29.2 C
Dar es Salaam
Monday, March 20, 2023

Contact us: [email protected]

Ukatili wa ngono kwa watoto watikisa

TUNU NASSOR-DAR ES SALAAM

MATUKIO ya ukatili dhidi ya watoto yameongezeka kutoka 4,728 kwa mwaka 2017 hadi kufikia 6,376 mwaka 2018.

Akizungumza katika uzinduzi wa ripoti ya haki za binadamu kwa mwaka 2018, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga, alisema changamoto kubwa iliyokuwapo ni ukatili wa kingono, hasa ubakaji na ulawiti.

 Alisema ukatili huu mara nyingi umekuwa ukifanywa na ndugu wa karibu kama baba, mama, kaka pamoja na watoto wenzao wawapo shuleni.

 “Aina hii ya ukatili imekuwa changamoto kwa wilaya 20 katika mikoa yote 10 ambayo imetembelewa na LHRC kwa mwaka 2018 na hasa mikoa ya Mwanza, Dar es Salaam, Kilimanjaro, Mbeya, Iringa, na Singida,” alisema Anna.

Aliongeza kuwa matukio ya ubakaji wa watoto yaliongezeka kutoka 759 katika kipindi cha miezi sita ya mwanzo ya 2017 hadi kufikia matukio 2,365 katika kipindi kama hicho mwaka 2018.

Anna alisema katika matukio ya ukatili wa watoto yaliyoripotiwa na vyombo vya habari na kukusanywa na kituo hicho, asilimia 91 ni ukatili wa kingono huku asilimia 9 ikiwa ni ukatili wa kimwili na kisaikolojia.

“Jitihada za kupambana na ukatili huo zinahitajika zaidi ili kusaidia kuondokana na ukatili huo ambao unawaathiri watoto kisaikolojia,” alisema Anna.

Alisema hata hivyo haki ya kuishi imeendelea kuimarika nchini ikiwa kwa mwaka 2018 hakuna tukio lililoripotiwa la mauaji ya watu wenye ualbino.

Aliongeza kuwa haki ya kupata dhamana pia imeimarika baada ya Waziri wa Mambo ya ndani, Kangi Lugola kuruhusu kutoa dhamana siku za mwisho mwa wiki na sikukuu.

“Jambo jingine zuri ni mahakama kuanza kuzifanyia kazi kesi zinazohusu watoto,” alisema. 

Alisema kuna mambo ambayo hayakufanya vizuri ikiwamo haki za kujieleza, kupata habari, kukusanyika ambayo bado yamekuwa na changamoto.

Naye Ofisa Mtafiti wa LHRC, Fundikila Wazambi, alisema ripoti hiyo pia imebaini kuimarika kwa haki ya kuishi kutokana na kupungua kwa matukio ya wananchi kujichukulia sheria mkononi.

 “Wastani wa watu 65 kwa mwezi waliuawa kutokana na wananchi kujichukulia sheria mikononi ambapo katika kipindi cha miezi sita ya kwanza 2018 jumla ya matukio 385 yaliripotiwa,” alisema.

Wazambi alisema mauaji yanayotokana na imani za kishirikina yamepungua kutoka 307 Juni mwaka 2017 hadi kufikia 106 Juni 2018.

Alisema kwa mwaka 2018 uhuru wa kukusanyika uliathiriwa na katazo la kutokufanya mikutano ya hadhara nje ya jimbo la mwanasiasa husika.

 “Wanasiasa kadhaa wa vyama vya upinzani walikamatwa kwa kutotii katazo hilo japo halina uhalali kisheria,” alisema Wazambi.

Aliongeza kuwa wanawake wamekuwa wakikumbana na ukatili wa kingono, kiuchumi, kimwili na kisaikolojia, ulawiti kwenye ndoa, rushwa ya ngono na manyanyaso katika utoaji wa matunzo ya mtoto.

Akizungumzia haki za kijamii, Wazambi alisema sera ya elimu bure imesaidia kuongeza upatikanaji wa elimu msingi japokuwa inakabiliwa na changamoto ya uhaba wa madarasa kwa wanafunzi wanaomaliza darasa la saba, umbali mrefu kati ya nyumbani na shuleni na bajeti isiyotosheleza kwa sekta hiyo.

 “Shule zinapungukiwa matundu ya vyoo, walimu, vifaa vya kujifunzia, mimba za utotoni, na mazingira duni ya kufanyia kazi walimu,” alisema Wazambi.

 Aliongeza kuwa katika sekta ya afya Serikali imechukua hatua kadhaa ikiwa ni pamoja na maandalizi ya ujenzi wa hospitali 60 za wilaya, lakini bado inakabiliwa na changamoto za uhaba wa hospitali, zahanati, vituo vya afya na uhaba wa wafanyakazi.

“Pia sekta ya afya inakabiliwa na ufinyu wa bajeti, fedha zilizotengwa kuchelewa, uhaba wa vitanda, dawa na vifaa vya afya,” alisema.

Kwa upande wa upatikanaji wa maji safi, Wazambi alisema mwaka 2018 hayakupatikana kirahisi jambo lililosababisha wanawake na wasichana kutumia muda mwingi kutafuta maji.

Kwa upande wake, mhanga wa matukio ya unyanyasaji wa kingono kutoka Kigoma, Ramla Issa alisema wanawake katika Mkoa wa Kigoma wamekuwa wakinyanyaswa kingono na watu wanaojiita ‘Tereza’.

Alisema unyanyasaji huo umekuwa ukiwapata zaidi wanawake wasioolewa, mabinti na walioolewa, lakini waume zao wana kazi ya kusafiri ama kutoka alfajiri kwa majukumu mengine.

 “Watu hawa wanakuja na mapanga na kulazimisha kufanya ngono mbele ya watoto na ukikataa wanakukata na panga,” alisema Ramla.

Alisema kwa muda wa miaka mitano wamekuwa na vitendo hivyo na kuwasababishia hofu wanawake na mabinti.

 LHRC imekuwa ikizindua ripoti ya haki za binadamu kila mwaka kuangazia mambo mbalimbali ya haki za binadamu ili kuweza kujitathmini na kujipanga upya kwa ajili ya kulinda haki za binadamu nchini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
210,784FollowersFollow
563,000SubscribersSubscribe

Latest Articles