29.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 18, 2024

Contact us: [email protected]

Ujenzi vyumba vya madarasa shule ya Kabale wamkuna Kiongozi wa Mbio za Mwenge

Na Clara Matimo, Kwimba

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, 2022, Sahili Geraruma, ameonyesha kuridhishwa na uboreshwaji wa miundombinu ya shule ya Msingi Kabale iliyopo wilayani Kwimba mkoani Mwanza kwa gharama ya Sh milioni 121.

Jinsi vyumba vya madarasa katika shule ya Msingi Kabale iliyopo Wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza ambayo ilijengwa mwaka 1956 vilivyokuwa kabla ya kufanyiwa ukarabati mkubwa kwa fedha za mapato ya ndani. 

Geraruma ametoa pongezi hizo Julai 12, wakati akizindua mradi huo wa ujenzi wa vyumba sita vya madarasa katika shule hiyo ambayo ipo Kata ya Ng’hundi ambapo ukarabati huo umefanywa na halmashauri ya wilaya ya Kwimba kupitia fedha zake za mapato ya ndani. 

Alisema ujenzi huo uliofanywa unaendana na thamani halisi ya fedha zilizotumika na kwamba watumishi wa halmashauri hiyo ambao walikuwa wakiusimamia mradi huo wamedhihirisha uzalendo na uadilifu wao kwa fedha za umma.

“Majengo haya ya vyumba sita vya madarasa pamoja na madawati 120 ambayo mmetengeneza yanaendana na thamani halisi ya fedha hizo maana yamejengwa kwa kiwango kinachoridhisha kabisa huu ndiyo uzalendo na uadilifu unaotakiwa kwa watumishi wa umma.

“Rai yangu kwa wanafunzi mnaosoma katika shule hii tieni juhudi katika masomo yenu, serikali inayoongozwa na mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, itaendelea kuwatatulia changamoto mbalimbali zinazowakabili katika masomo yenu nanyi walimu timizeni wajibu na majukumu yenu kwa watoto hawa maana w ndiyo tegemeo kwa taifa la kesho,” amesema kiongozi huyo wa mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2022.

Awali akitoa taarifa ya ujenzi wa mradi huo, Mkuu wa Wilaya ya Kwimba, Johari Samizi, amesema Shule ya Msingi Kabale ilianzishwa mwaka 1956 lakini ilikuwa haijawahi kufanyiwa ukarabati mkubwa hali iliyosababisha madarasa kuchakaa sana na nyufa kupasuka kwani kuta zingeweza  kubomoka hivyo kuhatarisha usalama wa wanafunzi na walimu.

Samizi alifafanua kwamba kati ya fedha hizo Sh milioni 121  Sh milioni 7.2 zilitumika kutengeneza madawati 120 ambayo wanafunzi hao watayatumia hivyo kuwaondolea adha ya kukaa chini.

Alitaja manufaa ya kukamilika kwa mradi huo kwamba umepunguza msongamano wa wanafunzi darasani kutoka 147 kwa darasa moja hadi kufikia 74, ongezeko la madawati 190  mpaka 310 ambayo yatachochea na kuongeza ufaulu na unadhifu kwa wanafunzi.

“Pia kukamilika kwa mradi huu kumeboresha mazingira ya kujifunza na kufundishia kwani shule imekuwa na mazingira ya kuvutia wanafunzi katika kujifunza hivyo kwa dhati kabisa tunatoa shukrani zetu kwa Rais wetu mpendwa Samia Suluhu Hassan kwa kujali wananchi wake wakiwemo watoto wetu wanafunzi,” amesema mkuu huyo wa wilaya.

“Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2022 katika Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba ulizindua miradi mitatu, uliweka mawe ya msingi na kukagua miradi katika sekta za elimu, ardhi, maji, afya, ujenzi wa barabara na kuwawezesha vijana kiuchumi yenye thamani ya Sh bilioni 3.83

Kauli mbiu ya Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2022 inasema ‘Sensa ni Msingi wa Mpango wa Maendeleo, Shiriki kuhesabiwa Tuyafikie Malengo ya Taifa’.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles