24.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

UKAME WASHTUA MAASKOFU KATOLIKI

Mwenyekiti wa Baraza la Maaskofu wa kanisa hilo (TEC), Askofu Tarcsius Ngalalekumtwa
Mwenyekiti wa Baraza la Maaskofu wa kanisa hilo (TEC), Askofu Tarcsius Ngalalekumtwa

EVANS MAGEGE N LEONARD MANG’OHA-DAR ES SALAAM

KANISA Katoliki nchini limewaelekeza waumini wake kufunga, kufanya hija, mikesha na maombi maalumu kwa lengo la kuombea mvua.

Pamoja na hilo, kanisa hilo limewaelekeza viongozi wake kuadhimisha misa kwa lengo hilo hilo.

Maelekezo hayo yametolewa na Mwenyekiti wa Baraza la Maaskofu wa kanisa hilo (TEC), Askofu Tarcsius Ngalalekumtwa, kupitia barua yenye kumbukumbu namba ya TEC/PR/ 1/2017 iliyoandikwa Januari 13, mwaka huu kwenda kwa maaskofu wote wa kanisa hilo.

“Ni kipindi cha mvua za kilimo katika maeneo yetu mengi lakini hali ya hewa siyo ile tuliyoizoea. Mvua hazifiki kuruhusu shughuli zetu za kilimo kuendelea na baadhi ya maeneo tayari yana uhaba mkubwa wa chakula.

“Ninaomba kasi ya sala iwepo pote nchini. Mungu aliyewatunza wana wa Israeli walipokuwa safarini kuelekea nchi ya ahadi kwa kipindi cha miaka 40, atuangalie kwa wema, huruma na upole. Tuombe baraka juu ya kazi zetu za kilimo, tukayapate mazao ya nchi tuweze kumtumikia Mungu kwa mioyo yenye utulivu na shukrani,” inasomeka barua hiyo.

Katika barua hiyo yenye kichwa cha habari ‘Ukame nchini’ ambayo pia ina saini ya Askofu Ngalalekumtwa inawaelekeza viongozi wake kuadhimisha misa za kuomba mvua, kuwepo kwa hija, mfungo, mikesha na maombi maalum kwa lengo hilo huku ikisisitiza kuwa; aombaye hupewa.

Katika hatua nyingine baadhi ya waumini wa Kanisa Katoliki kupitia Jumuiya zao jana asubuhi walieleza kujulishwa juu ya jambo hilo.

Mmoja wa waumini aliyezungumza na gazeti hili alisema wamejulishwa kufanya ibada za kuombea mvua lakini pia nchi na viongozi wake.

Gazeti hili lilimtafuta Askofu Ngalalekumtwa kwa njia ya simu ili kuthibitisha kama tamko hilo ameliandika yeye ambapo alisema: “Mimi nimewaandikia maaskofu basi ndio kazi yangu”.

Askofu Ngalalekumtwa ambaye yupo mkoani Iringa alipoulizwa kama kuna msukumo wowote wa kuandika barua hiyo kwa sasa alijibu kwa kumhoji mwandishi wa habari hizi akisema: “Ulichokisoma ni kweli au si kweli? Kuna mvua au hakuna?”

Wakati Kanisa Katoliki likija na uamuzi huo, Mamlaka ya Utabiri wa Hali ya Hewa nchini (TMA), imesema maeneo mengi yamepata mvua za vuli chini ya wastani na kwa kuchelewa hivyo kuathiri mfumo wa kawaida wa mvua hasa katika maeneo ambayo yamekuwa yakipata mvua mara mbili kwa mwaka.

Kutokana na hilo, Mtaalamu wa kilimo kutoka Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, amewataka wakulima kuacha kulima mahindi na badala yake wajielekeze kwenye mazao yanayostahimili ukame.

Akizungumza na MTANZANIA Jumapili, Meneja Ofisi Kuu ya Utabiri, Samwel Mbuya, alisema kuchelewa kwa mvua hizo ambazo zilitarajiwa kuanza kati ya Septemba na Oktoba mwaka jana katika baadhi ya mikoa nchini, zilisababisha mikoa hiyo kukabiliwa na vipindi virefu vya kiangazi tofauti na ilivyozoeleka.

Aliitaja baadhi ya mikoa iliyokumbwa na ukosefu mkubwa wa mvua uliokwamisha kufanyika kwa shughuli za kilimo ni pamoja na Dar es Salaam, Morogoro na mikoa yote ya Kanda ya Ziwa.

Alisema pia mvua zilizokuwa zikitarajiwa katika baadhi ya maeneo ambayo hupata mvua za vuli kuanzia Novemba zimenyesha kwa kiwango cha chini na kwa kuchelewa.

“Lakini kuanzia Januari hii na Februari tunatarajia mvua za msimu zitaanza hasa katika maeneo ambayo hupata mvua mara moja kwa mwaka lakini zitakuwa za wastani, ambapo kwa mikoa ya Dodoma na Singida kutakuwa na mvua za chini ya wastani hali inayotegemewa pia katika mikoa ya Ruvuma na Mtwara,” alisema Mbuya.

Mbuya alisema maeneo mengi ambayo muda wa mvua za vuli umepita wasitegemee kupata mvua za uhakika na kuwataka wananchi kuendelea kufuatilia taarifa na maangalizo yanayotolewa na TMA ili kufahamu hali ya mwelekeo wa mvua katika siku zijazo.

Aliitaja baadhi ya mikoa inayotarajiwa kupata mvua hizo zinazotarajiwa kunyesha kati ya mwezi huu na ujao kuwa ni pamoja na Tabora, Kigoma, Katavi, Rukwa, Songwe, Mbeya, Njombe na Iringa.

Katika taarifa aliyoitoa kwa gazeti hili ilionyesha kuwa mvua za kati ya Oktoba na Desemba mwaka jana zilinyesha chini ya wastani katika maeneo mengi ya Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki ikijumuisha mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara.

“Mvua za chini ya wastani zimenyesha pia katika maeneo ya ukanda wa Pwani ya Kaskazini mikoa ya Pwani, Dar es Salaam, Tanga, Morogoro, visiwa vya Pemba na Unguja,” ilieleza taarifa hiyo.

Alipotafutwa Mtaalamu wa Kilimo kutoka Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Lilian Mpinga, kuelezea hali hiyo ya mvua na mwelekeo wake katika masuala ya kilimo, aliwataka wananchi kujielekeza kulima mazao yanayostahimili ukame.

“Mazao yanayopaswa kulimwa ni yale yanayostahimili ukame ambayo ni mihogo, viazi vitamu, uwele, mbaazi lakini mazao kama mahindi hayafai kulimwa wakati huu kutokana na kuhitaji kiasi kikubwa cha mvua,” alisema Mpinga.

Awali, Meneja huyo wa TMA akizungumzia hali ya upepo uliokuwa ukivuma baharini kiasi cha kusababisha ajali ya jahazi lililokuwa likitoka Tanga kuelekea Pemba na kukatisha maisha ya zaidi ya watu 12 mwanzoni mwa wiki hii, alisema kwa sasa hali imerejea kawaida.

“Ni kweli kulikuwa na upepo mkali uliosababisha kuwapo kwa mawimbi makubwa na baada ya kuona hali hiyo tulitoa angalizo siku mbili kabla ya siku ya tukio lile ambapo kulikuwa na viashiria vilivyoonyesha kuwapo upepo mkali kati ya Januari 10 na 12.

“Lakini hali imerejea kawaida kama kutakuwa na mabadiliko na kukawa na kuimarika kwa mfumo wa upepo ambao mwanzo ulionekana kuimarika na upepo kuvuma kutoka Kaskazini mwa Bahari ya Hindi tutatoa taarifa,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles