25.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Ukawa, Mwigilu wateta na Rais wa Ujerumani

GauckNa Elizabeth Hombo, Dar es Salaam
VIONGOZI wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), wamefikisha kilio chao kwa Rais wa Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani, Joachim Gauck na kudai kuwa Serikali ya Rais Jakaya Kikwete imekuwa ikiwanyanyasa kwa kutumia Jeshi la Polisi, pindi wanapokuwa wana mikusanyiko ya kisiasa.
Hatua hiyo imekuja siku moja baada ya Rais Kikwete kukutana na rais huyo wa Ujerumani Ikulu jijini Dar es Salaam na kueleza kuwa tukio la kipigo cha Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahimu Lipumba na wafuasi wake kilitokana na kuvunja sheria.
Viongozi hao wa Ukawa ambao waliongozwa na Profesa Lipumba pamoja na Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Wilbroad Slaa waliiambia MTANZANIA jana kuwa katika kikao chao na Rais Gauck, kilichofanyika juzi walitumia fursa hiyo kueleza hali ya kisiasa nchini na namna vyama vya upinzani hasa viongozi wake wanavyokuwa wakidhalilishwa na vyombo vya usalama.
Katika mkutano huo, Chama cha NCCR-Mageuzi, kiliwakilishwa na mwanasheria wake Mohamed Tibanyendera, huku Chama Cha Mapinduzi (CCM) kiliwakilishwa na Naibu Katibu Mkuu wake (Bara0, Mwigulu Nchemba.
Katika mkutano huo, Dk. Slaa alisema walimweleza Rais Gauck mwenendo wa demokrasia hapa nchini na namna Rais Kikwete alivyopotosha ulimwengu kuwa CUF hawakutimiza taratibu za kufanya maandamano.
“Tumemweleza kila kitu, kwanza inasikitisha mkuu wa nchi anapokosa woga, anadanganywa na watendaji wake na baadaye yeye mwenyewe, umma na ulimwengu kwamba CUF hawakufuata taratibu walipotaka kuandamana kukumbuka wapendwa wao.
“Tumeeleza utaratibu wa vyama kufanya maandamano au mikutano ya hadhara kwamba ni kutoa taarifa polisi ndani ya saa 48, CUF walitoa taarifa Januari 22 lakini walijibiwa Januari 25 jioni wakati ofisi zimeshafungwa.
“Sasa leo asubuhi (jana) ndio tumetoka kuonana na Rais wa Ujerumani tumemweleza mambo mengi sana ikiwepo hali ya demokrasia hapa nchini kwa sababu anatakiwa kujua kila kinachoendelea,”alisema Dk. Slaa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba alisema alimweleza yote yaliyotokea siku waliposhambuliwa na Jeshi la Polisi.
Profesa Lipumba alisema katika mkutano huo Rais Gauck alionyesha kusikitishwa na kauli za Serikali kuhusu kupigwa kwake kwa madai ya kuwa chama chake hakikufuata taratibu za maandamano.
“Rais Kikwete alidanganya lakini nimemweleza rais wa Ujerumani yote yaliyotokea kwamba tulitoa taarifa lakini polisi ikachelewa kuleta barua ya kusitisha maandamano, baadaye nikawaeleza wanachama kwamba kuhusu hilo na wakati naelekea Mbagala kuwaambia wanachama wengine ndipo tukazuiliwa, tukakamatwa na kupigwa,”alisema Profesa Lipumba.
Alisema baada ya kumweleza hayo yote ndipo rais huyo wa Ujerumani akamhoji kwamba ni kwanini hauchukui hatua ya kuwashtaki polisi mahakamani.
“Nikamjibu kwamba sisi ndio tumeshtakiwa na kesi yetu iko mahakamani…alisikitika sana kusikia hivyo huku akinishauri kwamba nisubiri kwanza kesi hiyo iishe na kwamba jukumu la kujenga demokrasia ndani ya nchi ni letu sote,”alisema Profesa Lipumba.
Mbali na hilo, Profesa Lipumba alisema rais huyo alimshauri awasilishe malalamiko yake kwa Balozi wa Ujerumani hapa nchini ikiwemo kueleza yaliyomkuta wakati wa maandamano yaliyofanyika Januari 27, mwaka huu.
“Baada ya kunishauri hivyo nikamwambia kuwa wanaosikilizwa zaidi ni viongozi wa Serikali na chama tawala lakini si wapinzani,”alisema.
Pia alisema kuwa wamemweleza rais huyo kuhusu namna ambavyo hawatashikiri katika kura ya maoni kwa sababu daftari la wapiga kura bado halijafanyiwa marekebisho.
“Akatujibu kwamba yote ameyapokea na kwamba atayafanyia kazi na hapo hapo akamwuliza Naibu Katibu wa CCM, Mwigulu Nchemba ambaye naye alikwepo kwenye kikao hicho kuwa daftari la wapiga kura litakuwa tayari lini? Lakini alimjibu kwamba Tume ya Uchaguzi itakamilisha hivi karibuni,”alisema Profesa Lipumba.
Viongozi wa vyama vya siasa walioshiriki katika mazungumzo hayo ni Dk. Slaa (Chadema), Profesa Lipumba (CUF), Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Mwigulu Nchemba pamoja na Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe, huku NCCR-Mageuzi ikiwakilishwa na Mohammed Tibanyendera.
Akizungumzia sheria ya maandamano, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk. Helen Kijo Bisimba, alisema sheria husika ni ‘Public Order ACT cap 385’ ambayo inaruhusu maandamano.
“Mikutano na maandamano inaruhusiwa na political parties Act 1992 chapter 258 kifungu cha 4 hadi 8 kinatoa maelekezo ya jinsi ya kufanya na sheria ya Police force & Auxiliary Services Act Chapter 323.
“Kinachotakiwa ni kutoa notisi ya saa 48 kabla na baada ya hapo kuendelea, polisi wanatakiwa wajibu kwa maandishi iwapo kuna tatizo,” alisema.
Januari 27, mwaka huu Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, lilazimika kutumia nguvu kubwa kupambana na wafusi wa CUF, waliokuwa wanaandamana katika kile kilichoelezwa kukumbuka mauaji ya wanachama wake yaliyotokea Januari 26 na 27, mwaka 2001 visiwani Zanzibar.
Katika harakati hizo, askari walimpiga Profesa Lipumba kwa kutumia kitako cha bunduki na kisha kirungu, mpigapicha wa gazeti la Jambo Leo, Hamisi Mussa, aliyekuwa anatekeleza majukumu yake ya kazi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles