26.4 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

Ukawa yajizatiti kuelekea Ikulu 2015

lipumbaNA GRACE SHITUNDU, DAR ES SALAAM
CHAMA cha Wananchi (CUF) kimedhamiria kudumisha ushirikiano wa vyama vinavyounda UKAWA kuhakikisha wanaking’oa madarakani Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kupata serikali itakayoondoa matabaka, uonevu na udhalilishaji pamoja na kupunguza umasikini kwa wananchi.
Maazimo hayo yalifikiwa katika kikao cha Baraza Kuu la Uongozi Taifa, CUF, kilichofanyika kwa siku mbili jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa chama.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mwenyekiti wa CUF Taifa, Profesa Ibrahim Lipumba, alisema kikao hicho kilijadili mambo mbalimbali yanayohusu chama na Taifa kwa ujumla, likiwemo la migogoro na migomo ya mara kwa mara kati ya serikali na wananchi, uporaji wa ardhi, hali ya uchumi, maafa, ajali na mauaji ya albino na pia suala la uandikishaji katika daftari la wapiga kura, uchaguzi mkuu na kura ya maoni.
Alisema mambo hayo yote yanashindwa kutatuliwa kutokana na serikali iliyopo madarakani kuwa na utendaji mbovu katika sekta mbalimbali.
“Baraza limewahimiza UKAWA kuendeleza juhudi na lengo la kuing’oa CCM madarakani na kujenga taifa litaloongozwa na misingi ya uadilifu, uwajibikaji na uwazi, ambapo kutakuwa na haki sawa kwa wote,” alisema Lipumba.
Alisema pia Watanzania waunge mkono juhudi hizo ili kukataa uonevu, unyanyasaji unaotendwa na baadhi ya watu wenye uwezo kujinufaisha wao kiuchumi na kisiasa.
“Wananchi wana madaraka ya kujiamulia wenyewe masuala yote ya maendeleo yao ya kisiasa, kiuchumi, kijamii na kiutamaduni, hivyo kuondokana na mtindo wa kupangiwa na wajanja wachache wenye ukiritimba wa wazi na uroho wa madaraka au kujipatia mali zisizo halali, ili kuondoa mambo yote ya rushwa, ufisadi, ubadhirifu na uonevu,” alisema Lipumba.
Pamoja na azma hiyo, chama hicho kimeitaka serikali kuhakikisha inaondosha mianya ya migogoro na migomo, pia kufanya utafiti wa kina sababu ya ajali zinazotokea mara kwa mara sambamba na kukarabati miundombinu.
Aidha Serikali ihakikishe wananchi wote wanaandikishwa katika daftari la wapiga kura, kutimiza makubaliano yaliyofikiwa na vyama vya siasa na Rais juu ya marekebisho ya baadhi ya vifungu vya Katiba ya sasa ili vitumike katika uchaguzi mkuu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles