23.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, June 6, 2023

Contact us: [email protected]

Ukaguzi waja kubaini wasioajiri watu wenye ulemavu

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (anayeshughulikia masuala ya watu wenye ulemavu), Ummy Nderiananga amesema wanatarajia kufanya ukaguzi katika maeneo mbalimbali ya kazi ili kuona kama waajiri wanatoa nafasi za ajira kwa watu wenye ulemavu kama Sheria ya Watu Wenye Ulemavu ya mwaka 2010 inavyoelekeza.

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya watu wenye ulemavu, Ummy Nderiananga.

Akizungumza na Mtanzania Digital, Ummy amesema Serikali imekuwa ikijitahidi kutekeleza sheria hiyo ya watu wenye ulemavu namba 9 inayoelekeza kuwa sehemu ya kazi yenye waajiriwa kuanzia 20, asilimia tatu wawe ni wenye ulemavu.

Akitolea mfano wa ajira za walimu zinazotolewa na serikali ambapo kuanzia Januari hadi Juni mwaka huu walimu zaidi ya 6,700 waliajiriwa, walimu 402 walikuwa ni wenye ulemavu.

“Sisi Serikali tunajitahidi katika kila ajira zinazotangazwa lazima watu wenye ulemavu wawepo. Tunaomba sekta binafsi na mashirika nao watuunge mkono, hatutaki tufike kwenye kufungana ndiyo maana tunaendelea kujengeana uwezo na kuweka msisitizo,” amesema Nderiananga.

Kulingana na sheria hiyo atakayebainika amekiuka atalipa faini ya Sh milioni 2, kifungo cha miaka miwili au adhabu zote kwa pamoja.

Hata hivyo Mkurugenzi wa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), Dk. Aggrey Mlimuka, amesema utekelezaji wa sheria hiyo bado ni changamoto, lakini wanaendelea kuwahamasisha wanachama wao kuitekeleza.

“Sisi hatukatai lakini aina ya ajira nayo ni changamoto kwa sababu si kila ajira unaweza kumpa mtu mwenye ulemavu, mfano kama migodini, kwahiyo suala hili bado linataka mjadala zaidi,” amesema Dk. Mlimuka.

Naye Joyce Jumbe mwenye ulemavu wa uziwi na mhitimu wa Shahada ya Sayansi ya Jamii na Uongozi amesema licha ya kuitwa kwenye usaili wa nafasi mbalimbali za kazi lakini amekuwa akikumbana na changamoto ya kukosa mkalimani na hivyo kushindwa kufanya vizuri.

“Niliwahi kuitwa kwenye usaili uliofanyika uwanja wa taifa lakini nilipofika pale hakukuwa na mkalimani kwa ajili yetu, kwahiyo niliwaeleza matatizo yangu wakanipa karatasi niandike. Nilianguka kwenye hatua ya kwanza sikuweza kuingia hatua ya pili,” amesema Joyce.

Utafiti wa Nguvu Kazi Tanzania ambao hufanyika kila baada ya miaka mitano, kwa mwaka 2018 ulionyesha ukosefu wa ajira nchini ulikuwa asilimia 9.7 huku malengo ya Serikali yakiwa ni kupigania ushuke zaidi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
213,303FollowersFollow
568,000SubscribersSubscribe

Latest Articles