28.7 C
Dar es Salaam
Sunday, November 28, 2021

Ukitaka kupata mwenza sahihi anza kubadili mwenendo wako

Na CHRISTIAN BWAYA

MAISHA yana mitihani mingi. Sitotoa mifano. Lakini mtihani ulio mkubwa zaidi, kwa maoni yangu, ni ule wa kumpata mwenzi wa maisha. Nadhani tunakubaliana kimsingi kuwa ukiacha uhusiano wa kifamilia, ndoa ndio uhusiano wa kudumu zaidi unaoweza kuanzishwa. Tunaweza kuchagua marafiki, kuwa na marafiki wa karibu mkaelewana nao, lakini utafika wakati mtapoteana.

Kazini unaweza kuwa na watu mnaofanya kazi kwa karibu. Lakini unaweza kufika mahali ukaondoka hapo na mkasahauliana na watu mliofanya kazi kwa karibu.

Pasipokutoa mifano mingi, ndoa inabaki kuwa uhusiano wa kudumu anaoweza kuuchagua mwanadamu. Nafahamu kuna familia, lakini ni ukweli kwamba mama, baba na ndugu wa damu, huwachagui. 

Unazaliwa unawakuta. Tofauti na familia, ndoa inabaki kuwa uhusiano wa karibu zaidi ambao ni matokeo ya uamuzi wako mwenyewe. Mke au mume huzaliwi naye.

Huyu ni mwenza wa maisha unayempata kwa hiyari yako mwenyewe kwa kutumia vigezo ulivyojiwekea.

Ingawa nafahamu uwezekano wa watu kuachana kwa sababu mbalimbali, ni ukweli kwamba hata mnapolazimika kuachana, maumivu yanayoambatana na uamuzi huo huwa ni makubwa.

Gharama ya kuachana na mke/mume ni wito kwa kijana anayefikiria kuingia kwenye ndoa, kuwa suala la ndoa linahitaji kuchukuliwa kwa uzito unaostahili. 

Sio siri, ndoa nyingi zinafukuta. Lakini tunafahamu pia matatizo mengi yanayowasumbua watu walio kwenye ndoa huanza mwanzoni kabisa mwa uhusiano wao.

Ukizungumza na wanandoa wanaopitia mitafaruku mizito ya ndoa, unaweza kushangaa namna mambo yalivyobadilika hatua kwa hatua.

Ukiwauliza na wakapata ujasiri, watakuambia vile walivyokutana kwa mapenzi makubwa.

Urafiki wao ulikuwa mzito kiasi kwamba kama ungewaambia kuna siku wangefikia kutishiana kuachana wasingekubaliana.

Wengine walipendana kiasi kwamba hata kusikiliza maonyo ya watu walioona dalili ya changamoto mbele yao hawakusikiliza. Mapenzi yalikuwa na nguvu kubwa ya kuwafumba macho wasiweze kusikiliza chochote kilichokuwa kinyume na mapenzi yao.

Kilichokuwa muhimu kwao, kwa wakati huo, ni mapenzi na maisha yao, mengine yote yaliyokuwa kinyume na hilo yaliitwa majungu, roho mbaya, kutokutakiana mema na lugha nyingine hasi.

Sasa mtu unajiuliza, nini kinatokea hadi mapenzi haya yanapotea na watu wanageuka kuwa maadui? Kwanini mtu mliyekuwa hamlali mkiongea usiku kucha kwa simu, mtu uliyekuwa unaweza kutembea umbali mrefu kwa mguu ukamwone japo sura yake urudi nyumbani, baadae anageuka kuwa shubiri unayotamani usingewahi kuonana nayo?

Unakutana na mtu unamwona kama mwanamume /mwanamke wa maana anayekufaa, mnaanza kuwa karibu, mapenzi yanawaka moto, hatimaye mnaoana.

Unashangaa baadae, lahaula, hamuongei kama mlivyokuwa mkiongea, hamuwasiliani kama mlivyokuwa mkiwasiliana, hamsameheani kama mlivyokuwa mkisameheana. Nini kinakuwa kimetokea? 

Majibu ni mengi. Lakini moja ni kwamba ndoa ni uhusiano wa karibu unaofunua uhalisia wa mwenzako.

Nje ya ndoa wakati mwingine ni vigumu kumfahamu mtu kwa sababu hampo karibu kivile.

Nje ya ndoa kuna ubondia mwingi. Kuna mambo mengi hamuwezi kushirikiana nje ya ndoa.

Ukaribu wenu nje ya ndoa, una mipaka. Lakini mnapoingia kwenye ndoa mnajikuta mkilazimika kuwa karibu. Ukaribu huo ndio hasa unaokufanya ugundue unayeishi naye siye yule uliyekuwa unawasiliana naye usiku kucha.

Ukaribu huo unakufanya ugundue kumbe unayeishi naye siye yule aliyekuwa na mapenzi makubwa kwako, aliyekuwa mwepesi kuomba msamaha, aliyekuwa akifanya kila linalowezekana kuhakikisha unakuwa mtu mwenye furaha.

Ukaribu wa kwenye ndoa unamfunua mwenzako, unagundua kumbe tabasamu lake lilificha mengi. Utanashati, ucheshi wake, mapenzi yake, ilikuwa sura inayoficha ukatili, ubabe, kisasi, kutokujali hisia za mwingine na tabia nyingine zisizovumilika. Unajiuliza, imekuwaje yule mchumba mcha Mungu ageuke kuwa mume asiyejali ibada? Imekuwaje yule mchumba mwaminifu ageuke kuwa mke asiyejiheshimu, jeuri anayeona fahari kubishana? Imekuwaje?

Sehemu ya tatizo ni vile ulivyokuwa wakati unakutana naye. Ingawa natambua kwamba mwanadamu ni kiumbe anayebadilika kulingana na mazingira, bado kuna ukweli kwamba mara nyingi huwa tunapata kinachofanana na sisi.

Kuna ukweli kwamba watu wengi huvaa sura tofauti na uhalisia wao wanapokuwa wanaanzisha uhusiano. Binti anayetaka kuolewa na kijana mcha Mungu anaamua kuonekana ni mcha Mungu hata kama kiukweli hana ucha Mungu wowote. Kijana anayetaka kumpata binti mwenye kuthamini watu wenye uwezo wa kifedha anajiweka kwa namna inaayofanana na matarajio ya binti.

Naamini unaelewa ninachojaribu kukisema hapa. Vijana wengi huingia kwenye uhusiano wakiwa bandia. Kuna namna fulani watu hubeba sura fulani kwa ajili ya kuwafurahisha wale wanaowataka.

Mtu yuko tayari kubadili mfumo wake wa maisha, misimamo aliyonayo, kwa ajili ya mapenzi.  Watu wengi wanafanya makosa hapa. Wanakuwa bandia lakini wanashangaa kwa nini wanakutana na bandia. Usinielewe vibaya.

Hoja yangu ni rahisi. Jitahidi kuwa mtu bora zaidi ya ulivyo lakini usilazimike kuigiza usivyo. Pambana kuwa kijana bora lakini usiigize maisha yasiyo ya kwako. Usilazimike kuwa mtu bandia ili ufanane na aina fulani ya watu.

Bandia ina utumwa. Bandia haidumu. Mbaya zaidi, bandia huvutia bandia. Ukianza na tabia bandia, mwonekano bandia, mawazo bandia, itakugharimu mbele ya safari. Unapotafuta mwenzi wa maisha jitahidi kuwa wewe. Simamia kile unachokiamini, ishi maisha yanayolingana na uhalisia wako. Usijaribu kuwa mtu tofauti na vile ulivyo. Mtu sahihi atakupenda vivyo hivyo ulivyo. 

ITAENDELEA

Mhadhiri wa Saikolojia Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge (MWECAU). Twitter: @bwaya Simu: 0754870815

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
167,206FollowersFollow
526,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles