30.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Ukizembea kumeza dawa Kifua Kikuu kinakuwa sugu

mchoro-unaoonyesha-mapafu-ya-mwanadamu-yaliyoathiriwa-na-ugonjwa-wa-kifua-kikuuUpendo Mosha, Moshi

UGONJWA wa Kifua Kikuu (TB) ni miongoni mwa magonjwa yanayosumbua katika Mkoa wa Kilimanjaro na kusababisha kuwa miongoni mwa mikoa 10 nchini inayoongoza kwa kasi.

Takwimu zinaonyesha kuwa katika kipindi cha mwaka 2015 kulikuwa na wagonjwa 2,414 wa Kifua Kikuu mkoani humo.

Takwimu hizo zinaonyesha kasi ya ugonjwa huu bado iko juu ikilinganishwa na jitihada ambazo zimekuwa zikifanywa na serikali katika kuhakikisha inapambana na ugonjwa huo ambao ni wa tatu kuongoza kwa vifo ukitanguliwa na Malaria na Ukimwi.

Mbali na ugonjwa huo kuonekana kuwa bado ni hatari, wagonjwa wengi wamekuwa wakikwepa kutumia dawa hali inayosababisha wengi kupata kifua kikuu sugu.

Ugonjwa huo ni wa kuambukiza na wanaombukizwa zaidi ni watu wenye upungufu wa kinga mwilini kama wenye Ukimwi, kisukari, utapiamlo, watumiaji wa dawa za kulevya  na watoto kutokana na kinga zao kuwa chini.

Mratibu wa Kifua Kikuu Mkoa wa Kilimanjaro, Dk. Manase Chelangwa, anaeleza namna ugonjwa huo unavyo athiri jamii ya Watanzania na kuangamiza nguvu kazi ya taifa.

Dk. Manase anasema mbali na ugonjwa huo kuitesa jamii kubwa ya Watanzania, watalamu wa afya nao wamekuwa miongoni mwa watu ambao wapo hatarini kupata maambukizi.

Anasema mwaka huu pekee jumla ya wataalamu wa afya 13, wakiwemo madaktari, wauguzi na wahudumu wa maabara mkoani humo wamebainika kuugua ugonjwa huo.

Anasema si jambo la ajabu watumishi wa afya kuambukizwa ugonjwa huo kwa sababu nao wako kwenye jamii na wanaishi katika maeneo hatarishi ya ugonjwa huo.

“Katika kipindi cha mwaka huu wahudumu 13 wa afya wameugua ugonjwa huu katika mkoa wetu, ijulikane kuwa nao ni sehemu ya jamii hivyo wanaweza kupata ugonjwa huu katika eneo lolote hata kwenye msongamano,” anasema Dk. Chelangwa.

Anasema maambukizi  ya ugonjwa huo bado yapo juu kutokana na baadhi ya wagonjwa kuchelewa kufika hospitali ili  kupata matibabu mapema hali ambayo inasababisha ugonjwa kuwa sugu na kusababisha vifo.

Anasema wako wagonjwa ambao wamekuwa wakifika hospitali kuchukua vipimo na kukimbia majibu, hali inayowafanya kuendelea kuambukiza pindi wanapokuwa kwenye maeneo hatarishi ikiwemo kwenye msongamano wa watu.

“Zipo changamoto kadhaa ambazo zinatukabili katika mkoa wetu na kubwa ni kuwepo kwa baadhi ya wagonjwa ambao hawazingatii dozi. Hii ni hatari sana na inafifisha jitihada zetu za kutokomeza maambukizi ya ugonjwa huu,”anasema Dk. Chelangwa.

 

HOSPITALI YA MAWENZI

Akizungumzia namna wanavyotoa matibabu kwa wagonjwa wanaolazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kilimanjaro (Mawenzi), anasema wagonjwa wamekuwa wakitengewa kona katika wodi za wagonjwa wengine.

“Kwa namna wanavyowatenga kwenye kona na kuhakikisha kunakuwa na hewa ya kutosha, hawawezi kuambukiza. Suala la kutengwa halina msingi sana, jambo la muhimu ni kitoa elimu kwa jamii, wahudumu wa afya na wagonjwa waliopo katika wodi.

“Pale Mawenzi katika kila wodi kuna kona ambayo tumetenga kwa ajili ya wagonjwa hawa, lakini mgonjwa akishaanza matibabu baada ya wiki mbili hawezi tena kuambukiza ugonjwa huo…suala la msingi hapa ni kutoa elimu,” anasema.
Dk. Chelangwa anasema elimu kuhusu ugonjwa bado inahitajika kutolewa ili kujenga uelewa kwa jamii na kuwezesha wananchi kuchukua tahadhari.
“Sote tunatambua kuwa ugonjwa huu unaenezwa kwa njia mbalimbali na kuu ni njia ya hewa, hivyo maeneo ya msongamano kama sokoni, vyombo vya usafiri, nyumba za ibada na hata kwenye mikutano kama kuna mtu mwenye ugonjwa huu anaweza kuambukiza, ni lazima wananchi wapewe elimu ya kutosha,” anasema.
Mratibu huyo anawataka wananchi kutambua kuwa gharama za matibabu ya ugonjwa huo ni kubwa, ambapo mgonjwa sugu mmoja hutumia kati ya Sh milion15 hadi 20 ili aweze kupona huku wagonjwa wa kawaida wakitumia Sh milioni tano.

Ipo haja ya wagonjwa wa kifua kikuu kuzingatia elimu na ushauri wa wataalamu ili kuepuka maambukizi mapya na kulipunguzia taifa gharama kubwa ambazo imekuwa ikizitumia kutibu wagonjwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles