26.9 C
Dar es Salaam
Friday, January 3, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Ujenzi reli ya SGR ulipofikia

Na NORA DAMIAN

-DAR ES SALAAM

NCHI nyingi zilizoendelea duniani zinatumia reli kuchochea ukuaji uchumi na biashara kwa sababu usafirishaji kwa kutumia njia hiyo una uwezo wa kubeba mizigo mikubwa kwa mara moja na kwa gharama nafuu kulinganisha na aina nyingine za usafirishaji.

Hapa nchini Serikali imedhamiria kujenga Reli ya Kisasa (SGR) kwa kiwango cha kimataifa na Shirika la Reli Tanzania (TRC) ndilo limepewa dhamana ya kusimamia mradi huo.

Reli inayojengwa (Standard Gauge), yenye upana wa mita 1,435 ndio mfumo unaotumika sasa ukikadiriwa kuchukua asilimia 50 ya mitandao ya reli duniani.

Makala haya yanaangazia maendeleo ya mradi wa ujenzi wa reli hiyo kwa kipande cha Dar es Salaam hadi Morogoro na Morogoro hadi Makutupora.

Kulingana na mpango kazi Mradi wa SGR kutoka Dar es Salaam hadi Makutupora (Manyoni), unatazamiwa uwe umekamilika ifikapo Februari 2021.

Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Masanja Kadogosa, anasema kipande cha kwanza kati ya Dar es Salaam na Morogoro (kilomita 300), kilianza kujengwa Mei 2, 2017 na kitakamilika ifikapo Novemba 2, 2019 kwa gharama ya Sh trilioni 2.7.

Kipande cha Morogoro -Makutupora (kilomita 422), kilianza kujengwa Februari 26, 2018 na kitakamilika baada ya miezi 36 yaani Februari 25, 2021 kwa gharama ya Sh trilioni 4.4.

“Utandikaji wa reli umeshaanza hadi sasa zaidi kilomita 15 zimetandikwa. Tani 7,250 za reli sawa na urefu wa kilomita 60 zimeshapokelewa na zinaendelea kutumika katika utandikaji huo.

“Oktoba 23 tulipokea meli moja yenye tani 6,500 sawa na urefu wa kilomita 54,” anasema Kadogosa.

Meneja Mradi kwa kipande cha Dar es Salaam – Morogoro, Machibya Masanja, anasema ujenzi katika kipande hicho umefikia asilimia 36 na wanatarajia watamaliza katika muda uliopangwa.

“Tunaendelea vizuri na katika maeneo ambako tuta limetandikwa tumeanza kupanda nyasi maalumu kuzuia mmomonyoko wa udongo,” anasema Masanja.

Katika kipande cha Dar es Salaam – Morogoro, mbali ya kazi ya kutandika reli kazi nyingine zinazoendelea ni ujenzi wa madaraja, makaravati, kuzalisha mataruma, ujenzi wa miundombinu ya ishara ya mawasiliano na nguzo za umeme.

Kwa upande wa mataruma uzalishaji umeanza katika kiwanda kilichopo eneo la Soga mkoani Pwani na kiwanda hicho kinatarajia kuzalisha mataruma 1,200,400 kwa kipande cha Dar es Salaam – Makutupora.

Kwa kipande cha Dar es Salaam – Morogoro yatazalishwa mataruma 500,100 na kipande cha Morogoro – Makutupora mataruma 703,300.

“Mataruma tunazalisha hapa nchini kwa kutumia malighafi kutoka katika viwanda vyetu. Taruma moja lina uzito wa kilo 380 hivyo tunahitaji saruji nyingi na tunapeleka mchango katika viwanda vyetu,” anasema Masanja.

Katika eneo la Mzenga na Mlandizi ujenzi wa makutano ya barabara na reli kuwezesha watu na magari kuvuka kwenda upande mwingine tayari umekamilika ambapo barabara itapita chini na treni juu.

Masanja anasema kuna vivuko viko 32 na kati ya hivyo vitano ni vya reli na reli, makaravati 243, madaraja ya kati 26 na daraja refu kuliko yote (kilomita 2.54) linalojengwa Stesheni ya Dar es Salaam.

Anasema stesheni ziko sita na stesheni kubwa zitakuwa Dar es Salaam na Morogoro wakati stesheni ndogo zitakuwa Pugu, Soga, Ruvu na Ngerengere.

“Stesheni zetu zimesanifiwa kwa kufuata mazingira halisi ya nchi yetu, Dar es Salaam itakuwa na umbo la Tanzanite ya Morogoro imechanganywa kwa nyumba za asili na Milima ya Uluguru.

“Stesheni nyingine zimefuata nyumba zetu za asili na vilemba vya wanawake vinavyovaliwa kwenye nyumba za kifalme,” anasema.

Naye Mhandisi katika Stesheni ya Pugu, Lazaro Mwakyusa, anasema wako katika hatua ya awali ya ujenzi ambao umebuniwa kwa utamaduni wa Kiafrika.

Kwa kipande cha Morogoro hadi Makutupora, Meneja wa mradi huo, Mhandisi Faustine Kataraia, anasema hadi sasa mradi huo upo katika hatua za awali za ujenzi na umefikia asilimia 4.78.

Kazi zinazoendelea ni usafishaji wa maeneo reli itakapopita, kuondoa udongo usiohitajika na kujaza udongo utakaomudu utengenezaji wa reli, ujazaji wa vifusi, usanifu wa njia ya reli katika milima na utoaji wa ardhi.

Anasema reli hiyo itakuwa na stesheni nane ambapo kubwa zitakuwa mbili (Kilosa na Dodoma) huku ndogo zikiwa Mkata, Udata, Mgandu, Bahi.

Maeneo korofi

Masanja anasema katika Bonde la Mto Ruvu kuna changamoto ya udongo wa mfinyanzi, hivyo wamekata kina cha mita 2.5 kwa ajili ya kuweka mawe na kuboresha udongo ili kujenga tuta imara la reli. Katika eneo hilo pia kutajengwa madaraja sita.

Maeneo mengine korofi yako kwenye Milima ya Kilosa ambayo inatakiwa kupasuliwa kuwezesha treni kupita chini.

Naye Mhandisi Kataraia anasema wanaendelea kufanya utafiti wa miamba katika maeneo hayo na treni itapita chini ya mlima umbali wa kati ya mita 800 hadi 900 na kutokea Mto Mkondoa kisha kuingia upande mwingine wa reli ya zamani.

“Tumeamua reli ipite milimani na kuna kilomita kama saba hadi nane juu ya milima, tutatoboa matundu manne yatakayopita chini ya mlima na tundu refu linalokaribia kilomita moja litapita chini ya mlima na kuungana na daraja linalopita Mto Mkondoa,” anasema Kataraia.

Naye Meneja katika Kambi ya Ujenzi ya Kimambila iliyopo wilayani Kilosa, Timotheo Malima, anasema ufungaji wa mashine ya kusagia kokoto umefikia asilimia 96 na itaanza kazi Desemba 28 mwaka huu. Mashine hiyo itazalisha tani 300 kwa saa moja.

Kwa upande wake Mwakilishi kutoka Mamlaka ya Maji Morogoro (Moruwasa), Bertam Minde, anasema wako kwenye mchakato wa kuyahamisha baadhi ya mabomba ambayo yamepitiwa na mradi huo.

Walionufaika na mradi

Wafanyakazi 6,440 wameajiriwa katika mradi huo ambapo Watanzania ni 6,182 (asilimia 96) na wageni ni 258 (asilimia 4).

Kwa upande wa wataalamu Watanzania ni 189 na 258 ni wageni.

“Ajira 626 za Watanzania wasio na ujuzi na 19 za wenye ujuzi zimepatikana kupitia kampuni za wazawa wanaoshiriki moja kwa moja kwenye mradi,” anasema Kadogosa.

Anasema pia wameanza kujenga uwezo kwa wataalamu wa ndani ili ujenzi wa reli hiyo utakapokamilika kuwe na watu na kuiendesha.

Anasema mafunzo hayo katika nyanja tofauti za uendeshaji wa reli yatatolewa hapa nchini na nje ya nchi huku kukiwa na kipaumbele maalumu kwa madereva wanawake.

“Tusingependa kuona reli hii inakamilika halafu hatuna watu wa kuiendesha. Reli ya kutoka Manyoni hadi Singida (kilomita 86), ilijengwa na watu wa TRC wakati huo, hawa wanaotujengea sasa wataondoka ndio maana tunajenga uwezo wa kitaalamu.

“Na tutatoa kipaumbele maalumu kwa wanawake kwa sababu hata katika madereva wa treni tulionao ‘performance’ yao ni nzuri sana….sina maana kwamba wanaume hawafanyi vizuri ila hakuna kitu cha wanaume tu,” anasema Kadogosa.

Hadi sasa shirika hilo lina madereva wawili tu wanawake na kati ya kanda nne za kihandisi, mbili (Tabora na Kilosa) zinaongozwa na wanawake.

Mmoja wa wafanyakazi, Shabani Kopwe, ambaye alikutwa akisuka nondo za kutengeneza mirunda itakayounganishwa kwenye Daraja la Dar es Salaam – Ilala, anasema mradi huo umemwongezea ujuzi wa kiufundi.

“Nafurahi kufanya kazi katika mradi huu kwa sababu hata ukiisha nikirudi mtaani nitakuwa fundi bora zaidi ya nilivyokuwa awali,” anasema Kopwe.

Katika daraja hilo inahitajika mirunda 506 itakayowekwa hadi eneo la Majumba Sita na vijana hao tayari wametengeneza 120.

Fundi mwingine, Mohamed Nassoro, ameipongeza Serikali kwa kubuni mradi huo ambao umemwezesha kupata ajira.

Naye Petro Olemeleni ambaye ni mlinzi katika Kambi ya Ihumwa iliyopo mkoani Dodoma, anasema atatumia fursa ya kufanya kazi katika mradi huo kujiendeleza kiuchumi.

Katika kambi hiyo vijana 30 kutoka jamii ya Kimasai wamepewa kazi ya ulinzi.

Reli hiyo itakapokamilika itaongeza kasi ya ukuaji wa uchumi hasa katika sekta ya usafirishaji kwani treni moja itakuwa na uwezo wa kusafirisha tani 10,000 sawa na malori 500 yenye uzito wa tani 20 kila moja.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles