Na Khamis Mkotya, aliyekuwa Singida,
MRADI wa Backbone unaohusu ujenzi wa njia kuu ya umeme yenye msongo wa Kilovolti 400 kutoka Iringa hadi Shinyanga sasa umekamilika.
Mradi huo wenye urefu wa kilomita 670 umekamilika baada ya kipande cha kutoka Dodoma hadi Singida kilichokuwa kimesalia kuwashwa Desemba 22, mwaka huu na kuingizwa katika gridi ya taifa.
Kipande hicho chenye urefu wa kilomita 217 kilikamilika wiki iliyopita baada ya kukamilisha taratibu za kiufundi zilizosababisha kipande hicho kuchelewa kuwashwa tofauti na vipande vingine.
Uwashaji wa umeme katika kipande hicho ulifanywa na wahandishi wa Shirika la Umeme (Tanesco), chini ya Meneja Mradi wa Backbone, Mhandisi Oscar Kanyama, anayesimamia njia ya Singida hadi Shinyanga.
Uwashwaji huo pia ulishuhudiwa na timu ya wahariri wa vyombo vya habari walikuwa katika ziara kukagua mradi huo mkubwa wenye lengo la kuimarisha mfumo wa gridi ya taifa na kuondoa tatizo la kukatika umeme mara kwa mara.
“Ujenzi umechelewa kwenye kipande hiki kutokana na matatizo ya kifedha yaliyokuwa yanamkabili mkandarasi M/s JYOTI Structures Ltd wakati wa ujenzi,” alisema Kanyama.
Awali akizungumza na wahariri hao, Meneja Mradi, Mhandisi Khalid James alisema kukamilika kwa mradi huo ni mwarubaini wa matatizo ya umeme nchini.
“Kwa hivi sasa ujenzi wa umeme wenye msongo wa Kilovolti 400 kutoka Iringa hadi Dodoma, Singida hadi Shinyanga pamoja na upanuzi wa vituo vya kupozea umeme kwenye miji hiyo umekamilika kwa asilimia 100.
“Kukamilika kwa vipande hivi vya laini kumeboresha usafirishaji na upatikanaji wa umeme ulio bora kwenye mikoa ya kanda yote kanda ya kati, kaskazini, kanda ya ziwa na kaskazini magharibi mwa Tanzania,” alisema.
Mradi huo pia unatarajiwa kuiunganisha gridi ya Taifa na gridi za nchi nyingine za Afrika lengo likiwa ni kukuza ushirikiano wa kiuchumi na maendeleo.
Katika utekelezaji wa mradi huo, Serikali imetumia Sh bilioni 23 kwa ajili ya kuwalipa fidia wananchi waliohamishwa kupisha mradi huo.
James alisema kazi ya kuwaunganishia umeme wananchi wa vijiji 121 itaanza mapema mwakani, baada ya kukamilika kwa mchakato wa kuwapata wakandarasi inayofanywa baina ya Tanesco na REA.
Mradi huo ambao umehusisha ujenzi wa minara 1,747 ya aina mbalimbali kutoka Iringa hadi Shinyanga ni wa kwanza kufanyika nchini katika kuweka mfumo imara wa usafirishaji ili kuwa na umeme wa uhakika.
Alisema mradi huo ambao ujenzi wake ulianza Novemba 2013 hadi sasa umekamilika kwa asilimia 100 ikiwa ndani ya bajeti.