24.6 C
Dar es Salaam
Saturday, September 7, 2024

Contact us: [email protected]

Uingereza na sokomoko la Brexit

*Waziri Mkuu Theresa May anajiuzulu Juni 7

OTHMAN MIRAJI, UJERUMANI

BAADA ya kujiri miezi kadhaa ya malumbano ya kuwania madaraka kutokana na mzozo wa Uingereza kujitoa kutoka Umoja wa Ulaya (Brexit), Ijumaa iliyopita Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Theresa May, alitangaza kubwaga manyanga. Juni 7, ataacha kuwa mkuu wa chama tawala cha Conservative na atabaki tu kuwa Mkuu wa Serikali hadi mwisho wa Julai mwaka huu.

Kwamba mrithi wake, bila ya shaka, atakuwa mpinzani wa nchi yake kubakia ndani ya Umoja wa Ulaya, hali hiyo inazusha hofu mpya kwamba kutakuwapo vurumai pale Uingereza itakapojitoa kutoka Umoja huo hapo Oktoba mwaka huu.

“Ninashukuru sana kwamba nimepata uwezo wa kuitumikia nchi hii ninayoipenda,“ alisema May huku macho yake yakilengalenga  akijizuia asibubujikwe na machozi.

Aliyaelezea karibu miaka mitatu iliyopita ya yeye kuwa Waziri Mkuu kuwa ni “heshima kwa maisha yangu“. May ataingizwa katika vitabu vya historia kama Waziri Mkuu aliyetaka kutekeleza zoezi la Uingereza kujitoa kutoka Umoja wa Ulaya na akashindwa. Maisha atabaki anasikitika juu ya kushindwa kwake, alisema katika taarifa yake aliyoisoma kutoka ofisini kwake jijini London.

Alisisitiza kwamba masikilizano juu ya kujitoa Uingereza kutoka Umoja wa Ulaya yataweza tu kuja ikiwa pande zote zitakuwa tayari kulegeza kamba. :Kutafuta kufikia masikilizano ya pamoja si neno chafu. Maisha yanategemea juu ya masikilizano. 

May hajafaulu kulifanya Bunge la Uingereza liunge mkono pendekezo lake la kuusuka ushirikiano baina ya makundi yote bungeni. Makosa yake makubwa ni pale alipoitisha uchaguzi mkuu mpya nchini humo mwaka 2017 ili apate wingi ulio wazi. Alishindwa vibaya katika uchaguzi huo na akabakia anaiongoza serikali ya wachache. Ni kutoka hapo alipoanza kudhoofika kisiasa. Mapatano ya Brexit baina ya London na Brussels (Umoja wa Ulaya) yalishindwa mara tatu kuungwa mkono kwa wingi bungeni. Tarehe ya Uingereza kujitoa kutoka Umoja huo ikabidi iahirishwe mara mbili.

Kujiuzulu kwa Theresa May hakujawashangaza watu wengi. Mbinyo dhidi yake ulizidi mnamo siku chache zilizopita. Siku ya Jumatano alipendekeza mpango wa vifungu kumi ili kutafuta suluhisho, ikiwamo uwezekano wa baadaye iitishwe Kura ya Maoni juu ya Mwafaka wa kujitoa kutoka Umoja wa Ulaya. Wanasiasa wengi wa London hawajakubaliana kabisa na mpango huo, Baraza la Mawaziri likaasi, halijakubaliana na njia iliyofuatwa na Waziri Mkuu kuhusu Brexit. Jioni ya siku hiyo kiongozi wa wabunge wa chama cha Conservative, Andrea Leadsom, alijiuzulu wadhifa wake. Ijumaa Kiongozi wa Chama Kikuu cha Upinzani cha Labour, Jeremy Corbyn, alitoa mwito wa kuitishwa uchaguzi mpya. Alisema si May wala chama cha Conservative anachokiongoza viko katika hali ya kuweza kuitawala nchi hiyo.

Chenyewe chama cha Labour nacho kimegawika sana kuhusu suala la Ulaya. Japokuwa watu wengi katika chama hicho wanakubali iitishwe Kura ya Maoni ya pili ya wananchi kuamua juu ya jambo hilo, lakini Corbyn mwenyewe anatia na kutoa. Anapendelea wananchi waamue juu ya mustakbali wa nchi hiyo kupitia Bunge.

Katika karibu miaka mitatu ya utawala wa May mawaziri na mawaziri wadogo 36 wameiacha serikali yake. Hiyo ni ishara tosha namna mwanamke huyo alivyopata taabu kutawala na alivyopambana na misukosuko mingi.

Sasa kuna ushindani juu ya nani atachukua nafasi ya May. Waziri wa zamani wa Mambo ya Kigeni, Boris Johnson, anatiliwa dau kwamba ana nafasi nzuri ya kushika nafasi hiyo. Anapendwa miongoni mwa watu wa kawaida ndani ya chama chake cha Conservative. Lakini itabidi wabunge wa chama hicho wamteue miongoni mwa wagombea wawili watakaopata kura nyingi, Wagombea wengine wanaotiliwa sana maanani ni Waziri wa zamani wa Masuala ya Brexist, Dominic Raab; Waziri wa Mazingira, Michael Gove; Waziri wa Mambo ya kigeni, Jeremy Hunt; Waziri wa Mambo ya ndani, Sajid Javid; na Waziri wa Misaada ya Maendeleo, Rory Stewart.

Mkuu wa Komisheni ya Umoja wa Ulaya, Jean-Claude Junker, atakayeacha wadhifa huo karibuni, alisikitishwa na kujiuzulu kwa May, huku Kansela Angela Merkel wa Ujerumani, nchi kubwa na tajiri kabisa ndani ya Umoja wa Ulaya, alisema anaiheshimu hatua iliyochukuliwa na May.

Licha ya yote na hasa licha ya kutabiriwa kujiuzulu kwa May mnamo wiki kadhaa zilizopita, ukweli unabakia kwamba hatima ya kisiasa ya  Waziri Mkuu huyo wa pili wa kike katika historia ya Uingereza ni ya kusikitisha. Karibu miaka mitatu amekuwa madarakani, lakini akiangalia nyuma hawezi kudai kwamba ameacha urithi mzuri kwa nchi yake.

Suala la Brexit limekula nguvu zake zote na bado linaning’inia, halijapata suluhu ya mwisho. Kuna pia mkwamo katika siasa za ndani nchini humo na wananchi sasa wanaonekana wamegawika zaidi kuliko wakati wowote mwingine. Ndani ya Bunge la Uingereza kuna vurugu tupu. Kwa hivyo, watu itabidi wamlaumu hasa May na mtindo wa siasa zake. Yeye ni dhamana wa haya yote yaliyotokea. Mambo yalikuwa yasifike hali hii.

Japokuwa hata kama zoezi la kujitoa kutoka Umoja wa Ulaya ni kazi kubwa na methali yake haijawahi kuonekana katika historia na kuwa kama somo, lakini Chama cha Conservative kilikuwa na karata zote mikononi. Mwanzoni kiliposhika serikali kilikuwa na mamlaka yote ya kuweza kuichora njia ya mikakati kwa maslahi ya nchi hiyo kuelekea Brexit. Badala yake ilifuata njia ovyo, isiyotambulika, mara nyingi watu wakishangaa na kujiuzulu nini hasa Uingereza inachotaka kutoka kwa washirika wake wa Ulaya. Bila ya hata kuwapo dharura Uingereza ilijifunga mikono yake yenyewe na mwishowe ilipunguza nafasi yake ya kujipatia faida katika mashauriano.

Kwa miezi kadhaa May alikuwa anatumia maneno kama vile: Kutokuwa na mapatano ni bora kuliko kuwa na mapatano mabaya. Tamko hilo lilifungua njia ya kuenea nadharia ya kuwavutia watu wa siasa rahisi ambazo vichwa ngumu wanaopendelea Brexit kwa miezi wamekuwa wakiwalisha wananchi.

Ni huyo huyo Theresa May ambaye alikuja na mbadala wa uwezekano wa Uingereza kujipatia talaka kutoka Ulaya bila ya mpangilio. Ni hapo ndipo kazi yake ikawa ngumu zaidi. Nini kinachojiri sasa katika kisiwa hicho ni kama mchezo wa tamthilia. Mwisho wake hauonekani.

Nini kitakachofuata sasa? Ni kwa Waingereza kwanza kutanzua suala la uongozi wa nchi yao, Waziri Mkuu mpya kuziambia nchi nyingine za Ulaya nini hasa anataka na kama kweli anaungwa mkono na Bunge la nchi yake juu ya hayo anayoyataka. Pili ni juu ya nchi hizo zote za Ulaya zikubaliane kama zipo tayari kuipa Uingereza zaidi ya kile zilichotoa kwa May hapo kabla. Tukumbuke kwamba Umoja wa Ulaya una nchi 27 zilizobaki na kupata kauli ya pamoja miongoni mwa nchi zote hizo si rahisi. Kila nchi inaangalia maslahi yake.

Waingereza walipoamua kupitia Kura ya Maoni miaka mitatu iliyopita kujitoa kutoka Umoja wa Ulaya walisahau kwamba wanafungua kisanduku cha uchawi. Makosa makubwa aliyafanya Waziri Mkuu wa wakati huo, David Cameron, kuruhusu ipigwe kura hiyo ya maoni na yote sababu ni kwamba alitaka kujiimarishia madaraka ambayo tayari alikuwa nayo. Ugonjwa ni uleule wa kawaida: uchu wa madaraka kwa wanasiasa. Uchawi uliokuwamo ndani ya kijisanduku hicho sasa unaitafuna si tu Uingereza peke yake, lakini pia Ulaya yote.

Ninachoweza tu kusema ni kwamba Uingereza mwaka huu inkabiliwa mbele yake na kiangazi cha joto kali. Ninakusudia si tu kwa upande wa hali ya hewa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles