- Ni baada ya ajali, waliofariki wafikia 75
- Serikali kujenga mnara wa kumbukumbu
WAANDISHI WETU-MOROGORO/DAR
MJI wa Morogoro umeendelea kuwa katika hali ya utulivu huku ukimya ukitawala katika eneo ilipotokea ajali ya lori la mafuta ambalo lilipuka moto na kusababisha vifo vya watu 75 hadi sasa.
MTANZANIA ilitembelea katika eneo la ajali Msamvu Mtaa wa Itigi, ambalo lipo jirani na Kituo Kikuu cha Mabasi Mkoa wa Morogoro ambapo baadhi ya watu wanaofanya shughuli zao ikiwamo biashara, wamesema kuwa upweke umetawala huku idadi kubwa ya vijana ambao walikuwa wakionekana katika eneo hilo kufariki dunia kwa ajali hiyo.
Dereva Bodaboda Kijiwe cha Maraha, Daimon Chibigasi alisema eneo ilipotokea ajali hiyo ndipo kijiwe chao cha kazi, lakini siku ya tukio wengi walichelewa kufika huku kundi kubwa la watu waliopoteza maisha walikuwa ni wapiga debe, pamoja na wapita njia.
Alisema wakati ajali hiyo inatokea yeye alikuwa upande wake wa pili wa barabara ambapo walishuhudia idadi kubwa la wapiga debe, wapita njia wakikimbilia kwenye eneo hilo la tukio ambapo wengine walikuwa wakipiga picha kwa kutumia simu zao.
“Mateja (watumia dawa za kulevya) ndio waliokuwa wengi na wapita njia, maana wengi hatuwaoni mtaani, ule wingi wao ambao tumeuzoea mtaani haupo na zile pilikapilika za kuitia abiria hapa kwenye tuta umepungua sana, kwa kweli hali imepooza tofauti na awali.
“Ofisi yetu imeungua, hapa ndio kijiwe chetu, sisi mafundi pikipiki na muuza mitumba ambaye alikuwa anatundika nguo zake kwenye miti hii iliyoungua, kwa sasa inabidi tupaki huku pembeni,” alisema Chibigasi
Naye Rajabu Idd maarufu Jaji, alisema ugumu wa maisha hususani kwa vijana ni sababu ya kufanya kitu chochote bila kuangalia madhara yake.
“Kinachosababisha ni ugumu wetu wa maisha, mtu kalala na njaa halafu asikie kuna sehemu kuna riziki, hawezi kuiacha eti kwa hofu inaweza kutokea hatari, muda ule mtu unafurahia kutuliza njaa uliyonayo,” alisema Idd.
Aidha, alisema mpaka sasa waendesha bodaboda wawili katika kijiwe chao ndio walipatwa na maafa hayo huku akieleza kwamba kundi kubwa la waliopoteza maisha ni wapiga debe.
“Wapiga debe wengi hatuna historia zao na wengi hawajulikani wanakoishi, lakini wamepungua sana, hata ukishusha abiria sasa hivi huwaoni, mwanzo walikuwa wengi mpaka wanagombania abiria, wengine walikuwa wanatafuta abiria kwa ajili ya gari za IT na magari binafsi,” alisema
MNARA KUJENGWA
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, ameuagiza uongozi wa Mkoa wa Morogoro kujenga mnara wa kumbukumbu katika eneo iliyozikwa miili ya watu 61 katika eneo la Kola ambapo hadi sasa waliopoteza maisha katika ajali hiyo wamefikia 75.
Hayo aliyasema jana mjini hapa katika eneo la mazishi ya miili ya watu 61 katika eneo la Kola mjini hapa, ambapo alisema kuwa ni vema ukajengwa mnara huo wa kumbukumbu na ambao pia aliagiza uzungushiwe uzio.
Pamoja na hali hiyo Majaliwa amewataka viongozi wizara ya afya kwa kushirikiana na serikali Mkoa wa Morogoro kuendelea kusimamia kazi hiyo hadi hali ya utulivu itakaporejea.
“Viongozi muendelee kutoa ushirikiana na familia ya majeruhi na wafia kwa kipindi chote ili kuhakikisha zoezi linakwisha pasipo sintofahamu kuhusu miili ya marehemu hawa,” alisema Majaliwa
MIILI 61 YAZIKWA
Kwa upande wake Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu), Jenista Mhagama, alisema kuwa hadi sasa tayari miili ya watu 61 imeshazikwa katika makaburi ya Kola na mingine tisa iko katika chumba cha kuhifadhia maiti katika hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Morogoro.
WALIOFARIKI WAFIKIA 75
Idadi ya vifo vya watu waliofariki dunia katika ajali hiyo imeongezeka na kufikia 75 baada ya majeruhi wengine wanne waliokuwa wakipatiwa matibabu katika Hospitali ya Taifa ya Muhibili (MNH) kufariki dunia jana.
Akizungumzia na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Ofisa Habari Mkuu wa Muhimbili, Aminiel Aligaesha, aliwataja waliofariki kuwa ni pamoja na Jackson Shao(25), Kulwa Dominic (28), Isamail Mwanga (28) na Muhidin Mtingwa (42).
Aligeisha alisema hadi sasa ni majeruhi 39 pekee wanaoendelea kupatiwa matibabu hospitalini kati ya 46, waliofikishwa katika hospitali baada ya wengine watatu kufariki dunia juzi.
“Mpaka sasa kuna vifo saba ambapo watatu walipoteza maisha jana (juzi) wakati wanasafirishwa na leo (jana) wameongezeka wanne, tumebakiwa na majeruhi 39 kati ya wale 46 walioletwa Muhimbili.
“Kuna majeruhi wengine hawana ndugu tunaomba kama una ndugu yako hapa ujitokeze na hawa waliofariki ndugu zao wajitokeze pia ili waweze kuchukua miili ya ndugu zao ambayo imehifadhiwa hapa hospitalini.
“Kama hospitali tunaendelea kufanya kila tunachoweza katika kuwahudumia majeruhi hawa, dawa tunazo na wataalamu wapo muda wote kuwahudumia,” alisema Aligaeshi.
Aligaesha aliwaomba wananchi kuendelea kujitokeza kuchangia damu ili kuwasaidia majeruhi hao kutokana na uhitaji mkubwa wa damu katika matibabu yao.
MBATIA ATOA NENO
Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia, ameishauri Serikali kushirikiana na hospitali binafsi ili kuhakikisha majeruhi hao wanapatiwa matibabu katika mazingira rafiki kutokana na hali waliyonayo.
Mbatia aliwaambia waandishi Dar es Salaam jana kuwa licha ya Serikali kuahidi kugharamia matibabu ya majeruhi hao, ni vema pia ikashirikiana na hospitali hizo ili kuwezesha kupatikana kwa wodi kubwa na zenye viyoyozi tofauti na sasa ambapo wamewekwa katika chumba kidogo kinachotumia feni za kawaida.
Mbatia alisema Serikali na wadau wengine hawapaswi kuangalia suala la gharama badala yake wafikirie mateso wanayoyapata majeruhi hao ambao baadhi yao wameungua kwa zaidi ya asilimia 95 ya miili yao.
“Nitoe rai kwa Serikali na hili liwapendeze Watanzania wengine pale Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, kile chumba walichowekwa kwa kweli ile wodi ni ndogo kuwaweka wote kwa pamoja. Lakini niliwasiliana na wataalamu mbalimbali wa tiba wa ndani na nje ya nchi, watu walioungua miili yao kwa asilimia 95 au zaidi wanahitaji kuwa kwenye hali ya joto stahiki.
“Wanatakiwa wawe kwanza kwenye eneo kubwa la kutosha na wawe kwenye viyoyozi waweze kutunzwa na kuhudumiwa vizuri, joto walilonalo pale linaendelea kuwatesa,”alisema Mbatia.
Mbatia alisema hospitali binafsi kama vile Regency, TMJ, Aga Khan, Bugando, KCMC na hospitali nyingine za aina hiyo nchini, zinaweza kuchukua japo wagonjwa wawali au watatu kila moja ili kuipunguzia mzigo Muhimbili na kwamba hatua hiyo itawezesha baadhi ya watu wenye uwezo kujitokeza kuwalipia gaharama za matibabu baadhi ya majeruhi.
HABARI HII IMEANDALIWA NA ASHURA KAZINJA, RAMADHAN LIBENANGA (MORO), AVELINE KITOMARY, LEONARD MANG’OHA NA NEEMA SIGALIYE (Tudarco)