23 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Ukarimu kwa wahamiaji unapomponza Angela Merkel

angela-merkelSIASA inafanana na safari ya mashua inayotumia matanga yanayopulizwa na upepo unaosukuma chombo hicho baharini na anayejua kusoma nyakati za kusukumwa na upepo hutimiza malengo aliyokusudia bila kujali msimamo wake.

Chama tawala nchini Ujerumani kinachoongozwa na Kansela Angela Merkel cha CDU, kimegaragazwa katika uchaguzi na chama cha AfD chenye msimamo wa kihafidhina dhidi ya uhamiaji na Uislamu.

Katika uchaguzi wa Jimbo la Kaskazini Mashariki ambako wahafidhina hao wamezoa asilimia 21 wakinyakua nafasi ya pili nyuma ya chama cha SPD na CDU cha Merkel kimeshika nafasi ya tatu kwa asilimia 19.

Ni uchaguzi wa jimbo moja tu lakini umedhihirisha jinsi Wajerumani wanavyopingana na mtazamo wa Kansela wao kuhusiana na suala la wahamiaji wanaomiminika katika nchi hiyo wanaokingiwa kifua na sera za CDU ambapo Merkel amethubutu kupingana na viongozi wenzake barani Ulaya kuhusu suala hilo.

Inaashiria kihoro kwa Merkel kwani mwakani Ujerumani itafanya uchaguzi wa Bunge lake na tayari dalili za anguko kuu zinajidhihirisha, kwani licha ya vyama vyote kukitenga chama cha AfD kutokana na misimamo yake mikali lakini bado kina ufuasi wa kutosha, licha ya kuundwa miaka mitatu tu iliyopita kina uwakilishi katika mabunge tisa kati ya 16 ya uwakilishi jumuishi.

Kushindwa kwa Merkel jimboni Mecklenburg Pomerania Magharibi anakotokea ni kupigwa kelbu kwa sera zake za kupokea wimbi la wahamiaji, lakini wananchi hawakubaliani na mtazamo wake na kusababisha mabadiliko ya methali kwamba ‘mgeni (wahamiaji) njoo mwenyeji (Merkel) aangamie’ kwa kuwaonea huruma wahamiaji.

Wapiga kura wasipotimiziwa matakwa yao hata kama kuna mwanasiasa mwingine mwenye sera za ajabu, ni heri wamchague ili kumpinga aliyewachosha bila kujali sera zake kama kilivyo Chama cha Alternative Fuer Deutshland (AfD), kisichopenda wahamiaji na chenye msimamo mkali dhidi ya Waislamu kinachokonga wahafidhina wanaohofia usalama wao.

Lakini ni mapema mno kuamua kama Merkel amekwisha kisiasa licha ya mvuto wake kupungua sana miongoni mwa Wajerumani, kwani mwanasiasa huyo mkongwe ana kawaida ya kurudisha mvuto kwa mbinu mbadala kwa kuwa licha ya kutokukubalika kwa sasa hakuna mwanasiasa wa upinzani anayeweza kuwa mbadala wake.

Kinachomponza Merkel ni kufungua milango kwa wahamiaji bila kujali madhara ya magaidi wanaojipenyeza miongoni mwao, mwaka jana kiasi cha wahamiaji wapatao milioni moja na ushee waliruhusiwa kuingia nchini humo na kuwakera Wajerumani wenye uhafidhina walioamua kukipa kura chama cha AfD chenye hulka ya upinzani hata kwa EU.

Ingawa hakitarajiwi kuimarika zaidi kutokana na siasa zake za kibaguzi, CDU imekiri kuchomwa na ushindi wa AfD na inatafakari hatua ya kuchukua huku kiongozi wa AfD Leif-Erik Holm, akijinadi kuwa huu ni mwanzo wa mwisho wa Merkel ingawa CDU bado inatamba kuwa haijapunguza tija kwa wananchi licha ya kuwakirimu wahamiaji.

Lakini hupaswi kushangazwa na mashiko ya kiimani kwenye siasa za Ujerumani kwani si AfD pekee yenye msimamo huo, ambacho tangu kianzishwe kimebadili misimamo kutokana na uhafidhina ikiwemo kupinga matumizi ya sarafu ya Euro ingawa chenyewe kina wawakilishi saba kwenye Bunge la Jumuiya ya Ulaya.

Utata mwingine wa chama hicho kinachotumika kama bakora dhidi ya Kansela Merkel, ni kujumuisha katika sera zake za upinzani dhidi ya imani ya Kiislamu, pia kikidai kuwa maangamizi ya kihistoria yaliyofanya na Adolf Hitler dhidi ya Wayahudi yamekuzwa kuliko uhalisia.

Lakini hata Chama cha Christian Democratic Party kinachoongozwa na Merkel ambaye ni mtaalamu wa sayansi ya utafiti kina mwelemeo wa kiimani, ingawa hakina sera za kibaguzi kwani ni chama cha uhafidhina wa Kikristo yeye mwenyewe akiwa Mkristo wa Kilutheri katika mjumuisho wa makanisa ya Evangelical yanayohusisha pia makanisa ya Kiprotestanti katika umoja huo.

Merkel pia amewahi kuhusishwa na matukio yenye mkanganyiko aliposhutumiwa kwa kukubali kuhudhuria tuzo za ‘M100’ zilizomzawadia mchoraji, Kurt Westegaard, aliyezua hamkani kwa kuchora katuni iliyowakera Waislamu ulimwenguni ikimwonesha Mtume Muhammad S.A.W.

Pengine ni hulka hizo za Merkel mwenye shingo ngumu asiyetaka kubadilika hata wakati taifa hilo liliposhambuliwa mara nne mfululizo na magaidi hivi karibuni, zitakazopelekea anguko lake kisiasa ingawa kwa uzoefu wake ni mmojawapo wa wanasiasa wa kike mahiri duniani.

Ameinukia kutoka ngazi ya uwakilishi bungeni na kushika nafasi mbalimbali za uwaziri ukiwemo wa vijana na wanawake (1991), mazingira (1994) na kuwa Katibu Mkuu wa CDU kabla ya mwaka 2005 kuwa mwanamke wa kwanza kuchaguliwa kuwa Kansela.

Kimataifa amewahi kuhudumu katika nafasi ya Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya. Ni suala la kusubiri kushuhudia kama mwanamke huyu mwenye msimamo usiotikisika anayetumia jina la mumewe wa zamani, Ulrich Merkel wa ndoa yake ya kwanza, ambaye kwa sasa ni mke wa Joachim Sauer ambaye hajazaa lakini ana familia ya watoto wawili wa kambo kwa mumewe, atabadili msimamo kutokana na mbinyo wa kukubalika kisiasa au atashikilia msimamo wake ambao unahatarisha nafasi yake kisiasa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles