Na Mwandishi wetu
Mwandishi wa habari za uchunguzi, Erick Kabendera ambaye yuko rumande kwa mashtaka ya utakatishaji fedha, ametuma ujumbe wakati mama yake mzazi Verdiana Mujwahuzi akiagwa katika kanisa la Chang’ombe jijini Dar es Salaam leo Januari 3 ambao umewaliza waombolezaji wengi.
Katika ujumbe huo uliosomwa na Wakili wake, Jebra Kambole, Kabendera amesema uchungu wa kuondokewa na mama ni mkubwa sana, hasa anapokuwa ameondoka na ameshindwa kumuaga kama ilivyotokea kwake.
Kabla ya kusoma ujumbe huo, Kambole amesema Kabendera alijaribu kuandika ujumbe ambao alitaka niusome mbele ya waombolezaji
“Amepata taabu sana kuandika na kufuta ili kufikisha ujumbe anaoutaka. Ameniambia ametumia na karibu kurasa 20 kuandika ujumbe huu usiku mzima wa jana. Anaandika na kufuta.
“Ndiyo sasa nimejua kwamba kumbe kuna wakati hata waandishi mahiri nao hukwama kuandika! Hatimaye ameweza kuandika kwa ufupi yafuatayo; Naomba niwasomee….
“Kuna Mama mmoja. Anafariki mara moja, msiba mara moja. Uchungu wa kuondokewa na mama ni mkubwa sana, hasa anapokuwa ameondoka na umeshindwa kumuaga kama ilivyotokea kwangu.
“Hata hivyo nimefarijika kwa Watanzania wote walioguswa na msiba huu bila kujali itikadi zao za kisiasa na kidini na kunisaidia kumsitiri Mama yangu.
“Upendo huu umeonyesha nchi ambayo nimeipenda na naipenda kutoka moyoni. Shukrani za dhati ziwafikie watu wote kwa upendo wao na ushiriki wao kufanikisha msiba wa Mama yangu.
“Mwenyezi Mungu na awabariki sana na kuwaongezea pale mlipopunguza kwa ajili yangu. Mtuombee.”