24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 30, 2023

Contact us: [email protected]

Ujenzi SGR wafikia asilimia 36

Na NORA DAMIAN-PWANIZAIDI ya kilomita 15 za kipande cha reli ya kisasa (SGR) kati ya Dar es Salaam na Morogoro tayari zimeshatandikwa reli.

Kipande hicho chenye urefu wa kilomita 300 kilianza kujengwa Mei 2, 2017 na kinatarajiwa kukamilika Novemba 2, 2019.

Akizungumza na waandishi wa habari jana wakati wa kukagua ujenzi huo, Meneja Mradi (Dar es Salaam – Morogoro), Mhandisi Machibya Masanja, alisema ujenzi katika kipande hicho umefikia asilimia 36 na wanatarajia watamaliza katika muda uliopangwa.

“Tunaendelea vizuri na kama mnavyoona, katika maeneo ambako tuta limetandikwa tumeanza kupanda nyasi maalumu kuzuia mmomonyoko wa udongo,” alisema Masanja.

Alisema reli inayojengwa yenye upana wa mita 1,435 ndio mfumo unaotumika sasa ukikadiriwa kuchukua asilimia 50 ya mitandao ya reli duniani.

Katika kipande cha Dar es Salaam – Morogoro, mbali ya kazi ya kutandika reli kazi zingine zinazoendelea ni ujenzi wa madaraja, makaravati, kuzalisha mataruma, ujenzi wa miundombinu ya ishara ya mawasiliano na nguzo za umeme.

Kwa upande wa mataruma, uzalishaji umeanza katika kiwanda kilichopo eneo la Soga mkoani Pwani.

Kwa mujibu wa meneja huyo, kiwanda hicho kinatarajia kuzalisha mataruma 1,200,400 kwa kipande cha Dar es Salaam – Makutupora.

Alifafanua kuwa kwa kipande cha Dar es Salaam – Morogoro wanatarajia kuzalisha mataruma 500,100 na kipande cha Morogoro – Makutupora watazalisha mataruma 703,300.

“Mataruma tunazalisha hapa nchini kwa kutumia malighafi kutoka katika viwanda vyetu. Taruma moja lina uzito wa kilo 380 hivyo, tunahitaji saruji nyingi na tunapeleka mchango katika viwanda vyetu,” alisema.

Aidha katika eneo la Mzenga na Mlandizi, ujenzi wa makutano ya barabara na reli kuwezesha watu na magari kuvuka kwenda upande mwingine tayari umekamilika ambapo barabara itapita chini na treni juu.

Kwa mujibu wa meneja mradi huyo, vivuko viko 32 na kati ya hivyo vitano ni vya reli na reli, makaravati 243, madaraja ya kati 26 na daraja refu kuliko yote (kilomita 2.54) linalojengwa Stesheni ya Dar es Salaam.

Alisema stesheni ziko sita na stesheni kubwa zitakuwa Dar es Salaam na Morogoro wakati stesheni ndogo zitakuwa Pugu, Soga, Ruvu na Ngerengere.

“Stesheni zetu zimesanifiwa kwa kufuata mazingira halisi ya nchi yetu, Dar es Salaam itakuwa na umbo la Tanzanite ya Morogoro imechanganywa kwa nyumba za asili na Milima ya Uluguru.

“Stesheni zingine zimefuata nyumba zetu za asili na vilemba vya wanawake vinavyovaliwa kwenye nyumba za kifalme,” alisema.

Hata hivyo alisema katika Bonde la Mto Ruvu kuna changamoto ya udongo wa mfinyanzi na kwamba wamekata kina cha mita 2.5 kwa ajili ya kuweka mawe na kuboresha udongo ili kujenga tuta imara la reli.

Katika eneo hilo pia kutajengwa madaraja kati ya matano hadi sita.

Naye Mhandisi katika Stesheni ya Pugu, Lazaro Mwakyusa, alisema wako katika hatua ya awali ya ujenzi ambao umebuniwa kwa utamaduni wa Kiafrika.

Mmoja wa wafanyakazi Shabani Kopwe, ambaye alikutwa akisuka nondo za kutengeneza mirunda itakayounganishwa kwenye Daraja la Dar es Salaam – Ilala, alisema mradi huo umemuongezea ujuzi wa kiufundi.

“Nafurahi kufanya kazi katika mradi huu kwa sababu hata ukiisha nikirudi mtaani, nitakuwa fundi bora zaidi ya nilivyokuwa awali,”alisema Kopwe.

Katika daraja hilo inahitajika mirunda 506 itakayowekwa hadi eneo la Majumba Sita na vijana hao tayari wametengeneza 120.

Fundi mwingine Mohamed Nassoro, aliipongeza Serikali kwa kubuni mradi huo ambao umemwezesha kupata ajira.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
211,285FollowersFollow
564,000SubscribersSubscribe

Latest Articles