25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

UJUMBE MZITO WA VIONGOZI WA DINI IJUMAA KUU

 

Na WAANDISHI WETU – DAR/MIKOANI 


VIONGOZI wa dini katika makanisa mbalimbali nchini jana walitumia ibada ya Ijumaa Kuu kutoa ujumbe mzito wakikemea tabia ya kigeugeu, woga, visasi, vinyongo, malumbano na kuhubiri amani, upendo na ushirikiano.

Kauli zao hizo zimekuja katika wiki ambayo imeshuhudia mijadala na hata malumbano, msingi ukiwa ni waraka wa maaskofu 27 wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri nchini (KKKT), ambao pamoja na mambo mengine, uligusa na kuonya mwenendo wa masuala ya uchumi, siasa na kijamii.

Si hilo tu, mijadala na malumbano ya wiki hii ilikolezwa na kauli iliyokuja baadaye ya Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Kardinali Polycarp Pengo, ambaye alilitumia kongamano la vijana lililofanyika Bagamoyo kupinga waraka wa Kwaresma uliotolewa mwanzo kabisa na Kanisa Katoliki, akisema viongozi wa dini hawapaswi kuchanganya siasa na kazi yao ya kitume.

 Askofu Ruwa’ichi: Viongozi wa sasa vigeugeu

Akihubiri katika ibada ya Ijumaa Kuu iliyofanyika katika Kanisa la Ephifania la Parokia ya Bugando, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Mwanza, Mhashamu Juda Thaddeus Ruwa’ichi, alisema viongozi wa sasa ni vigeugeu, akiwafananisha na Pilato na Makuhani kutokana na kushindwa kusimamia ukweli.

Alisema ugeugeu unaowakumba viongozi wa sasa ni jinamizi ambalo wamelirithi kutoka kwa waliowatangulia, ambao ni mapilato, makuhani na mitume.

“Leo tunaadhimisha fumbo la mateso ya Yesu Kristo, ambalo limegawanyika katika awamu tatu, ambazo ni simulizi, kuheshimu msalaba na kukomunika, katika simulizi tumesikia jinsi ambavyo viongozi hao, yaani Pilato, makuhani na mitume walivyokuwa vigeugeu katika matamshi yao.

“Ugeugeu huo haujaisha miongoni mwa binadamu, maana ni jinamizi ambalo linaendelea kuwakumba wengine, ndiyo maana hadi leo bado wapo viongozi ambao ni vigeugeu, leo wanaongea hivi kesho vile, wanashindwa kuusimamia na kuukiri ukweli,” alisema.

Alisema katika masomo ya Ijumaa Kuu imeelezwa jinsi ambavyo Mtume Petro alivyomkana Yesu na kubainisha kuwa, hata leo hii wapo viongozi kuanzia ngazi ya familia, taasisi na mashirika mbalimbali ambao ni Wakristo, lakini wanashindwa kuusimamia ukweli na kuwakana wananchi.

Alisema viongozi hao wanaoukana ukweli wamekuwa wafuasi wa shetani na kuonya kuwa wanapaswa kumfuata Yesu Kristo na kumuaibisha shetani kwa kuusimamia na kuukiri ukweli katika maisha yao yote ya hapa duniani, ili azma ya Mungu ya kumtoa mwanawe wa pekee ateswe na kufa kwa ajili ya wanadamu itimie.

ASKOFU CHENGULA

Kwa upande wake, Askofu wa Kanisa Katoliki, Jimbo la Mbeya, Evarist Chengula, amesema hakuna maana ya kufurahia watu fulani waliochaguliwa ilhali  tunaishi katika hali ya woga.

Askofu Chengula alitoa kauli hiyo jana, wakati akihubiri waumini waliohudhuria   ibada ya Ijumaa Kuu, katika Kanisa la Bikira Maria wa Fatima, Parokia ya Fransisco Asizi ya Mwanjelwa, jijini Mbeya.

Katika mahubiri yake ambayo yalirushwa mubashara na Kito cha Televisheni cha TBC 1, Askofu Chengula alizungumzia mambo matatu yaliyomo kwenye waraka wa Pasaka, ulioandaliwa na maaskofu wa kanisa hilo kwa ajili ya Pasaka ya mwaka huu.

Alisema ujumbe huo uliangalia hali halisi ya Tanzania, ikiwamo ya kisiasa na kijamii, hivyo haukutolewa kwa kumlenga mtu Fulani, bali wale wanafiki ambao wanadai ni Wakristu, lakini hawana misimamo ya Kikristu.

“Mwaka huu kwa ujumbe wetu tumesema  Wakristo wote katika jumuiya ndogondogo  waanze kufikiri mwakani wachague watu wa aina gani na si chama gani,” alisema Askofu Chengula.

Alisema watu kupitia jumuiya ndogondogo wanatakiwa kuonyesha fikra za kuwatambua watu wanaotaka maendeleo na amani, ili watakapokuja kuomba kura za kugombea udiwani au uenyeviti wa vitongoji  wawe wanatambulika.

“Kwa hiyo nasema kila jumuiya ndogondogo za kila parokia waweze kukaa na mapadri wao waongee, watathmini waumini wao ni wa aina gani, kama wapo wapole… ili tuweze na sisi kutimiza azimio la Umoja wa Mataifa (UN) lililofanyika miaka 70 iliyopita kwamba lazima kila mmoja aishi akipatiwa haki, akitendewa haki  na mwisho kuwe na amani.

“Sasa tuangalie, tumetoka mbali, kila mara baada ya uchaguzi tunakimbizana kama sungura na mbwa, hii maana yake nini? Ina maana tunapochagua, hatuchagui mtu  anayeweza kutusaidia? Najua tuna mambo yetu sisi, tuna fikra zetu, tunataka chama fulani ndio kiongoze na kitutendee, badala ya kufikiri wale waliochaguliwa wawe na lengo moja tu la kutupa haki zetu sisi Watanzania na kuishi kwa amani kwa sababu hakuna maana tufurahie watu fulani tuliowachagua, lakini tunaishi katika hali ya woga,” alisema Askofu Chengula.

Alisema watu hawakujiweka wenyewe madarakani, bali wananchi ndio waliowaweka, hivyo katika kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwakani, kwa minajili ya kujenga nchi, wananchi wasiwachague viongozi wale ambao wana roho ya ubinafsi.

“Sisi hatuna ubaya na mtu yeyote, ujumbe ule tumeutoa kwa kujiangalisha wote  kwamba tuanze kujiandaa mwaka 2019 tuchague watu ambao watajenga nchi, unaweza kukosea kwa sababu mawazo ya wanadamu hayana ukamilifu, lakini tujitahidi katika udhaifu wetu tuone na kutambua watu wa tabia nzuri ndio watakuwa viongozi wetu.

“Kila mmoja aende akasimulie huko anakokwenda kwa sababu ni vita ya wote, tukipata viongozi wabaya tunaumia wote, tukipata viongozi wazuri tunapata faida wote, kila mmoja awe ni kiu ya kuona Tanzania inakuwa na upendo na mshikamano kati yetu,” alisema Askofu Chengula.

Aliongeza kwamba, wazo lingine lililotolewa katika ujumbe wa mwaka huu wa maaskofu ni shukrani kwa Mwenyezi Mungu juu ya watumishi wake.

Aidha, aliwataka vijana wasifanane na Pilato, aliyeshindwa kuamua kwamba Yesu anaonewa.

NZIGILWA AHUBURI MSAMAHA

Akiadhimisha ibada hiyo iliyofanyika katika Kanisa la Bikira Maria Mama wa Huruma lililopo Mbezi Beach, Askofu Msaidizi wa Jimbo Katoliki la Dar es Salaam, Eusebius Nzigilwa, aliwataka waumini kuwa na moyo wa huruma, hasa katika kipindi hiki cha kukumbuka mateso ya Yesu Kristo na kuondoa malumbano ili waweze kuiona pepo.

Nzingilwa aliwataka waumini wawe tayari kusamehe kwa wote waliowakosea na kuondoa visasi na vinyongo ambavyo vinaweza kuharibu maisha yao.

“Katika kipindi hiki cha kukumbuka mateso ya Yesu Kristo, tunapaswa kukumbuka matendo ya huruma ambayo yatazidi kutuongezea imani na kuondoa visasi na malumbano katika jamii na familia zetu,” alisema Nzigilwa.

Aliwataka Wakristu kujifunza kukaa kimya ili kuepusha maneno na kumgeukia Kristu ili waweze kumweleza shida zao, jambo ambalo alisema linaweza kuwasaidia wakikutana na huruma yake.

Nzingilwa alimtaka kila mmoja kuweka azimio la kuwa mtetezi kwa wanaoonewa na kamwe wasinyanyase mtu au kumtendea mabaya.

Alisema katika ngazi ya familia lazima kuwe na roho ya msamaha, ili kudumisha amani na utulivu.

 Askofu Mstaafu Lelubu aacha wosia   

Naye Askofu Mkuu Mstaafu wa Jimbo Kuu, Kanisa Katoliki la Arusha, Josaphat Lebulu (75), ameutaka Umoja wa Madhehebu Mkoa wa Arusha uwe chombo cha amani chenye kuleta msamaha palipo na kukosewa.

Wosia huo aliutoa jana kwenye Ibada ya Ijumaa Kuu, iliyofanyika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid na kushirikisha waumuni na viongozi wa madhehebu yote mkoani humo, unaojulikana kama Kanisa la Arusha.

Askofu Lebulu, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Umoja wa Kanisa la Arusha, akisaidiwa na Makamu wake, Askofu Dk. Stanley Hotay wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Dayosisi ya Mount Kilimanjaro (DMK), kizungumza uwanjani hapo kwenye Ibada iliyotanguliwa na maandamano ya waumini kutoka kona za Jiji la Arusha, alilitaka Kanisa kuangalia matunda yanayotokana na kifo cha Yesu Kristo msalabani.

“Kila mtu ni mwenye dhambi aliyesamehewa na Yesu Kristo, fujo zipo na watu wanaotenda dhambi wapo, lakini Yesu Kristo anatutaka tuwe vyombo vya amani.

“Kanisa la Arusha tunatakiwa palipo na chuki tulete mapendo, palipo na kukosewa tulete msamaha na palipo na giza tulete nuru, maana sisi ni watoto wa Kristo,” alisema Askofu Mstaafu Lebulu, ambaye anatarajiwa kuagwa Aprili 8, mwaka huu, kwenye Ibada ya kuwekwa wakfu Askofu Isack Aman, anayechukua nafasi yake.

“Waliomsulubisha Yesu msalabani walikosa maarifa na ukikosa maarifa ya Mungu unakuwa mtu unayeenda kichwa kichwa. Watu wale walikosa maarifa ya kujua Yesu ni nani.

“Walijawa hofu wakidhani Yesu ataleta mapinduzi katika shughuli zao, kukosa maarifa kwao ni sababu moja iliyomuua Yesu. Pia hofu na woga wa kutokuwa tayari kuusimamia ukweli miongoni mwao,” alisema Askofu Lebulu, ambaye alitumia ibada hiyo kuwaaga waumini hao akisema Desemba 27, mwaka jana, aliomba kustaafu, ikiwa ni baada ya kufikisha miaka 75.

MALASUSA AONYA

Kwa upande wake, Askofu wa KKKT Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Dk. Alex Malasusa, amewataka waumini wa kanisa hilo kujipambanua kwa kufahamu mambo mema na mabaya na kuepuka kufanya mambo kwa kufuata makundi ya watu.

Aliyasema hayo katika ibada takatifu ya Ijumaa Kuu, iliyofanyika katika Kanisa la KKKT Usharika wa Azania Front, jijini Dar es Salaam.

Dk. Malasusa alisema hata kifo cha Yesu Kristo kilitokana na Pilato kusikiliza kundi kubwa la watu waliokuwa wakipiga kelele za kutaka Yesu asulubiwe.

“Watu wengi hufanya maamuzi kwa kufuata makundi ya watu yanasema nini, nasi mara nyingi tunaingia katika dhambi kwa kufuata kundi la watu, hata kifo cha Yesu Kristo kiliharakishwa na kundi la watu waliopiga kelele asulubiwe na kuwachanganya viongozi.

“Hivyo ndivyo tunavyoishi leo kwa kufuata makundi ya watu, kwa hiyo lazima Wakristo tujipambanue. Ijumaa Kuu ni zaidi ya kuvaa nguo nyeusi na kutokula baadhi ya chakula,” amesema Askofu Malasusa.

Padri Mapunda: Uchaguzi si vita

Wakati maaskofu hao wakisema hivyo, Padri wa Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph Mukasa, Parokia ya Nyakato, Jimbo Kuu Katoliki la Mwanza, Baptist Mapunda, amesema uchaguzi siyo vita au chuki, lakini kwa sasa hapa nchini umegeuka kuwa vita na mateso.

Akiadhimisha Ibada ya Ijumaa Kuu, Mapunda alisema mamlaka waliyopewa viongozi wa dini huyatazama na kuyatafakari mambo mbalimbali kwa jicho la Mungu, ili kuwasadia waumini, watendaji na viongozi wa serikali kujifunza na kurekebisha matendo yao.

Alisema siyo dhambi kwa viongozi wa dini kuikosoa taasisi yoyote na kuwataka watawala wajifunze kusoma alama za nyakati katika ujumbe unaotolewa kwa Taifa, kwani itawasaidia kutambua linakoelekea.

“Padri amepewa mamlaka ya kutakatifuza ulimwengu, ndiyo maana anapiga chetezo (anafukiza ubani kanisani) na siyo rais, mfalme au wabunge, katika ulimwengu bila dini na imani maisha yanakwenda ndivyo sivyo.

“Hakuna mtu anayeweza kuwa juu ya Yesu, hata kama una madaraka yote duniani, viongozi wa kanisa hawana bunduki wala jeshi, bali ujumbe wa kuwashawishi. Viongozi wa dini wanaona kwa jicho la mbinguni na huwasaidia wanasiasa kujifunza,” alisema.

Alisema maadui wa haki na maendeleo tunao miongoni mwetu, kwa kuwa wapo watu ambao hawapendi ukweli katika jamii yetu, wanapenda kupotosha, hivyo kuwataka Wakristo kusimamia msalaba kama Yesu, licha ya chuki zote wanazokutana nazo.

“Tunaposhindwa tumgeukie Mungu, tumwambie Baba mikononi mwako naiweka roho yangu,” alisema.

Akizungumza juu ya mwenendo wa Taifa, alisema kuna watu wanafungwa gerezani kwa fitina na chuki, huku wengine wakitekwa, kupotea, kunyanyaswa na kuteketea.

“Yesu hakuwa mchochezi, alikuwa msema kweli, sisi ni mali ya Mungu, mali ya Kristo, kwa hiyo Yesu amekuja kuwa kiunganishi cha wanadamu, tuache ukabila kwa sababu undugu wa Watanzania umeanza kuwa na uadui, tuheshimiane tutafakari pamoja.

PADRI MALILO: NAFASI IPO

Naye Kasisi wa Kanisa Kuu la Mtakatifu Albano, Kanisa Kuu la Anglican, Padri Meshaki Malilo, wakati akiendesha misa ya Ijumaa Kuu alisema viongozi wa dini bado wanayo nafasi ya kuweza kushirikiana na serikali kwa kukaa pamoja kujadili mustakabali wa maendeleo ya Taifa.

“Sisi viongozi wa dini tunayo nafasi ya kuwaza kushirikiana na Serikali kwa kukaa pamoja na kushirikiana mustakabali wa maendeleo ya nchi…amani haitokei wala kuzuka tu na uzuri wa amani inategemea wahusika wenyewe wanavyoishi kuilinda, hivyo hivyo maendeleo hayaji bila watu kukaa na kupanga namna gani wanaweza kuyaleta,” alisema Padri Malilo.

Padri Malilo aliwataka waamini kuyaenzi maneno ya mwisho ya Yesu Kristo akiwa msalabani kuhusu kusameheana.

MCHUNGAJI KKKT asisitiza waraka kusomwa

WAKATI  jamii ikiwa ina hamu ya kujua juu ya waraka unaokusudiwa kusomwa katika makanisa ya KKKT, Msaidizi  wa Askofu wa kanisa hilo Dayosisi ya  Iringa, Himidi Saga, amesisitiza kuwa, waraka huo unakusudiwa kusomwa kesho.

Saga  aliyasema haya jana, nje ya Kanisa Kuu la Usharika wa Iringa Mjini, mara baada ya kumalizika kwa ibada ya Ijumaa Kuu. Alisema kuwa, ni  kweli  upo  waraka ambao umetolewa na kanisa hilo kwa makanisa yote kwa ajili ya kusomwa mbele ya waumini wake.

“Kwanza nishukuru kwa ajili ya nafasi ambayo tumepewa kwa ajili ya kumbukumbu ya kifo cha Bwana wetu Yesu Kristo, niombe sana Wakristo wote na wasio Wakristo kuiona siku hii ni njema sana katika kuponya nafsi zao, kwa kuwa kupitia siku hii ndipo tunapata nafasi ya kuweka huzuni zetu mbele za Mungu kanisa letu, Pasaka hii litakuwa na tamko ambalo limesambazwa maeneo mbali mbali.”

Alisema kimsingi, waraka huo wa maaskofu  utasomwa siku ya Jumapili na kwamba siku hiyo ndipo kitajulikana nini kimesemwa na maaskofu kwenye waraka huo, kwani kwa sasa haujafunguliwa.

Kwa upande wake, Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Petro, iliyopo Oysterbay, jijini Dar es Salaam, Padri Asizi Mendosa, amewashangaa wanaotengeneza na kuvaa hereni zenye msalaba kwa kusema kuwa, wanapoteza maana yake.

Alisema katika kitabu cha Biblia kimeandika kuwa mtu akitaka kuokoka na aubebe msalaba wake anifuate, hivyo hauwezi kubebwa masikioni.

“Nashangaa sasa watu wanatengeneza na kuvaa msalaba masikioni, sijui ni nani ameamua kufanya hivi na kupoteza maana halisi ya neno msalaba,” alisema Mendosa.

Alisema msalaba ni tumaini kwa wagonjwa na wenye shida mbalimbali, hivyo si rahisi kuubeba katika masikio.

“Hapo awali msalaba ulimaanisha ni kushindwa na kudharaulika, lakini sasa maana yake ni ushindi na matumaini mapya,” alisema Padri Mendosa.

Alisema ushindi uliopatikana msalabani baada ya Yesu Kristo kufufuka umebadilisha maana ya msalaba na hivyo Wakristo wanastahili kuuheshimu.

“Msalaba ni ukombozi kwa watu wanaoishi katika dunia isiyo na usawa na uonevu wa kila aina,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles