26.5 C
Dar es Salaam
Wednesday, January 26, 2022

UKOSEFU VYUMBA VYA MADARASA UNAVYOKWAMISHA ELIMU MKINGA

Na SUSSAN UHINGA,

WILAYA ya Mkinga iliyopo mkoani Mkoa ina halmashauri 11 mojawapo ikiwa ni Mkinga yenyewe.

Katika matokeo ya darasa la saba mwaka jana, wilaya hiyo ilishika nafasi ya mwisho.

Hivi majuzi gazeti hili lilifika wilayani humo ili kujionea hali halisi ya elimu na kufahamu kwanini kiwango cha elimu kipo chini kiasi hicho.

Wilaya ya Mkinga yenye shule za msingi 80 ambazo ni za Serikali, zina jumla ya wanafunzi 30,156 wakiwamo wavulana 15,399 na wasichana 14,757.

Pia kuna shule moja ya msingi ambayo ni ya binafsi inayofundisha kwa lugha ya Kingereza ambayo ina darasa la kwanza hadi la saba.

Kaimu Ofisa Elimu Msingi wa wilaya hiyo, Shabani Maliwa anaeleza sababu ya Mkinga kushika mkia katika matokea ya darasa la saba.

Anasema sababu mojawapo ni kuwapo kwa miundombinu mibovu, hasa vyumba vya madarasa, upungufu wa walimu na wazazi kutokuwa na mwamko juu ya suala la elimu.

Anasema kwasasa vyumba vilivyopo ni 281 huku uhitaji ikiwa ni 741; jambo ambalo linasababisha watoto kulundikana darasani.

Anataja changamoto nyingine kuwa ni matundu ya vyoo, ambapo kwa sasa yaliopo ni 869 wakati kunahitajika matundu 1,340 ili kuweza kukidhi mahitaji.

Nyumba za walimu, upungufu wa walimu pia ni tatizo, wilaya nzima ina jumla ya walimu 551 huku uhitaji ukiwa ni 773 hivyo wanahitajika walimu 222 ili kuendana na idadi ya shule na wanafunzi.

Maliwa anasema mbali na changamoto hizo, pia kuna tatizo la wazazi kutojitolea katika kufanikisha mahitaji mbalimbali yanayohusu elimu, ikiwamo ujenzi wa miundombinu ya shule.

“Wananchi wa Mkinga ni wagumu kutoa ushirikiano hasa katika kujitolea kuchangia ujenzi wa vyumba vya madarasa, nyumba za walimu na matundu ya vyoo, jambo ambalo linachangia kudhohofisha elimu Mkinga,” anasema.

Maliwa anaeleza mikakati waliyojiwekea ili kuboresha kiwango cha elimu kuwa ni pamoja na kufanya mikutano na viongozi mbalimbali wa elimu pamoja na Tume ya Utumishi ya Walimu (TSC) na walimu wote wa shule za msingi.

Katika mkutano huo, pamoja na mambo mengine wamejadili nini kifanyike ili kupata suluhisho la kudumu.

Pia kamati ya taaluma ya wilaya imepewa jukumu la kusimamia kikamilifu ufundishaji shuleni, pia shule zote zitafanya mtihani mmoja kwa madarasa yoote katika muhula wa kwanza na wa pili wa mosomo ili kuwaondolea watoto woga wa kufanya mtihani wa Taifa.

Shule ya Msingi Mbuta  iliyopo Kijiji cha Mbuta wilayani Mkinga, ni moja kati ya shule ambazo wanafunzi wake huwa wanafeli kwa kiwango kikubwa.

Akizungumzia suala hilo, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Anthon Mganga anasema shule yake ina jumla ya wanafunzi 231 ambao wote wanasoma katika vyumba viwili tu vya madarasa.

Shule hiyo yenye darasa la kwanza hadi la saba, ina vyumba viwili vya madarasa huku ikiwa na wanafunzi 231.

Mwalimu Anthon anasema hali hiyo huwalazimu kuwachanganya wanafunzi wa madarasa tofauti katika chumba kimoja na kuwafundisha kwa pamoja.

“Wanafunzi hawa wanatoka katika vijiji tofauti, wengi wao wanatoka katika familia za wafugaji hivyo tukisema waje kwa awamu yaani wengine waingie mchana, basi hawatakuja kutokana na mazingira wanayoishi watoto hawa,” anasema.

Anasema katika madarasa hayo mawili waliyonayo, huwa wanawapanga chumba kimoja darasa la kwanza na la tatu na kingine ni darasa nne na la sita. Wanafunzi wa darasa tano na saba wao hukaa nje wakisubiria wenzao wamalize kufundishwa ndipo nao huingia darasani.

Akizungumzia jinsi wanavyofundisha, Mwalimu Anthon anasema kuwa anapoingia darasani huwaamuru wanafunzi wa darasa la kwanza wainamishe vichwa chini huku wenzao wa darasa la tatu wakielekeza macho ubaoni ili wamsikilize mwalimu.

“Imetulazimu kubuni mbinu hii ya kuwaweka pamoja ili tusiwakose kabisa, maana bila kufanya hivi wanafunzi hawatakuja shule.

“Awali tulikuwa na chumba kimoja tu na hali ilikuwa hivyo hivyo ya ufundishaji, kwa sasa tunashukuru tumepata chumba kingine kilichojengwa kwa fedha za mfuko wa jimbo,” anasema.

Anasema wazazi hawatoi ushirikiano wowote kwa kuwa bado hawajatambua umuhimu wa elimu, kwamba hawapendi kujitoa hasa katika shughuli za kuchangia ujenzi wa miundombinu.

Leonard Shuza ambaye ni mkazi wa karibu na shule hiyo, anasema kuwa huwa anawahamasisha wazazi kujitolea kujenga miundombinu ili wanafunzi wapate elimu katika mazingira bora.

Anasema jambo hilo huwa gumu kwa kuwa wanakijiji hao wengi wao hujishughulisha na kilimo na ufugaji hivyo hutumia muda mwingi kwenda mashambani na kuchunga mifugo yao, kwa hiyo hukosa muda wa kuchangia shughuli za maendeleo.

“Binafsi naumia mno kuona watoto wetu wakisoma kwenye mazingira haya, lakini hatuna jinsi,” anasema.

Naye Mbunge wa Jimbo la Mkinga, Dunstun Kitandula anasema ili kuhakikisha kiwango cha elimu kinapanda, amehakikisha fedha yote ya mfuko wa jimbo imejielekeza katika kuboresha miundombinu ya elimu pamoja na kuhamasisha wananchi kujitolea pale inapobidi kufanya hivyo.

“Jambo hili huwa linanihuzunisha mno, hivyo nimejipanga pamoja na watendaji wa halmashauri kuhakikisha suala hili linakwisha.

“Ninapokuwa jimboni mara nyingi huwa nahamasisha watu kuchangia elimu, hivyo huwa tunajitolea nguvu zetu kwa kubeba mchanga, matofali, mawe mimi na wananchi wenzangu na kupeleka katika ujenzi.

“Wananchi wa Mkinga ni wasikivu na waelewa, hivyo nina imani tutafanikisha kuboresha elimu Mkinga,” anasema.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
176,803FollowersFollow
531,000SubscribersSubscribe

Latest Articles