana kama ambavyo mwenyewe (Maalim Seif) amewahi kusema,” alisema Lipumba.

Alimtaka Seif asiogope kurejea ofisini kwake (Buguruni) kwani kuna amani na ulinzi wa vijana wa Blue Guards na kwamba walipewa vitambulisho na Seif mwenyewe.

Lipumba ambaye alirudia kueleza sababu za kujiuzulu na kisha kurejea tena katika nafasi yake, alisema Seif akifika ofisini ataelezwa na Naibu Katibu Mkuu, Magdalena Sakaya, mambo yanayoendelea likiwamo suala la ruzuku.

Alisema ni vyema kumaliza mgogoro huo ili kuendelea kuimarisha muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwani hauwezi kuwepo kama kutakuwa na vyama vilivyogawanyika pande mbili.

Alitaja sababu nyingine iliyokirudisha nyuma chama hicho kuwa ni kufutwa kwa uchaguzi wa Zanzibar wa mwaka juzi na chama kushindwa kudai haki yake mahakamani kwa kile alichodai Seif aliwazuia mawakili kufungua shauri hilo.

Kwa upande wake aliyewahi kuwa Mbunge wa CUF, Mohamed Habib Mnyaa, alisema licha ya mgogoro wa CUF kufikishwa mahakamani, hautatatuliwa hata Mahakama ikitoa haki kwa upande mmoja kushinda.

CUF YA MAALIM

Kwa upande wake CUF ya Maalim ilitumia maadhimisho hayo kutuma salamu kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuitaka kuacha kutumia nguvu na vyombo vya dola katika chaguzi mbalimbali sambamba na kukandamiza haki za wapiga kura.

Naibu Mkurugenzi wa Haki za Binadamu  na Sheria, Pavu Abdalah Juma, alisema chama hicho kinalaani mauaji ya raia wasio na hatia na vitendo vyote vya ukiukwaji wa haki za binadamu.

Pamoja na hilo, pia chama hicho kilimtaka Rais Dk. John Magufuli kutotumia nguvu kubwa katika kuendesha shughuli za kidemokrasia na uchaguzi katika nchi.

Akizungumzia maadhimisho hayo, Pavu alisema wanachama na wapenzi wa chama hicho walikuwa na haki ya kudai kupatikana kwa katiba mpya na Tume Huru za Uchaguzi –NEC na ZEC lakini  Jeshi la Polisi walitumia nguvu katika   kuwazuia na kusababisha mauaji ya wafuasi wa CUF takribani 45 waliotambuliwa na Tume ya Hashim Mbita.

Povu alisema baada ya historia hiyo ya mauaji kulifanyika na juhudi za mwafaka wa kisiasa uliomshirikisha Maalim Seif Sharif Hamad na Rais Mstaafu, Dk. Amani Abeid Karume, hivyo kuwafanya Wazanzibari kuwa kitu kimoja.

 “Ni kutokana na juhudi za Maalim Seif na Dk. Karume waliopata ridhaa na ushirikiano wa kutosha kutoka kwa Wazanzibari, walioweza kuirejesha Zanzibar katika hali ya amani na utulivu baada ya uhasama uliodumu kwa kipindi kirefu miongoni mwa wananchi.”

Alisema kutokana na hilo, viongozi hao wanapaswa kuheshimiwa na kuenziwa kutokana na juhudi  waliyoifanya kuitoa Zanzibar katika dimbwi la uhasama na mtafaruku wa kisiasa na kijamii miongoni mwa wananchi.

Pavu alisema licha ya maridhiano hayo, lakini kuna viongozi ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) wameshindwa kujifunza na kutaka kuirejesha Zanzibar ilikotoka.

Alieleza kuwa wakati jana wakiadhimisha kumbukumbu hiyo kwa huzuni na majonzi ya kupotelewa kwa ndugu zao kwa makusudi, Wazanzibari wamerejeshwa tena katika mgogoro wa kisiasa na kusababisha uhasama, chuki na mkwamo wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Alisema hali iliyopo sasa inawafanya wananchi waishi kwa hofu ya usalama wao kutokana na vitendo vinavyofanywa na vyombo vya dola na vikosi vya SMZ.

Katika taarifa hiyo ametajwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi-ZEC, Jecha Salum Jecha, kuwa ndiye mtu aliyeirejesha nchi katika dhahama baada ya kudaiwa kushinikizwa kufuta matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar uliofanyika Oktoba 25, 2015.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,770FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles