23.7 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Ukistaajabu ya Profesa Ndalichako utayaona ya TCU

Waziri wa Elimu, PrOFESA Joyce Ndalichako.
Waziri wa Elimu, Profesa Joyce Ndalichako.

NA JUSTIN DAMIAN,

TUME ya Vyuo Vikuu nchini (TCU), wiki iliyopita ilitangaza kushusha viwango vya kujiunga na elimu ya juu (GPA) kwa wahitimu wa ngazi ya stashahada kutoka 3.5 hadi 3.0.

Bila kueleza sababu ya kufikia uamuzi huo, TCU ilisema kushushwa kwa viwango hivyo kumelenga kuruhusu idadi kubwa ya wanafunzi kudahiliwa katika vyuo vikuu mbalimbali nchini.

Itakumbukwa kuwa, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako, aliivunja Bodi ya TCU Mei mwaka huu, kwa madai kwamba imedahili wanafunzi wasio na sifa kujiunga na vyuo vikuu.

Hatua ya Profesa Ndalichako kuvunja bodi ya TCU, ilivuta hisia za wengi huku baadhi ya watu wakihoji mustakabali wa elimu ya juu ambayo ndiyo inayozalisha wataalamu katika fani mbalimbali.

Binafsi niliridhika na hatua ya kuvunjwa kwa bodi hiyo kwa kuwa ilishindwa kusimamia sheria na kanuni katika kudahili wanafunzi na hivyo kujikuta ikidahili ‘vilaza’.

Wakati Tanzania ikielekea kuwa nchi ya uchumi wa kati, bado inakabiliwa na changamoto nyingi. Moja kati ya changamoto hizo ni upatikanaji wa rasilimali watu au wataalamu bora  katika fani mbalimbali ambao wanahitajika. Wataalamu bora wanaweza kupatikana endapo mfumo wa elimu utakuwa imara na hivyo kuweza kuzalisha wahitimu watakaoweza kushindana katika soko la ajira.

Lakini katika mazingira kama haya ya sasa ambapo TCU inasema inashusha viwango vya kujiunga na elimu ya juu ili kuruhusu idadi kubwa zaidi ya wanafunzi kudahiliwa, ni wazi kuwa ndoto ya kuwapata wahitimu wenye ubora inafifia kwa kuwa sasa umuhimu umewekwa zaidi kwenye wingi wa wanafunzi na wala si ubora tena.

Wadau wengi wa elimu wamekuwa wakionyesha wasiwasi wao juu ya elimu ya Tanzania kwa ujumla wake kutokana na kutokuwa na usimamizi thabiti na unaoeleweka, jambo ambalo limekuwa na athari kubwa kwa aina ya wahitimu wanaowazalisha.

Hiki kilichofanywa na TCU kushusha viwango vya udahili kwa wahitimu wa ngazi ya stashahada, ni jambo ambalo linakuwa vigumu kuingia akilini kama kweli nchi ina lengo la kuboresha elimu na kutoa wahitimu bora wanaoweza kushindana katika soko la ajira.

Kwa mtazamo wangu, Profesa Ndalichako hakuna alichokifanya pamoja na nguvu kubwa ya kuvunja Bodi ya TCU, ndiyo! Hapa Watanzania wanachezewa mazingaombwe tu kwa kuwa sasa badala ya kuwadahili wasio na sifa kimya kimya wameamua kushusha ufaulu ili kuonekana hakuna sheria au kanuni iliyovunjwa, na kwamba hata wale waliodahiliwa baada ya viwango kushushwa wana sifa pia za kujiunga na vyuo vikuu.

Kama kweli Tanzania inataka kupata wahitimu bora wa vyuo vikuu, ni muhimu kuwa na msimamo katika viwango vya ufaulu. Wanafunzi wahimizwe kusoma kwa bidii ili waweze kufikia viwango vinavyohitajika na kwa atakayeshindwa afahamu wazi itambidi asome mpaka atimize vigezo.

TCU haikusema ni kwanini imeshusha viwango vya udahili kwa wahitimu wa stashahada, jambo ambalo pia linaacha maswali mengi. Kwa utaratibu kama huu, ni wazi kuwa tutaendelea kuwa na wahitimu wasio na ubora (half cooked).

Hivi sasa Tanzania pamoja na nchi nyingine wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, zipo katika utekelezaji wa mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na haki ya kuishi na kufanya kazi katika nchi yoyote mwanachama. Katika utaratibu huu, mkazi wa nchi yoyote anaweza kuajiriwa hapa Tanzania na suala hili limeshaanza kuzua mjadala kuwa wageni wanachukua ajira za wazawa. Kama elimu haitapewa uzito wa kutosha, ni wazi kuwa ajira zaidi zitaangukia kwa wageni.

Tafsiri yangu katika suala hili la TCU kushusha viwango vya udahili ni kuwa, Tume hii inaangalia zaidi wanafunzi kuwepo na kujaza madarasa bila kujali kama wana sifa au hapana na ni wazi kuwa inawezekana ufaulu ukawa unaendelea kushuka kila kukicha ili kuhakikisha madarasa yanapata wanafunzi.

Ili kufanikiwa, ni muhimu kuweka misingi thabiti ya elimu kuanzia ngazi za chini kabisa ili kuwaandaa wanafunzi vyema. Ni bora kuzalisha wahitimu wachache walio bora kuliko kuzalisha wengi ambao wote ni ‘mambumbu’.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles