30.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Ukawa wampa masharti Kikwete

Wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba wanaunda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA).
Wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba wanaunda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA).

NA SHABANI MATUTU, DAR ES SALAAM

UMOJA wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), umetoa masharti manne kwa Rais Jakaya Kikwete, ikiwamo kumtaka asitishe shughuli za Bunge Maalumu la Katiba.

Mbali na hatua hiyo, pia wamemtaka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kufanya ukaguzi maalumu juu ya matumizi ya fedha za Bunge hilo, kuanzia Bunge la Bajeti lililopita wakidai wamebaini kuwapo ufisadi na kukosekana maelezo sahihi.

Tamko hilo lililotolewa jana na wenyeviti wa vyama vya NCCR-Mageuzi, CUF na Chadema, vinavyounda umoja huo.

Katika tamko hilo lililosomwa na Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, Ukawa wamemtaka Rais Kikwete asitishe Bunge hilo ili wajumbe wake wasiendelee kufuja fedha za Watanzania.

Hata hivyo, tamko la Ukawa halikumpa Kikwete siku ya mwisho ya kutekeleza agizo lao.

Mbatia alisema iwapo Kikwete atashindwa kutumia mamlaka yake kusitisha vikao vya Bunge hilo, watafanya maandamano makubwa pamoja na mikutano ya hadhara nchi nzima, itakayohamasisha wananchi kupinga mchakato mzima wa Katiba.

“Bunge Maalumu la Katiba limeendelea kufanya vikao vyake mjini Dodoma kuanzia Agosti 5, mwaka huu kinyume kabisa na matarajio ya Watanzania, ambao kupitia fursa mbalimbali wamepaza sauti zao kusisitiza kuwapo kwa maridhiano na muafaka wa kitaifa utangulizwe mbele badala ya maslahi ya watawala,” alisema Mbatia.

Alisema wamefuatilia kwa karibu Bunge hilo linavyoendeshwa, na kushuhudia namna ambavyo mchakato wa Katiba unavyoharibiwa kwa kutumia rasilimali za taifa kwa vitu visivyokuwa na maslahi na taifa.

“Matokeo ya hayo yote ni kukosekana kwa uongozi wa kisiasa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kinachoongoza Serikali, kwani kuna ombwe la uongozi wa kisiasa katika jambo hili.

“Inavyoonekana jambo lenyewe linajiendea bila mwongozo wa watu walioko madarakani, waliokuwa wakitegemewa kutumia mamlaka yao ya dhamana ya uongozi ili taifa lipite salama katika wakati huu mgumu na tupate Katiba mpya na bora,” alisema Mbatia.

Kwa mujibu wa Mbatia, moja ya viashiria alivyodai vinaweka ombwe, ni kauli kinzani zinazotolewa na viongozi wa Serikali.

“Wakati Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akizungumza kama anayehitaji mazungumzo zaidi kwa kutaka suala la muundo wa Serikali kupigiwa kura kabla, lakini mwenyekiti wa Bunge hilo anaendelea kuliongoza kama vile mchakato wa Katiba ni mali binafsi ya CCM na wale walioko madarakani,” alisema Mbatia.

Alidai kuwa CCM imelewa madaraka na viongozi wake wakiwa hawajali umuhimu na nafasi ya mamlaka ya wananchi katika kuamua mustakabali wa taifa lao.

“Tunapenda kusema wazi kushangazwa na kitendo cha Serikali ya CCM kuendelea na mchakato wa Katiba mpya, tena kwa mtindo wa kupuuza maoni ya wananchi yaliyomo kwenye rasimu ya pili ya Katiba mpya, kama yalivyopendekezwa na Tume ya Jaji Warioba,” alisema.

Alisema uamuzi uliochukuliwa na Serikali kuendelea na vikao vya Bunge Maalumu haukujali vilio vya wananchi wanaotaka maoni yao yazingatiwe.

Kutokana na sintofahamu iliyopo sasa kuhusu Katiba mpya, vikao vya kutafuta suluhu kati ya CCM na Ukawa vimekuwa vikivunjika bila kuwa na mwafaka, hali inayolifanya taifa kuwa njia panda.

Juni 25, mwaka huu, kikao kati ya viongozi wa CCM na wale wanaounda Ukawa, kilishindwa kupata mwafaka baada ya pande hizo mbili kuendelea kuvutana.

Kikao hicho cha siri kilichofanyika katika Hoteli ya Sea Cliff, Masaki jijini Dar es Salaam, kiliongozwa na Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Fransis Mutungi.

Jaji Mutungi aliingilia kati suala hilo, baada ya kuona mwafaka wa Ukawa kurudi bungeni umekwama kutokana na madai kuwa wajumbe wa CCM wanajadili mambo yasiyokuwamo ndani ya rasimu ya Katiba iliyowasilishwa na Jaji Warioba.

- Advertisement -

Related Articles

4 COMMENTS

  1. Wananchi tunasikitika kuona migogoro inayofanyika bungeni. Je hawa wabunge wameenda shule? wameelimika au walisoma tu? Kwa nini hawana busara wala maarifa? Ni aibu sana migogoro inayojitokeza mara kwa mara bungeni kwa kuwa walio ndani ya bunge ni wasomi na watu wenye busara na wanao uwezo wa kufikiri kabla ya kutenda ili kuzuia migogoro. uwezo wao wa kukubali kukaa bungeni na kuzungumzia masuala ya katiba unaonesha kuwa ni mdogo sana kwa kuwa hawawezi kutatua matatizo yanayojitokeza na kwamba huenda kikubwa wanachofuatilia ni posho tu. hatutegemei kuwa kutakuwa na suluhisho la kuridhisha endapo hawatatumia busara na hekima katika kuandaa katiba. Katiba inasitishwa ili iweje? wabunge waende shule kwanza? au kuna wengine wenye busara ambao watakuwa badala ya hao? kama pesa zinatumika visivyo bunge likisitishwa litakapoanza bunge hilo tena wajitegemea au bado watataka posho? kwa kuwa hali hii haielekei kuwa itabadilika isipokuwa ubinafsi ukiondoka. ninaposema ubinafsi ni ile hali ya mtu kuwa pale bungeni kwa ajili ya posho na kutia vurugu. tujiulize ni nini hasa kinachoniweka pale bungeni? kama kweli upo bungeni kwa ajili ya kutenda kile kinachokupasa tatizo haliwezi kuwapo kwa kuwa kuna utaratibu wa kutumia busara na hekima katika kujibizana tena kwa unyenyekevu. pale inapotokea jazba ndio kunakoleta matatizo na ushindani ambao ukiangalia ni kukosa hekima na busara. mambo ni kuelewana kwa kutumia hekima busara na elimu uliyo nayo. kuna sababu gani ya jazsba? bunge si lako wala siyo wewe peke yako unaweza kutoa hoja bora ujitoe kuliko jazba ambazo zinavuruga bunge lote na kuongeza muda na muda huo unagharimiwa. haya yote ukiyajumlisha utanona mizizi yake ni ubinafsi na kukosa upendo. penye upendo wa kweli na ukweli Mungu huwepo kuongoza na hapatokei lolote baya. mwisho napenda kusema kuwa upendo una nguvu ya kushinda kila ubaya. Chuki ina kila aina ya ubaya. na hizi chuki zinaashiria ubinafsi ambao haujitokezi kiuwazi lakini kiundani ndivyo.

  2. Ni vema rais kikwete akisitisha bunge maalumu la katiba linaloendelea dodoma ili kuzuia hali ya sintofahamu inayoweza kujitokeza kama ilivyo kwa ndugu zetu wa kenya na kupelekea kwa viongozi kushitakiwa kwenye mahakama ya kimataifa hague uholanzi.

  3. kwa kweli hii inasikitisha sana kuona nchi yetu inakosa dira. ninaloliona hapa ni kukosa mfumo dhabiti wa kuongoza nchi, hii nchi iliiokoke na matatizo ya umaskini ni bora kubadilisha uongozi wote uliokuwepo na hili lichama lililozeeka CCM maana hawa hata kiongozi awe nani haiwezekani maana watalindana na wananchi kuendelea kuteseka sana, bora tumuweke mtu mwingine atoke chama kingine mpaka naye azoeane na kulindana na watu hivi nchi hii itakuwa imebadilika. ndugu zanguni wananchi lazima tuwe makini hao wakina Arti afi, leticia nyerere na john magale shibuda ni njaa ndizo zimewapeleka huko hakuna lolote tena hao ndio hawana dhamira ya dhati kuwasaidia wananchi wao. wanakwenda kujadili masuala ya uvuvi, ardhi yanahusianaje na muungano

  4. Ingependeza kama viongozi wa ccm na UKAWA wafikie makubaliano kabla kumalza bunge la katiba ambapo inaonekana ulafi wa pesa za walipa kodi ndizo zina wafanya kuingia bungeni na hali wanajua katiba haitakuwa na afya,kama haina afya maana yake nn? Wanatudanya ni wazalendo,kama kwel ni wazalendo wacngeweza kupoteza pesa kwa kujadili katiba isiyokuwa na afya, Ili tupate uongoz usiokuwa na afya,Ni bora hizo pesa wangejenga maabara shule za kata za wato maskini.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles