KHAMIS MKOTYA NA RAMADHANA HASSAN, DODOMA
BUNGE limechafuka. Ndivyo unavyoweza kusema baada ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kutangaza kutokuwa na imani na Naibu Spika, Dk. Ackson Tulia kwa kile walichoeleza anayumbisha Bunge katika kutekeleza majukumu yake.
Kambi hiyo pia imeweka msimamo wake kwamba kuanzia sasa wabunge wa kambi hiyo watalazimika kutoka nje ya Ukumbi wa Bunge katika vikao vyote vitakavyokuwa vikiongozwa na Dk. Tulia.
Maazimio hayo yamekuja baada ya kuibuka mzozo mwingine katika kikao cha jana jioni kuhusu mjadala wa kutaka sakata la wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), ambapo wabunge walitaka lijadiliwe.
Baada ya Bunge kurejea jioni hali iliendelea kuwa tete, hasa baada ya kambi ya upinzani kupinga uamuzi wa Naibu Spika, ambaye alimwita Naibu Waziri wa Maji, Isack Kamwelwe kuendelea na majumuisho ya hoja ya maji.
“Tuliahirisha Bunge asubuhi kutokana na hoja ya Udom, sasa simwoni Waziri wa Elimu hapa na kwa kuwa simwoni tunaendelea na ratiba, hivyo badala ya kuendelea kujadili hoja ya maji muda hakuna tunakwenda moja kwa moja kwenye majumuisho, waziri akija nitampa nafasi,” alisema Dk. Tulia.
Wakati naibu waziri huyo akiendelea na majumuisho, baadhi ya wabunge wa upinzani walisimama kuomba mwongozo wakipinga majumuisho ya Wizara ya Maji, wakati kulikuwa na hoja ya dharura.
Baada ya vuta ni kuvute, Naibu Spika alimtoa nje Mbunge wa Kibamba, John Mnyika (Chadema), ambaye alionekana kukaidi agizo lake la kumtaka akae chini.
Baada ya Mnyika kutolewa nje, wabunge wa kambi hiyo waliendelea kugonga meza na kumfanya Naibu Waziri wa Maji ashindwe kuchangia, hatua iliyomlazimu Naibu Spika kuagiza wabunge wote wa kambi ya upinzani watolewe nje.
Wakati wakitolewa nje, kiongozi huyo wa Bunge aliagiza wabunge wawili wa kambi hiyo, Esther Bulaya (Bunda) na Jushua Nassari (Arumeru Mashariki) – wote kutoka Chadema, wapelekwe katika Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kutokana na vurugu hizo.
Baada ya wabunge hao kutolewa, kambi hiyo ilikutana katika Ukumbi wa Msekwa ambako pamoja na mambo mengine ilitangaza maazimio hayo mawili.
Akizungumza na waandishi wa habari, Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, alishangazwa na uamuzi uliofanywa na Naibu Spika baada ya Bunge kurejea jioni.
“Baada ya Bunge kuahirishwa leo (jana) asubuhi, Kamati ya Uongozi ilikutana, kama kamati tulikubaliana mambo mawili. Mosi, tutakaporejea jioni Naibu Spika aruhusu mjadala wa Udom. Pili, Waziri wa Elimu atoe kauli ya Serikali ya kutangaza kuwarejesha shuleni wanafunzi wote walioondolewa shuleni.
“Lakini ninyi ni mashahidi, Naibu Spika amefanya tofauti na maelekezo ya Kamati ya Uongozi. Tatizo tunaloliona katika Bunge hili la 11 ni Naibu Spika. Amekuwa akiendesha vikao vya Bunge kinyume na matakwa ya kanuni. Amefanya makosa mawili, la kwanza ameacha kuendelea na hoja iliyokuwa mezani na akaamua kufunga mjadala wa hoja ya maji.
“Katika order paper kuna taarifa ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, wameona mambo mengine yote hayana maana wakimbilie kwenye ripoti ya kamati hiyo ambayo inalenga kuwaadhibu wabunge wa upinzani.
“Hatutaki kutokuheshimu kiti cha Spika, lakini pia tunataka Spika aheshimu mawazo ya wabunge, aheshimu taratibu za kuliongoza Bunge, tunapoona kanuni zinatungwa za kuzima masilahi ya walio wengi hatutaziheshimu hizo kanuni na kama ni kutufukuza bungeni wanaweza kutufukuza na wala hatutafanya utii usiokuwa na dhamira ya kweli.
“Tatizo kubwa la Bunge la 11 la msingi kabisa ni Naibu Spika. Kwa sababu tunaona mara kwa mara Bunge la linavurugika, mwenendo wa Bunge unavurugika, maamuzi ya Bunge yanapuuzwa. Ni kwa sababu ya mtu anayeitwa Ackson Tulia (Naibu Spika). Mimi pendekezo langu kwenu wabunge leo, la kwanza kabisa tujadili kutokuwa na imani na Naibu Spika,” alisema Mbowe.
Pendekezo jingine lililoungwa mkono na kupigiwa makofi mengi na wabunge wa kambi hiyo, ni pale Mbowe alipotangaza kuwa watatoka nje katika vikao vyote vitakavyokuwa vikiongozwa na Naibu Spika.
Awali baada ya wabunge hao kutolewa nje, Mbunge wa Gairo, Ahmed Shabiby (CCM), alisimama na kuomba mwongozo akitaka wabunge waendelee kuchangia hoja ya maji, kwani ni wabunge 12 tu waliochangia bajeti hiyo jambo ambalo alisema likiendelea hivyo wizara hiyo itakuwa haikutendewa haki licha ya unyeti wake.
WANAFUNZI UDOM
Katika hatua nyingine, kuliibuka tafrani bungeni na kusababisha Bunge kuahirishwa kabla ya muda kufuatia hatua ya Serikali kuwaondoa wanafunzi 7,802 wa kozi maalumu ya stashahada (diploma) ya ualimu wa sayansi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).
Hatua hiyo ilijitokeza bungeni jana asubuhi, baada ya Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako kutoa ufafanuzi kuhusu uamuzi huo wa Serikali.
Wabunge wengi walionekana kutokubaliana na uamuzi huo, hatua iliyowalazimu kusimama na kuomba mwongozo, wakitaka Bunge lisitishe mjadala uliokuwapo katika ratiba na badala yake wajadili hoja ya dharura ya wanafunzi hao kufukuzwa.
Hata hivyo, hasira za wabunge zilichochewa zaidi na uamuzi wa Dk. Tulia, ambaye alikataa kuruhusu mjadala huo, kwa madai kuwa maelezo ya waziri yalikuwa yamejitosheleza.
Akitoa kauli hiyo, Waziri Ndalichako alisema uamuzi wa kuwarejesha nyumbani wanafunzi hao umefikiwa ili kutoa fursa kwa Serikali kuendelea kufanya mazungumzo na walimu waliogoma kufundisha kwa kipindi cha mwezi mmoja sasa.
“Kutokana na mgogoro huu walimu ndio waliogoma kuingia madarasani kufundisha, wanachogombea ni madai ambapo kwa mujibu wa mkaguzi wa ndani wa chuo hicho, madai hayo yanaonekana hayana usahihi, kuhusu masuala ya fedha Serikali haiwezi kumwingilia mkaguzi wa ndani.
“Kwa sababu walimu wameonekana kutokuwa tayari kuendelea kufundisha na wanafunzi wameshakaa muda mrefu bila kusoma, Serikali imeona ni busara wanafunzi waende nyumbani wakati suala hili linaendelea kutafutiwa ufumbuzi,” alisema Profesa Ndalichako katika taarifa yake fupi.
Baada ya kauli hiyo, wabunge wengi bila kujali itikadi zao za vyama walisimama na kuomba mwongozo. Alipopewa nafasi Mbunge wa Chemba, Juma Nkamia (CCM), alitaka kujua iwapo ni sahihi Serikali kuwaondoa chuoni wanafunzi ambao hawana makosa, huku akilitaka Bunge kuahirisha mjadala uliokuwapo na badala yake lijadili hoja ya wanafunzi hao kwa dharura.
Kutokana na hoja hiyo, wabunge wengi wakiwamo wa upinzani na CCM walisimama kuunga mkono.
“Watoto hawa hawana makosa, wanafunzi wengi hawa wanatoka maeneo mbalimbali nchini, waliogoma ni walimu, lakini walioadhibiwa ni wanafunzi, naomba mwongozo hivi Serikali haikuona umuhimu wa kumaliza tatizo la walimu ambao ni wachache badala ya kuwaadhibu wanafunzi 7,802” alisema.
Hata hivyo Naibu Spika, alisema kuwa hawezi kuruhusu mjadala huo kwa kuwa kanuni aliyotumia Nkamia haikuwa sahihi juu ya jambo alilokuwa anataka.
Naye Mbunge wa Arumeru Mashariki, Nassari (Chadema), aliomba mjadala unaoendelea kwenye order paper uahirishwe ili kutoa nafasi kujadili tatizo la wanafunzi wa Udom, aliosema wamelazimishwa kuondoka kwa muda usiozidi saa 24 kwa mgogoro uliosababishwa kwa kutokuelewana baina ya Serikali na walimu, lakini pia Naibu Spika alikataa kuruhusu akisema kuwa hakuridhika na udharura halisi wa jambo linalopiganiwa na wabunge.
Msimamo huo wa Dk. Tulia ulizidi kuwachefua wabunge ambao walikuwa wakishinikiza mjadala huo huku wakiwa wamesimama, hali iliyomfanya atumie nguvu za ziada kuwatuliza na kuwasihi wakae chini. Alipoona hali inazidi kubadilika ukumbini, aliwaagiza askari wa Bunge kuwatoa nje wabunge wote waliokuwa wamesimama.
Mbunge wa Arumeru Mashariki, Nassari alitolewa bungeni kwa nguvu hadi nje ya geti, ingawa baadaye alirudi katika viwanja vya Bunge akiungana na wenzake kupinga jambo hilo.
Wakati askari hao wakiwafuata wabunge hao, Naibu Spika aliamua kuahirisha kikao hadi saa kumi jioni, kwani wabunge walikuwa wamechachamaa wakipinga hatua ya kiti kuzuia mjadala.
WABUNGE
Baadhi ya wabunge waliozungumza na MTANZANIA katika viwanja vya Bunge waliilaumu Serikali kutokana na kitendo chake cha kuwaadhibu wanafunzi huku ikijua hawana makosa.
Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe (CCM), alisema. “Mimi naona kiti cha Bunge leo kimefanya ‘mismanagement’ ya nidhamu, busara ilikuwa ndogo. Naibu Spika alikuwa na mamlaka ya kufanya mambo mawili, aidha kuruhusu mjadala au kuagiza Kamati ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii itoke ikakutane na waziri na uongozi wa chuo cha UDOM saa kumi iletwe ripoti ili kujua hatima ya hawa wanafunzi.”
Mbunge wa Mafinga Mjini, Cosato Chumi (CCM), alisikitishwa na uamuzi huo na kusema kuwa Serikali haikutumia busara katika kushughulikia mgogoro huo.
KAULI YA UDOM
Nao uongozi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), umesema zaidi ya wanafunzi 7,000 wa Diploma ya Ualimu wa Sayansi waliosimamishwa kwa muda usiojulikana katika chuo hicho wiki iliyopita wanapaswa kuanzia kusoma ngazi ya cheti.
Akizungumza na MTANZANIA, Makamu Mkuu wa Udom, Profesa Idrisa Kikula alisema wanafunzi hao waliosimamishwa wanatakiwa kuanza kusoma ngazi ya cheti.
Alisema kwa mujibu wa utaratibu ambao upo, wanafunzi wa kidato cha nne hawatakiwi kuanza na diploma kabla ya ngazi ya cheti, hivyo wametoa ushauri kwa Serikali ifanye utaratibu wa kuwarudisha katika ngazi ya cheti.
“Wanafunzi kuondoka sio matakwa ya chuo, ni matakwa ya Serikali, na sisi tumepewa maagizo tu, suala hilo halikuanzia kwetu,’’ alisema Profesa Kikula.
Apoulizwa kilichosababisha walimu hao kugoma, Profesa Kikula alisema alikuwa nje ya ofisi hivyo anasubiri kupata taarifa kutoka kwa waliokuwepo.
Lakini kwa mujibu wa chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya chuo hicho, sababu ya walimu hao kugoma ni kukataa kufundisha wanafunzi wa diploma bila kuongezwa fedha kwa kuwa mikataba yao inaonyesha wanatakiwa wawafundishe wanafunzi wa shahada.
Kozi ya Diploma ya Ualimu wa Sayansi chuoni hapo ilianzishwa maalumu kwa agizo la Rais wa awamu ya nne Dk. Jakaya Kikwete lengo likiwa ni kuziba pengo la walimu wa sayansi na sifa za kujiunga ilikuwa ni kuhitimu kidato cha nne na kufaulu vizuri masomo ya sayansi.