27.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

Ukawa watishia kujitoa ALAT

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

MAMEYA na Wenyeviti wanaounda Umoja wa Katiba ya wananchi (Ukawa) ambao walihudhuria mkutano mkuu maalum wa uchaguzi wa Umoja wa Serikali za mitaa wametishia kujitoa katika umoja huo kwa sababu ya kukiukwa   taratibu mbalimbali.

Msimamo huo waliutoa   Dodoma jana saa chache baada ya kususia mkutano huo wakipinga majina ya wagombea wao kukatwa bila kuelezwa sababu za msingi.

Katika taarifa yao   jana, walitoa orodha ndefu ya kukiukwa   taratibu hizo ikiwa ni pamoja na hatua ya ALAT kumruhusu waliyemuita ‘meya batili’ wa jiji la Tanga kuhudhuria na kugombea nafasi ya makamu mwenyekiti wa Jumuiya hiyo.

Mameya hao na wenyeviti wa Ukawa walisema; “Machapisho ya ALAT tuliyopewa ukumbini yalikuwa na picha za wajumbe waliovaa sare za Chama Cha Mapinduzi (CCM)  wakati ALAT ni chombo kisichofungamana na chama chochote cha siasa. Mfano   Meya wa Manispaa ya Dodoma anaonekana kwenye kabrasha la ratiba akiwa amevalia sare za CCM.

“Katibu mkuu kutokuchapisha orodha ya wagombea na kuisambaza kwa wajumbe wa mkutano huo kwa mujibu wa kifungu cha 30 (6) cha kanuni za kudumu za mkutano na uchaguzi wa viongozi wa jumuiya za serikali za Mitaa za mwaka 2009”.

Mwenyekiti ALAT apatikana

Wakati huohuo, ALAT jana ilipata mwenyekiti mpya licha ya wajumbe kutoka Ukawa, wakisusia uchaguzi huo kwa kutoka nje ya ukumbi.

Wajumbe walimchagua Meya wa Manispaa ya Shinyanga, Gulam Mukadam  kuwa mwenyekiti wa jumuiya hiyo kwa kura 179 kati ya kura 281 zilizopigwa.

Mgombea mwingine katika nafasi hiyo  alikuwa ni Murshid Ngeze aliyepata kura 97 huku kura tano zikiharibika.

Huo ni mkutano wa kwanza wa jumuiya hiyo katika uongozi wa Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dk. John Magufuli.

Awali, Mwanasheria wa ALAT, Cleofasi Manyangu, alisema nafasi zilizokuwa zikigombewa ni mwenyekiti, makamu mwenyekiti na nafasi za wajumbe wa kamati ya utendaji.

“Wakati wa mchakato wa uchaguzi huu waliochukua na kurejesha fomu za kugombea uenyekiti wa ALAT   ni Gulam Mukadam, Murshid Ngeze ambaye ni Meya wa Bukoba Vijijini, Chifu Kalumuna ambaye ni Meya wa Bukoba Mjini na Isaya Mwita ambaye ni Meya wa Jiji la Dar es Salaam.

“Waliokidhi vigezo kwa mujibu wa Katiba ya ALAT ni watia nia wawili ambao ni Mukadam na Ngeze na waliosalia  hawakukidhi vigezo vya kuwa wagombea.

“Vigezo hivyo vilikuwa ni kurejesha fomu katika muda usiozidi saa 6:00 ya siku moja kabla ya uchaguzi na pia wagombea hao hawakupata wadhamini 10 kama taratibu zinavyoelekeza,” alisema Manyangu.

Wakati Manyangu akisema hayo, Mwenyekiti wa muda wa mkutano huo ambaye pia ni Meya wa Dodoma, Jafari Mwanyemba, alitangaza rasmi kwamba watakaogombea katika uchaguzi huo ni Mukadam na Ngeze jambo lililosababisha wajumbe wa Ukawa kususia shughuli zote za uchaguzi huo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles