Ujerumani
Ujerumani itasitisha ushiriki wake katika operesheni ya Umoja wa Ulaya (EU), Sophia inayopambana na biashara haramu ya usafirishaji binadamu katika bahari ya Mediterenia.
Uamuzi huo umetokana na msimamo mkali kuelekea wakimbizi wanaoingia Italia.
Afisa wa ngazi ya juu katika jeshi la Ujerumani, Bundeswehr Eberhard Zorn, ameileza kamati ya bunge ya ulinzi na masuala ya kigeni kuwa Ujerumani, haitotuma chombo chochote cha majini ili kuchukua nafasi ya manowari ya Augsburg, nje ya pwani ya Libya mapema mwezi ujao.
Waziri wa mambo ya ndani wa Italia Matteo Salvini, amejibu kwa haraka juu ya uamuzi huo akisema nia ya operesheni Sophia ilikuwa tu kuwapeleka wahamiaji wote Italia.
Watu wapatao 50,000 wamewasili Italia kama sehemu ya operesheni hiyo.Salvini, anasema kuwa ikiwa nchi nyingine itajiondoa hilo sio tatizo la Italia.
Operesheni Sophia pia inahusisha mafunzo kwa walinzi wa pwani wa Libya.