26.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

UKIWA HIVI MWANAMKE HABANDUKI KWAKO!

MAPENZI ni sanaa ambayo kwa hakika haitaki hasira hata kidogo. Ubunifu, utulivu wa akili na utundu binafsi ni kati ya mambo ya muhimu sana ambayo ukizingatia utaweza kumfanya mwezi wako afurahie uhusiano wenu.

Hata hivyo, ukweli utaendelea kubaki vilevile kuwa, wanaume wengi hawapo makini sana kuangalia namna ya kumfurahisha mwanamke. Wengi akili zao huishia kuhusu namna ya kuhakikisha anaheshimika faragha, baasi!

Hayo siyo mapenzi. Ni zaidi ya hivyo. Kwa bahati nzuri ni kwamba, mwanamke huvutiwa na mambo madogo kabisa, ya kawaida ambayo mwanamume anaweza kuyadharau tu.

Je, unajua mambo muhimu ambayo huwachizisha sana wanawake? Yapo mengi lakini hapa nimekutayarishia yale ya muhimu zaidi.

 

USAFI BINAFSI

 Asilimia kubwa ya wanawake wanapenda sana usafi. Ni aghalabu sana kukutana na mwanamke asiyejipenda. Ndiyo maana wanaitwa mapambo ya nyumba au la nyumba! Ni kwa sababu ya hulka yao ya kupenda sana usafi.

Mwanamke anavutiwa sana na mwanaume mtanashati. Usafi wako unamfanya ajiamini kuwa na wewe. Hata nyumbani kwako, lazima uishi katika nyumba safi. Hata anapokuja kukutembelea, anakuta mazingira masafi kuanzia sebuleni hadi chumbani.

Anapokukuta katika hali ya usafi, inakuwa rahisi zaidi yeye kuanzia hapo alipokukuta na kuendelea mbele.

 

KUJIAMINI

Mwanamke anajisikia salama zaidi akiwa na mwanaume ambaye anajiamini – mwenye uwezo wa kutetea hoja zake na kujieleza sawia. Siyo anayebabaika. Suala la msimamo binafsi, kwa mwanamke ni kubwa kuliko hata kumnunulia manukato mapya!

Mathalani unakuwa naye katika mtoko, angependa kukuona ukiwa katika hali halisi ya maisha yako, usiyeyumbishwa na mwenye kutoa maamuzi yasiyoyumba.

Wakati mwingine, mwanamke anaweza kukupima hata katika jambo ambalo amekosea yeye, ataangalia unavyotoa maamuzi yako, lakini pia atafuatilia kuona kama utakuwa mwepesi wa kuyabadilisha.

Anataka kuona msimamo wako muda wote. Mwenye kujiamini na mawazo yasiyo na matege wala makengeza!

 

KUJITETEA

Kipengele hiki hakina tofauti kubwa sana na kilichopita, lakini hapa ni kwenye upande wa kujitetea zaidi. Wakati unapodai haki yako mbele ya mwanamke wako, suala la kujitetea linapewa nafasi kubwa sana.

Wanawake hawapendi kuwa na wanaume ambao wapo tayari kuonewa. Wanataka wenye uwezo wa kusimama kidete kuona haki zao hazichukuliwi kirahisi.

Hili si suala la kutetea tu haki yako pekee kama mwanaume, bali inapobidi kusimamia haki ya mwanamke wako. Nisieleweke vibaya katika hili, lakini mwanaume imara ni yule ambaye ana nguvu – anafanya mazoezi na ambaye yupo tayari kwa lolote!

Inapowezekana, uwe na uwezo wa ‘kuzichapa’ ikiwa mtakutana na vibaka au watu wabaya wenye lengo wa kukudhuru/kuwadhuru au kumdhuru mpenzi wako.

Mwanaume aliye ‘fiti’ ni chaguo la wanawake wengi. Si mnyonge. Mpole kupitiliza na aliye tayari kuonewa! Huyu hana nafasi.

 

KUJALI

Wanawake wanapenda sana wanaume wanaojali. Wanawaona wao ni kila kitu na wanaotoa kipaumbele kwao. Kama huna tabia hiyo, ujue upo katika nafasi kubwa ya kumkwaza mpenzi wako. Mjali mpenzi wako kwa kila hali.

Kumjulia hali kila wakati na kutaka kujua maendeleo yake, kutakupa nafasi kubwa sana ya kuendelea kudumu katika uhusiano hai.

 

UKARIBU

Kati ya vitu vinavyowapa mshawasha mkubwa wanawake ni pamoja na kusogezwa karibu. Hapa ni kuwa naye katika mambo mengi unayoyafanya kila siku.

Ni vizuri kuwasiliana naye mchana, ukitaka kujua aina ya chakula alichokula siku hiyo au ikiwezekana mchagulie. Ni mambo madogo sana lakini yanayoongeza nakshi katika mapenzi.

Yapo mengi sana ambayo kwa kuyafanya utakuwa umemsogeza mpenzi wako karibu yako. Hebu tumia ubunifu wako ili uweze kuteka hisia za mwenzi wako kisawasawa.

Wiki ijayo tutaendelea na mada hii, USIKOSE!

 

Jiandae kupata kitabu changu kipya cha SIRI ZA MAISHA YA NDOA YENYE FURAHA kitakachokuwa mitaani hivi karibuni.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles