NA KULWA MZEE-DODOMA
MBUNGE wa Malindi, Ally Saleh Ally (CUF), amewasilisha barua ya kutoridhishwa na hukumu iliyotolewa dhidi ya Mbunge wa Kawe, Halima Mdee na Mbunge wa Bunda, Esther Bulaya (wote Chadema) ya kufungiwa kuhudhuria vikao vya Bunge mwaka mzima.
Saleh ambaye ni Mnadhimu Msaidizi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, alisema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari akiwa na wabunge wengine wa Ukawa.
Alibainisha kwamba barua hiyo ameiwasilisha kwa Katibu wa Bunge na Spika.
“Kutokana na sababu za kutoridhishwa na hukumu hiyo, tunaomba Kamati ya Kanuni iitishwe ili kutoa uamuzi juu ya upungufu ili haki itendeke kwa ajili ya mustakabali mwema wa uendeshaji shughuli za Bunge letu,” alisema.
Alitaja sababu za kutoridhishwa kuwa ni watuhumiwa katika shauri lililowasilishwa katika hoja ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge hawakupewa haki ya kusikilizwa na hakukuwa na dharura yoyote ya kuendesha shauri hilo wakati wa mwisho wa wiki, huku ikifahamika kwamba bado kuna muda wa kutosha kwa kuwa Mkutano wa Bunge la Bajeti unaendelea hadi mwishoni mwa Juni.
“Ilikuwa inafahamika kwamba mashahidi hao walikuwa wamepatwa na msiba wa kiongozi wao wa chama na kwa vyovyote vile wangesafiri kuelekea msibani Moshi.
“Uharaka huu ulisababisha Esther Amos Bulaya kuhukumiwa kwa kosa la kuhamasisha wabunge wa upinzani kutoka nje, kosa ambalo si lake kwa kuwa alikuwa akitekeleza agizo la Mnadhimu Msaidizi wa Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni,” alisema.
Alisema sababu nyingine ni hati ya wito haikuwasilishwa kwao siku ya Juni 2, mwaka huu kama ilivyoagizwa, huku ikifahamika kuwa wakati wa jioni siku hiyo mashahidi hao walihudhuria kikao cha Bunge jambo ambalo linaonyesha kwamba hakukuwa na nia njema.
“Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka inafanya kazi zake kwa faragha, lakini mara tu baada ya Mwenyekiti wa Kamati kuanza kusoma taarifa yake, ndani ya dakika kumi iligawanywa hoja ya pendekezo la mabadiliko ya maazimio ya kamati, hata kabla Mwenyekiti hajamaliza kusoma,” alisema.
Juzi, Mdee na Bulaya walisimamishwa kuhudhuria vikao vyote vya mkutano wa saba, nane na tisa wa Bunge kwa kudharau mamlaka ya Spika wa Bunge.