27.5 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Ukicha kutajwa hutotenda jambo

Na Barnabas Maro

“UKIOGOPA kusemwa na watu ufanyapo jambo hulifanyi asilani. Methali hii hutumiwa kumhimiza mtu anayedhamiria kulifanya jambo fulani kisha akawa anaogopa watakavyosema watu.

Bangi ni mmea ambao majani yake, mbegu zake au hata mizizi yake ikitafunwa au kuvutwa kama sigara hulevya na aghalabu hupumbaza akili. Ni ulevi unaotokana na majani ya m-bangi yaliyokaushwa au kusokotwa.

Tanzania, kama zilivyo nchi nyingi duniani, matumizi ya bangi ni marufuku. Ndiyo maana askari wa Jeshi la Polisi wamekuwa wakipita maeneo mbalimbali nchini kung’oa mimea hiyo na wahusika wanapokamatwa hufunguliwa mashitaka ya kulima na kupanda mmea huo haramu uliopigwa marufuku na serikali.

Mbunge Joseph Musukuma (CCM) wa Geita Vijijini, aliishauri serikali iruhusu matumizi ya bangi kwa madai kuwa haina madhara yoyote kwa watumiaji! Alitoa rai hiyo wakati wa mjadala wa mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2019/20 uliokuwa ukiendelea bungeni.

‘Maendeleo’ ni hali ya kupata ustawi yaani hali ya neema na faraja. ‘Maendelezo,’ pia ‘mwendelezo,’ ni namna au utaratibu wa kustawisha hali, vitu au watu, kusonga mbele kwa mawazo,  uchumi au mahali; upigaji hatua.

Nilimshanga m-bunge kusema bungeni kuwa bangi haina madhara yoyote wakati wenzake wakijadili Mpango wa Maendeleo ya Taifa! Uuzaji na uvutaji bangi ndio mchango wa m-bunge huyo wa kuleta maendeleo? Ndivyo alivyotumwa na wapiga kura wake?

Eti kwa kuwa baadhi ya nchi kama Afrika Kusini, Lesotho na Zambia zimehalalisha bangi na watu hununua kwa foleni hata kudhani “wamepanga foleni ya kumchagua rais” basi na Tanzania ifuate mkumbo! Huo ni upotoshaji na upuuzi. Eti yeye anaipigia debe bangi lakini hatumii. Awezaje kukisifia kitu asichojua uzuri na ubaya wake?

Pia aliitaka serikali iache watu wanywe pombe usiku kucha mpaka asubuhi kwani serikali itapata fedha nyingi kupitia kodi badala ya baa kufungwa saa tano usiku! Eti watu waachwe wakeshe wakinywa pombe! “Kwani kuna shida gani?” aliuliza m-bunge huyo.

Naam, shida ipo, tena kubwa. Watafanya kazi wakati gani wakiwa wanakunywa kucha ilhali wanatakiwa kufanya kazi zao au za kuajiriwa kuanzia asubuhi mpaka jioni?

Sasa nazungumzia suala la Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paulo Makonda alipowataka wakazi wa Dar es Salaam kuwataja watu wanaojihusisha na vitendo vya ushoga (uhusiano wa kirafiki wa wanawake kwa wanawake; hali ya wanaume kufanyana mapenzi wao kwa wao; usenge, uhanithi). Pia aliwataka wenye simu za ngono kwenye simu zao wazifute.

Yawezekana Makonda amefanya makosa mengi tangu alipoteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam lakini kwa nini alaumiwe kwa kupinga vitendo vya ushoga? Jamani mnyonge mnyongeni haki yake mpeni. Hakuna anayekuwa mbaya au mzuri kwa kila jambo.

Wakati watu wakiwa na mawazo tofauti kuhusu suala la ushoga, viongozi wa serikali nao wanaonekana kutofautiana wao kwa wao!

Kwa mfano, Wizara ya Mambo ya Nje ilitoa taarifa kwa vyombo vya habari kumkana Makonda kwamba kampeni ya kuwasaka watu wanaojihusisha na vitendo vya ushoga inayoratibiwa naye ni mawazo yake (Makonda) na si msimamo wa serikali. Kujiweka kando na kampeni ya Makonda ina maana serikali inaafiki ushoga?

Akijibu swali la mbunge Khatib Said Haji wa CUF kuwa suala la ushoga limekuwa na kauli zinazotofautina baina ya Wizara ya Mambo ya Ndani na Wizara ya Mambo ya Nnje, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola alisema  kuna sheria inayokataza vitendo vya ushoga, kwa hiyo msimamo wa serikali haujabadilika kuhusu mambo hayo na kama kuna msimamo tofauti, basi ni upotoshwaji wa vyombo vya habari! Ama kweli mnyonge kupata haki ni mwenye nguvu kupenda.

Waziri Lugola akasisitiza kuwa “Serikali hii chini ya Rais John Magufuli haitaruhusu mtu kubadili matumizi ya kiungo cha kutolea haja kwa matumizi mengine. Kiungo hicho kina kazi maalum na si kwa ajili ya mambo ya ushoga. Hatutakubali hata siku moja.

“Tanzania ni hekalu la Roho Mtakatifu, kwa hiyo hatukubali hekalu ya Roho Mtakatifu liingiliwe na vitendo vya ushoga,” alisema Lugola.

Si kila afanyacho Makonda ni kibaya, hasha (sivyo kabisa)! Yapo mazuri aliyofanya ila kinachomponza ni papara na kuingilia sehemu zisizomhusu.

Yasemwa “Mwenye pupa hadiriki kula tamu.” Pupa ni nia ya kutaka kufanya jambo haraka. Maana yake anayekula chakula kwa kupapiapapia hawezi kufaidi utamu wake. Methali hii huwanasihi watu wasiwe na tabia ya kufanya mambo kwa papara na pupa kwa kuwa aghalabu matokeo yake huwa mabaya.

Kuna wakati Makonda aliwaamuru wafanya biashara ndogo ndogo, maarufu kwa jina la ‘wamachinga’ kutofanya shughuli zao kando ya barabara na maeneo ya waenda kwa miguu. Hata hivyo wamachinga wakapewa ‘jeuri’ na mkubwa kuwa wasihame mpaka watakapooneshwa eneo lingine la kufanyia biashara zao.

Kauli ya mkubwa ikawapa nguvu wamachinga kuenea kila eneo lenye nafasi bila kujali hata kama ni mbele ya maduka ya wafanyabiashara wanaolipa kodi za serikali! Sasa wengine wamejazana mpaka barabarani na kuwa kero kwa magari na waenda kwa miguu. Hata pale Gerezani jijini Dar es Salaam, pamevamiwa na wamachinga mpaka maeneo wanayopita abiria!

Hawa jamaa hawakufanya mkutano kuwa wavamie pamoja eneo lile na mengine, bali alianza mmoja akifuatiwa na wengine mpaka wakajazana kama walivyo sasa. Hata vibanda vilivyojengwa kuwasitiri abiria wa daladala kwa jua na mvua, sasa vimevamiwa na wamachinga wanaoweka meza za kufanyia biashara zao.

Tatizo ni kwamba serikali ya mkoa wa Dar es Salaam haikuwa na utaratibu wa kuwa na maeneo maalumu ya kuwaweka wamachinga ambao leo wangekuwa wanalipa kodi kama wafanyabiashara wengine. Kwa hiyo serikali ya mkoa inapoteza fedha nyingi kwa uzembe huo. Ni kama jiji la Dar es Salaam halina serikali. Ni vurugu tupu!

Nawakumbuka wahenga waliosema: “Kupanda mchongoma kushuka ndio ngoma.” Maana yake kuupanda mchongoma ambao una miiba ni rahisi kuliko kushuka. Hutumiwa kumnasihi mtu asijiingize katika hali ambayo itakuwa vigumu kutoka. Yafaa kuyachunguza mambo kabla ya kuyaingilia tusije kujizulia balaa kubwa.

Kuna wakati Makonda aliamuru watu masikini, maarufu kwa jina la ‘ombaomba’ wanaojazana barabarani na watoto wao kuomba hela, warejee walikotoka. Ilikuwa ‘nguvu ya soda!’

Ibara ya 17(1) ya Katiba imeweka wazi kuwa “Kila raia wa Jamhuri ya Muungano anayo haki ya kwenda kokote katika Jamhuri ya Muungano na kuishi katika sehemu yoyote, kutoka nnje ya nchi na kuingia, na pia haki ya kutoshurutishwa kuhama au kufukuzwa kutoka katika Jamhuri ya Muungano.”

Je, Makonda hakuwa ameisoma Katiba au aliisoma juujuu tu bila kuielewa na kuizingatia?

Ingekuwa busara kama Bunge lingepitisha sheria kutaka kila mkoa uwe na makazi maalumu ya watu masikini. Kabla ya kupelekwa huko, ufanywe utafiti kujua wanakotoka na kama wana familia zao. Kama ndivyo, warudishwe kwa familia zao na kama wakionekana tena mitaani, familia zao ziwajibishwe.

Kinachoshangaza ni kuwaona wanawake wasiokuwa na hitilafu yoyote ya miili yao wakiandamana na watoto wao barabarani kuomba hela. Kwa nini wanakubali kupewa ujauzito na wanaume wasioweza kuwatunza? Yapo madai kuwa hughilibiwa na kuchukuliwa usiku na wanaume khabithi (watu wasiojali utu wa wengine) ili kukidhi (kutosheleza makusudio yao) kisha kuwatelekeza!

Wahenga hawakukosea waliposema: “Fedha fedheha” kwani pesa huweza kuleta mambo ya aibu baina ya wanadamu. Methali hii hutumiwa kutuonya kuhusu maovu yanayoweza kusababishwa na pesa.

“Fedha ilivunja nguu milima ikalala.”

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

  1. Hili la Machinga lingeweza kutatuliwa kirahiiiisi ! Kila alipo Machinga aandikishwe. Kila mmoja ajulikane anaishi wapi na anafanya biashara gani na wapi anakopata mali anayouza. Jirani na kila stendi ya daladala na kituo cha mabasi patengwe eneo kwa ajili ya Machinga. Wasiruhusiwe kupanga bidhaa kila mahali.

    Machinga waliojiandikisha wasambazwe kwenye hayo maeneo karibu na vituo vya mabasi na daladala. Yatafutwe pia maeneo mengine ambayo watu wanapita kwa wingi yatengwe maeneo hapo. Kila Machinga awe amepata eneo lake na liandikishwe. Alipe kodi kwa kibanda chake. Kama ambavyo mabasi yanavyolipa kila yakiingia stendi basi na Machinga alipie kibanda chake siku kwa siku.

    Kama Machinga anatokea mbali na anapopanga bidhaa zake (kwa mfano kama anapanga stendi ya Ubungo lakini anaishi Tegeta), basi mpango wa kuwapa Machinga maeneo uzingatie hilo. Wale wa eneo fulani wapangiwe eneo la vibanda vyao karibu na makazi yao. Mahali wanapopata bidhaa pakijulikana, anayewapa (kama ni mfanya biashara mkubwa) alipishwe kodi kwa mali anazowapa Machinga. Machinga atakiwe kuweka eneo lake safi wakati wote.

    Mpango huu ukifanyika kwa nchi nzima, miji yetu itakuwa safi, serikali itakusanya kodi nyingi zaidi na Machinga watapata biashara za kufanya waweze kujikimu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles