25.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

Ukawa, CCM wazichapa kavukavu

CHRISTINA GAULUHANGA Na TUNU NASSOR-DAR ES SALAAM

MADIWANI wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) na wale wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), jana waliugeuza ukumbi wa Aanautoglou kuwa ulingo wa masumbwi baada ya kuchapana ngumi.

Hatua hiyo ilitokana na madiwani wa Ukawa kulalamikia kuwa kura zilizompa ushindi mgombea wa CCM, Omary Kumbilamoto hazikuwa halali.

Vurugu hizo zimetokea, baada ya Kumbilamoto kutangazwa mshindi kwa kuwabwaga wapinzani wake kutoka Chadema na CUF.

Katika uchaguzi huo, Kumbilamoto alifanikiwa kutetea kiti hicho kwa kupata kura 27, huku mgombea wa CUF ambaye ni Diwani wa Kata ya Buguruni, Adam Rajabu alipata kura 25 na Diwani wa Tabata, Patrick Assenga (Chadema) akiambulia patupu.

MWANZO WA VURUGU

Vurugu hizo zilianza baada ya madiwani kupiga kura na kwenda kuhesabiwa katika chumba cha kuhesabia kura.

Wakati matokeo yakisubiriwa, mgombea wa Chadema, Asenga alitoka ndani ya chumba hicho akipiga kelele kuwa CCM wameanza kuharibu uchaguzi.

Asenga alidai msimamizi wa uchaguzi huo ambaye ni Kaimu Katibu Tawala wa Wilaya ya Ilala, Jabir Makame alihalalisha kura ambazo ziliharibika kutokana na wajumbe wanne wa CCM kukosea kuandika majina.

Wakala wa Kumbilamoto ambaye ni Diwani wa Kata ya Chanika, Deogratius Masaburi, alitoka katika chumba hicho akishangilia na alikutana na Assenga akiwa na madiwani wa upinzani wakilalamika kuibiwa kura na hapo vurugu zikaanza. Madiwani wengine waliinuka na kuanza kurushiana ngumi na kutoleana lugha chafu.

POLISI WAVAMIA UKUMBINI

Tukio hilo lilisababisha polisi kuvamia ukumbi huo, kisha wengine kuingia katika chumba cha kuhesabia kura kuimarisha ulinzi.

Hali hiyo, ilizidisha vurugu kwa baadhi ya wanachama wa vyama hivyo waliokuwa wamekaa ukumbini eneo la juu kuanza kurusha chupa za maji.

Katika uchaguzi huo, ulioongozwa na Kaimu Katibu Tawala wa Ilala, Jabir Makame, wajumbe kutoka upande wa upinzani walikuwa wakilalamikia kutoridhishwa na mwenendo wa uchaguzi huo na kusababisha kelele za mara kwa mara.

Awali wagombea walianza kwa kujinadi, kisha wajumbe wa mkutano huo wakiongozwa na Meya wa Manispaa ya Ilala, Charles Kuyeko kuanza kupiga kura.

Baada ya shughuli ya upigaji kura kukamilika, msimamizi wa uchaguzi aliwataka wagombea kila mmoja kuweka wakala ili aende chumba maalumu akahesabu kura zake.
Hata hivyo, wagombea Rajab na Assenga walienda wao wenyewe chumba hicho kuhesabu kura zao huku Kumbilamoto akimweka wakala wake.

Kabla uchaguzi huo kuanza, Assenga aliomba kujiuzulu ili asigombee nafasi hiyo, lakini msimamizi alikataa kwa madai kuwa sheria za uchaguzi zinamtaka mgombea anayetaka kujiondoa katika uchaguzi awe ametoa taarifa ndani ya saa 24.

RPC
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Salum Hamduni alisema bado anafuatilia kwa watendaji wake kujua idadi ya watu waliokamatwa katika tukio hilo.

“Niko nje ya ofisi bado sijapata taarifa kutoka kwa askari waliokwenda kusimamia uchaguzi huo, nafuatilia kujua kama kuna waliokamatwa,” alisema Hamduni.

 

WAGOMBEA WAZUNGUMZIA MATOKEO
Akizungumzia matokeo, Rajab alisema amesikitishwa na mwenendo wa uchaguzi huo akidai kwamba polisi walionyesha kutumia nguvu kumpa ushindi mgombea wa CCM.

Alisema kuanzia sasa Watanzania wanatakiwa waelewe kwamba hakuna demokrasia na kamwe hatarudia tena kugombea nafasi yoyote kwa sababu ya dhuluma wanayofanyiwa.
“Nimesikitishwa na matokeo haya kwa sababu inaonyesha dhahiri polisi waliweka nia ya kulazimisha ushindi kwa CCM,” alisema Rajab.

Alisema kwakuwa yeye ni baba wa familia ana maisha yake, ni vyema akaelekeza kwa sasa nguvu zake kuhudumia familia yake.
Kwa upande wake, Assenga alisema matokeo ya uchaguzi huo ni aibu kwa Serikali na chama tawala.

Alidai kuwa alishuhudia polisi wakimlazimisha mgombea wa CUF achukue kura zake na kumpa wa CCM ili ashinde.
Assenga alisema kitendo hicho kinaonyesha dhahiri jinsi nguvu ya dola inavyotumika katika chaguzi mbalimbali hapa nchini.

“Polisi wanalazimisha matokeo, nimeshuhudia kwa macho yangu wakichukua kura za mgombea wa CUF ambaye alishinda na kumpa wa CCM,” alidai Assenga.
Kwa upande wake, Kumbilamoto alisema anashukuru Mungu uchaguzi umeenda vizuri, sasa kazi aliyokuwa nayo ni kuwaunganisha madiwani wa upinzani na wa CCM waweze kufanya kazi pamoja.

Alisema iwapo watashirikiana wataweza kuongeza mapato kutokana na kukamilika kwa miradi mbalimbali.
“Nashukuru nimepata kura moja kutoka kwa upinzani na ninaahidi kufanya kazi nao bila kujali itikadi zao,” alisema Kumbilamoto.

WAZUIWA KUSHIRIKI UCHAGUZI
Awali kabla ya kuanza kwa uchaguzi huo, wajumbe Suzan Lyimo (Chadema) na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, kazi, Vijana, Ajira na wenye ulemavu, Stella Ikupa (CCM) walizuiliwa kushiriki baada ya kukosa sifa kutokana na waziri mwenye dhamana kushindwa kuwatambua.

Hata hivyo Suzan hakuhudhuria, lakini Stella alikuwapo na alitolewa nje ya chumba cha uchaguzi.
Kabla ya kuanza kwa uchaguzi huo, madiwani wapya waliapishwa ambao ni Kumbilamoto (Vingunguti), Hussein Togolo (Zingiziwa, CCM) na diwani wa viti maalumu, Nuru Chuma (CUF ).

Nafasi ya Naibu Meya Ilala ilikuwa wazi baada ya aliyekuwa akiishikilia, Kumbilamoto kujiuzulu hivi karibuni na kuhamia CCM.

Vurugu kama hizo ziliwahi kutokea wakati wa uchaguzi wa Naibu Meya wa Jiji la Dar es Salaam uliohusisha mgombea wa CCM, Mariam Lorida na Mussa Kafana wa CUF.
Uchaguzi huo ulitawaliwa na vibweka, vitimbi na majibizano kati ya wajumbe kutoka vyama vinavyounda Ukawa dhidi ya wale wa upande wa CCM.

Ukawa hawakuwa tayari uchaguzi huo kufanyika kwani mgombea wao hakuwepo ukumbini, huku CCM wakiona ipo haja ya kufanyika ili shughuli za kimaendeleo zifanyike.
Kuhusu kutokuwapo kwa mgombea wao, Meya wa Ubungo, Boniphance Jacob alidai kuwa huenda ametekwa.

Kauli hiyo iliwakera baadhi ya wajumbe wa upande wa CCM na hasa Meya wa Temeke, Abdallah Chaurembo aliyetaka Jacob aifute.
Baada ya matokeo kutangazwa, Meya Jacob alimkaba koo Meya wa Temeke Chaurembo alipotaka kusogelea karatasi za kura.

Hali hiyo ikaibuka malumbano baina ya pande mbili, kiasi cha askari polisi waliokuwa wamevaa kiraia kuamua kuingilia kati ili amani iendelee.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles