30.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Ukawa ni gumzo

Wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba wanaunda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA).NA WAANDISHI WETU, DAR ES SALAAM

HATUA ya vyama vya upinzani vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kutangaza kuungana imepokewa kwa hisia tofauti na watu wa kada mbalimbali ambapo baadhi yao wamepongeza na kutoa angalizo kwa viongozi wake.

Vyama hivyo vilisaini maazimio saba juzi jijini Dar es Salaam yatakayoviongoza kuelekea katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika mwaka huu pamoja na Uchaguzi Mkuu mwakani.

Akitangaza makubaliano ya umoja huo ambao unaundwa na vyama vya Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Jangwani, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibroad Slaa, alisema hatua hiyo itafungua ukurasa mpya na kiu ya Watanzania ya muda mrefu.

Wakizungumza na MTANZANIA kwa nyakati tofauti jana, watu mbalimbali walipongeza hatua hiyo na kusema ni jambo jema katika kuimarisha demokrasi nchini.

WAZIRI WASIRA

Akizungumzia makubalino hayo ya Ukawa, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Steven Wasira, alisema mawazo ya kisiasa yanapimwa na wananchi.

“Kuungana sawa, lakini mimi ninafikiri wangevunja vyama vyote na kubaki kimoja ndiyo wataacha ubishi… mawazo ya kisiasa yanapimwa na wananchi na siamini kuungana kwao kama kutaleta tofauti.

“Pamoja na muungano wao, lakini CCM itaendelea kushindana nao iwe kwa kundi lao kwa pamoja au wakiwa chama kimoja kimoja kwa sababu kuungana na kufikia malengo ni mambo mawili tofauti,” alisema Wasira.

PROFESA MPANGALA

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Ruaha (RUCO), Profesa Gaudence Mpangala, alisema hatua hiyo itawapa nguvu hasa katika ushindani wa mfumo wa vyama vingi.

“Kwa historia ya Tanzania upinzani haujawa na nguvu kushindana na CCM, lakini kwa hatua waliyoifanya inawapa nguvu zaidi.

“NARC Kenya isingeweza kuishinda Kanu kama isingeamua kushirikiana… watafanikiwa ingawa si katika kila kitu, uwezekano wa mgombea wao kupita utakuwa mkubwa zaidi kuliko ilivyokuwa zamani,” alisema Profesa Mpangala.

DK. LWAITAMA

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Josia Kibira, Dk. Azaveli Lwaitama, alisema hatua ya vyama hivyo kuamua kushirikiana ni maendeleo mazuri kwa demokrasia nchini.

“Demokrasia ya vyama vingi itakuwa imekamilika CCM itakapoondolewa madarakani, na CCM haiwezi kujiondoa yenyewe madarakani lazima kuwapo na nguvu kubwa.

“Ni jambo jipya na lina afya kwa demokrasia ya Tanzania,” alisema Dk. Lwaitama.

Kwa mujibu wa mhadhiri huyo, vyama vya upinzani vinapoungana kwa suala la kitaifa kama la kudai Katiba yenye maslahi ni jambo jema kwa sababu zamani vilikuwa na ajenda ya kutaka kuiondoa CCM peke yake.

“Wamejitahidi sana, wameanza kutengeneza mazingira ya kisheria kwa sababu huko nyuma ilikuwa ni maneno tu.

“Ni ubunifu mzuri, wametengeneza mazingira kwamba vyama viingie kwenye mashauriano na makubaliano,” alisema.

BASHIRU ALLY

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Bashiru Ally, alisema vyama hivyo vitapimwa kwa yale waliyoyaahidi.

“Hivi sasa ni mapema kusema kama watafanikiwa au la, waanze kwanza halafu tuone kama walichokiahidi watakitekeleza kwa sababu wameweka mkataba hadharani,” alisema Ally.

Hata hivyo alishauri hata kama vyama hivyo vitaenda na utambulisho wa Ukawa, lakini ni vyema viangalie kwa makini utambulisho wa vyama vyao ili usipotee.

“Suala la utambulisho wa vyama vyao na lenyewe linahitaji kuangaliwa kwa sababu vyama vyote hivi vimesajiliwa na vingine vina miaka 20, lakini utambulisho wa Ukawa ni wa siku moja,” alisema.

ASKOFU DK. KITULA

Mwenyekiti Mstaafu wa Jumuiya ya Kikristo (CCT), Askofu Dk. Peter Kitula, alipongeza hatua hiyo na kusema kwa kuwa hawajalazimishwa na mtu, ni vyema wakajiepusha na uroho wa madaraka.

“Kwa kuwa hawakulazimishwa ni uamuzi mzuri, lakini huko mbeleni wasije wakagombania madaraka. Wafanye yale mazuri bila kuathiri amani na utulivu nchini,” alisema Dk. Kitula.

ASKOFU NIWEMUGIZI

Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Maaskofu wa Katoliki (TEC), Askofu Severine Niwemugizi, alisema vyama hivyo vinapaswa kuwa makini ili ushirikiano wao uwe na maana.

“Si mara ya kwanza kusikia habari kama hiyo, lakini kama wana dhamira ya dhati wanapaswa kuwa na nia ya kweli na kufanya kazi pamoja.

“Waepuke ubinafsi hasa katika kuchagua mtu ambaye watamsimamisha kugombea urais kwa sababu chama fulani kinaweza kikadhani kina nguvu kuliko kingine kwa ajili ya kutafuta kufika kwenye madaraka,” alisema Askofu Niwemugizi.

SHEIKH KUNDECHA

Amir wa Baraza Kuu la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania (Baraza Kuu), Sheikh Mussa Kundecha, alisema wananchi hawapaswi kuwa watabiri katika muungano wa Ukawa bali wanapaswa kuzungumzia uhalisia uliopo.

“Hili hatutakiwi kutabiri, tunatakiwa kuongea uhalisia sio kazi yetu kutabiri mabaya kama wataendelea na muungano au watakosana,” alisema Sheikh Kundecha.

TUCTA

Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA), Nicholas Mgaya, alisema kama ushirikiano huo utatiliwa mkazo utaleta matunda mazuri.

“Kitu kikubwa tunachotaka ni demokrasia yetu isiyumbe, na ili isiyumbe tunatakiwa kuwa na upinzani ulio thabiti kwa sababu maana ya upinzani ni kuiangalia Serikali iliyoko madarakani na kuhakikisha inatimiza yale iliyoahidi kwa watu waliowapigia kura,” alisema Mgaya.

PPT-MAENDELEO

Mwenyekiti wa Chama cha PPT-Maendeleo, Kuga Mziray, aliipongeza hatua hiyo kwa sababu itapunguza utitiri wa wagombea.

“Mimi na chama changu tunawatakia kila la kheri kwa sababu tutapunguza utitiri wa wagombea, lakini wanapaswa wasome vizuri sheria ya vyama vya siasa,” alisema Mziray.

Hata hivyo Mziray alionyesha wasiwasi wake katika suala la ruzuku kwani atakaposhinda mgombea wa chama cha Chadema au NCCR-Mageuzi ruzuku itakwenda kwa chama husika na hivyo inaweza kuleta mgongano.

WANANCHI WA KAWAIDA

Mkazi wa Makumbusho jijini Dar es Salaam, Yudathade Assenga, alisema makubaliano hayo yatafanikiwa endapo hakutakuwa na tamaa ya madaraka.

Alisema kutakapotokea mgongano wa maslahi kati yao watashindwa kutekeleza waliyoazimia.

Mwananchi mwingine, Ashura Rajabu mkazi wa Dar es Salaam akizungumzia muungano huo, alisema wataleta ushindani mkubwa kama watakuwa na nia moja.

Hata hivyo si mara ya kwanza kwa vyama vya upinzani nchini kuungana. Mwaka 2000 Chadema kiliungana na CUF na hata kukubaliana kuachiana majimbo katika Uchaguzi Mkuu.

Makubaliano hayo kwa upande wa Chadema yalisainiwa na aliyekuwa Mwenyekiti wake, marehemu Bob Makani na Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba.

Habari hii imeandaliwa na Nora Damian, Aziza Masoud na Jonas Mushi (Dar)

- Advertisement -

Related Articles

5 COMMENTS

  1. SASA KUMEKUCHA…..NAONA UKAWA NI GUMZO HATA NJE YA TANZANIA, UKAWA,UKAWA….UKAWA.

    CCM na vibaraka vyake na waandishi wake waliohongwa kwa kazi hiyo, wameanza kuchonga na kuweweseka. Kazeni kamba UKAWA, kenya waliungana wakaityupa Kanu, Zambia MMD waliungana wakaitupa UNIP, kwa nini siyo Tanzania? Wananchi msikatishwe tamaa na wanasiasa uchwara wa CCM, ungeni mkono jitihada hizi mpya. Ni wakati wa matatizo ndiyo hata maadui wanaungana, Tazama jinsi ” PIlato alivyoungan na Kayafasi ili kutoa kafara Yesu.” Mbona hii ni sababu nzuri, wananchi miaka yote mlilia kwamba vyama viungane, sasa vimeungana, ewananchi ungeni mkono, CCM imekufa tayari, na haiwezi kusaidia kitu sasa, kinachiotakiwa nikuwakabidhi nchi UKAWA, nao wajaribu, mbona ccm miaka 53 imeshindwa kuleta maendeleo bali imeleta Ufisadi, chuki, udini, utapeli, uporaji wa maliya umma(tembo), unyanyasaji wa polisi, mikataba feki na kuwaruhusu wachina watunyanyase, hikini chama gani hicho?Kipumzike, Watanzania kazeni moyo konde, msikatishwe tamaa na maneno ya watu wenye hofu hasa ccm. Kumbuka “UKAWA TUMAINI JIPYA LA WATANZANIA”. Mungu ubariki Ukawa, kitu chema lazima kiungwe mkno bila kujificha, sitakiunafiki” ukweli unaniweka huru” usikose mada ya kesho katika gazeti la Mwananchi.

  2. Kutakuwa na kiwewe hofu na mashaka makubwa kwani kuungana kwa vyama hivi chini ya mwavuli wa Ukawa ni tishio kubwa. Kwa chama tawala ambacho serikali yake imefikia kwenye siasa za kuangamizana (Politics of Elimination)tena kwa uwazi kabisa, sio rahisi kuachia madaraka ila kwa kutumia nguvu ya ziada. Ukiangalia walivyoipinda katiba mpya inayotarajiwa, ndipo utagundua kuwa hawa wanataka kukaa madarakani milele. Lakini kwa muungano huu wa Ukawa, hata wao wanajua kuwa huko mbele kuna kazi. Umoja ni nguvu kubwa na utengano ni udhaifu mkubwa. Kila mwananchi na aunge mkono juhudi hizi za wenzetu wanaotaka kuikomboa nchi

  3. Wakati sasa umefika kwa ajili ya Watanzania kuamka na kujitambua. Haki na wajibu huambatana. Tunadai haki ya kupata huduma bora na kunufaika na matunda ya nchi yetu, je, tunatimiza wajibu wetu wa kuhakikisha kuwa tunawajibika kufuatilia masuala ya muhimu ya nchi kama vile kujiandikisha kupiga kura na kujitokeza siku ya kupiga kura.

    Viongozi hawa wa kitaifa wa vyama 4 vya siasa wametupa funzo kuwa siku zote maslahi ya wananchi kwanza na vyama baadaye. Hii ndio maana wameungana. UDP, TLP na vyama vingine vidogo visiende vyenyewe, vishikamane kwa ajili ya ustawi wa nchi yetu.

  4. Kuna muungwana hapo juu kasema demokrasia itakamilika CCM itakapong’olewa. Sidhani kama hii ni “digestion” ya kisomi. Kuna Sheikh mmoja hapa kasema vizuri sana, na nadhani tunatakiwa tuwe na mtazamo wake. Huyu aliyezungumzia upungufu wa utitiri wa wagombea kagusa mada vyema kabisa. Wananchi wa kawaida wametamatisha vyema zaidi. Kwa mtazamo wangu sasa tuko pazuri. Tunahitaji vyama vichache, viwili au vitatu (hata Baba wa Taifa aliwahi kutuasa hivi) ndipo vitaonesha nguvu nzuri ya kupingana. Tumwombe Mungu umoja huu usivunjike, na hata ikibidi siku zijazo waainishe kiwe chama kimoja. Pia tukumbuke CCM si maadui, na tukifaulu kuking’oa kitakufa, na matokeo yake yanaweza kuwa mabaya zaidi kuliko tunavyofikiria. “to any action there must be a reaction.”

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles