29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

Ujumbe wa amani watawala Idd el Fitr

Na WAANDISHI WETU – DAR/MIKOANI

UJUMBE wa amani na upendo umetawala swala ya Idd el Fitr iliyofanyika jana baada ya Waislamu nchini kuhitimisha ibada ya mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Katika mawaidha yaliyotolewa katika misikiti mbalimbali nchini na baadaye katika Baraza la Idd lililofanyika mkoani Tanga na kuhudhuriwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, ujumbe huo ulitawala miongoni mwa watu waliopata fursa ya kuzungumza.

Akizungumza katika Baraza la Idd, Waziri Mkuu aliwataka Waislamu kuendelea kudumisha amani na upendo hata baada ya kumalizika kwa mwezi mtukufu wa Ramadhani.

 “Mwenyezi Mungu anatufahamisha kuwa lengo la swaumu (kufunga) ni kuwafikisha waumini kwenye kumcha Mungu, kuwaepusha na maasi na kuwaleta karibu zaidi na Mwenyezi Mungu.

“Tumekuwa tukijaza misikiti karibu yote tunayokwenda kuabudu na kuwakumbuka watu kwa kuwapa misaada mbalimbali, tumeendelea kuwa katika namna bora ya kupigiwa mfano, baada ya kumalizika kwa Mwezi Mtukufu tuhakikishe hatutakoma kuendelea na upendo huu,” alisema.

Aliwaasa Waislamu pia kabla ya Ramadhani ijayo waendelee kuishi na wananchi wengine kwa upendo na amani, kutenda mema, kuheshimiana, kutobaguana na kuimarisha umoja miongoni mwao.

“Tunapofurahia kumalizika kwa mwezi mtukufu wa Ramadhani, tuendelee kuyaishi matendo mazuri. Tufuate mafundisho ya Mtume, mathalani suala zima la kuwataka Waislamu kulinda amani.

Utaifa wetu ni jambo la msingi, tuendelee kuvumiliana, kustahimiliana, hususani inapotokea kutoelewana miongoni mwetu,” alisema.

Pia Waziri Mkuu alilitaka Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) kuchukua hatua za makusudi kuhakikisha huduma za maendeleo kama elimu, afya, maji na nyingine zinawafikia watu wengi zaidi. 

“Kitendo wanachokifanya Bakwata kinapaswa kuigwa na kila anayependa maendeleo. Serikali peke yake haina uwezo wa kueneza huduma za elimu na maji katika kila pembe ya nchi hii. 

“Madhehebu ya dini mbalimbali yamekuwa yakijikita kutoa huduma za elimu, afya, maji na miundombinu. Tutumie vizuri misaada tunayopata kutoka kwa wafadhili, lakini na sisi wenyewe tuhamasike kuchangia,” alisema.

MAPAMBANO YA UKIMWI, RUSHWA

Waziri Mkuu aliwataka viongozi wa dini zote kuendelea kuunga mkono mapambano dhidi ya Ukimwi na VVU, hasa kampeni za 90, 90, 90.

Kwa mujibu wa Waziri Mkuu, lengo la kampeni hiyo ni kuhakikisha ifikapo mwaka 2020 asilimia 90 ya Watanzania wanajitambua, asilimia 90 ya waliogundulika wamepata dawa za kufubaza na asilimia 90 ya waliopata dawa wafanikiwe kuvifubaza virusi hivyo.

“Nawakumbusha viongozi wa dini zote kwamba Ukimwi unamaliza nguvu kazi ya taifa, na Waislamu ni miongoni mwa watu wanaokwisha. Ugonjwa huu hauna chanjo wala tiba, vita vyake si vya mtu au taasisi moja. 

“Sisi wanaume tumekuwa wavivu wa kwenda kutambua afya zetu, tumekuwa tukitegemea matokeo ya wenza wetu, wanaume wenzangu twende tukapime, tusitegemee vipimo vya wake zetu. Tunasisitiza hili kwa sababu maambukizi yake yanakuja katika namna tofauti,” alisema.

Kuhusu rushwa, alisema taifa likisimama vizuri kupinga rushwa tutapata maendeleo makubwa na kutaka kila mmoja awe balozi wa kupambana na rushwa. 

Pia alihimiza viongozi kuunga mkono kampeni ya kutokomeza mifuko ya plastiki kwani ina athari kubwa na haiozi kwa zaidi ya miaka 500.

MUFTI

Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir, alitoa wito kwa Waislamu kukubali kubadilika na kuacha mazoea.

Pia aliwataka kuwaombea viongozi wa Serikali na kutumia misikiti na maeneo mbalimbali katika kuombea nchi baraka.

“Katika nyanja zote za elimu, uchumi tuendelee kuendeleza mshikamano, viongozi wa dini na Waislamu tujiwekee njia za kiuchumi ili tusiwe na taabu katika mambo yetu maana mali nayo ina sehemu yake.

Tutii mamlaka za kidini na tuwatii viongozi katika mamlaka ya kiserikali kwa masilahi ya taifa letu kwa sababu sisi ndio taifa lenyewe,” alisema Sheikh Zubeir.

MAKAMBA

Mbunge wa Bumbuli ambaye pia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba, aliwataka Watanzania kuendelea kuwaombea viongozi mbalimbali ili watimize majukumu yao kwa ukamilifu. 

“Kazi zetu ni za kuhukumu masuala ya watu kila siku, mtuombee tuhukumu kwa haki na usawa. Tumechaguliwa, lakini kuongoza kwa mafanikio na hekima kunatokana na kibali cha Mwenyezi Mungu, hivyo naomba mtuombee ili tuongoze kwa busara, hekima na haki.

“Wakati Mwinyi (Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi), anakabidhiwa nafasi kuwa mgombea wa CCM mwaka 1985, alisema anakubali huku akiwa anadeka kwamba nyuma yake wako viongozi wenzake. 

“Sasa na sisi tuliopo katika Serikali tunaomba tudeke kwenu, tudekezwe na dua zenu, dhamira yenu na imani yenu,” alisema Makamba.

MKURUGENZI TAKUKURU

Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (Takukuru), Diwani Athumani, alisema ili nchi iendelee kuwa na amani, utulivu, usalama na maendeleo ya kasi, kuna kila sababu Waislamu na Watanzania wote kuungana pamoja katika mapambano dhidi ya rushwa.

“Rushwa ni dhambi kubwa sana, tunaofanya matendo hayo miongoni mwa Watanzania tukumbuke siku moja tutakwenda kuhukumiwa, na hukumu yake ni motoni.

“Tutachelewesha sana maendeleo yetu kama hatutaungana kupigana kwa nguvu zote vita dhidi ya rsuhwa,” alisema Athumani.

Awali jana asubuhi, Waziri Mkuu akiwa katika Msikiti wa Anwar uliopo Msasani, Dar es Salaam kushiriki swala ya Idd, aliwataka Waislamu wote nchini watumie sikukuu hiyo kutenda mema na kuwakumbuka yatima na wajane.

 “Leo ni siku kubwa na muhimu, Waislamu wanahitimisha mfungo wa mwezi Mtukufu wa Ramadhani na kusherehekea Sikukuu ya Idd el Fitr, hivyo tuendeleze matendo mema,” alisema.

Aliwaasa waumini wa dini hiyo kuwa sasa ni wakati mzuri wa kuimarisha mshikamano miongoni mwao na madhehebu mengine.

DODOMA

Mkoani Dodoma, Sheikh wa mkoa huo, Mustapha Rajabu, aliwataka Watanzania kuendelea kutenda matendo mema, ikiwa ni pamoja na kuwajali mayatima na watu wasiojiweza.

Kauli hiyo aliitoa wakati wa ibada ya swala ya Idd El Fitri.

Alisema ujumbe wa mwezi wa Ramadhani ni Watanzania kuendelea kutenda matendo mema kama waliyokuwa wakiyafanya wakati wa mfungo wa mwezi wa Ramadhani.

“Ujumbe wa Ramadhani ni tuendelee kutenda matendo mema, tuendelee kuhurumiana, kuheshimiana, kujaliana, kusikilizana na kusaidiana kama ilivyokuwa wakati wa mwezi wa Ramadhani,” alisema Sheikh Rajabu.

MOROGORO 

Mkoani Morogoro, waumini wa dini hiyo wametakiwa kuendelea kusaidia jamii hasa wenye maisha duni, kama walivyokuwa wakifanya wakati wa mwezi mtukufu wa  Ramadhani.

Wito huo ulitolewa na Kaimu Sheikh wa Wilaya ya Morogoro Mjini, Mohamedi Masenga,  wakati wa ibada ya swala ya Idd katika Msikiti Mkuu wa Ijumaa wa Boma.

“Kuna haja kuwasaidia wasiokuwa na uwezo, kuanzia masikini, mayatima na mafukara, na misaada hii isiishie mwezi wa Ramadhani tu, bali iendelee katika miezi mingine, kwani wale wenye mahitaji wanahitaji pia hata miezi ambayo siyo ya Ramadhani,” alisema Sheikh Masenga.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles